Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Gimbi Dotto Masaba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuweka mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa hii, pia nimpe pole Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wangu na viongozi wengine waandamizi wanaopitia changamoto zinazoendelea katika Taifa hili. Naamini kabisa kwamba nguvu ya umma iko siku itashinda dola. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kumrudisha Mheshimiwa Spika wetu na kwa uhai ambao anao kwa sasa Mungu aendelee kumjalia na kumpa afya njema ili aweze kuliongoza Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kwa moja naomba niende kwenye Mkoa wangu wa Simiyu nikianza na changamoto ambazo zinaendelea katika Wilaya ya Itilima tarehe 30 Machi, kuna watu ambao wanaishi kandokando ya hifadhi waliuawa na tembo ambao wanazunguka kwenye mashamba ya wananchi. Naomba nitoe masikitiko yangu kwamba Serikali imekuwa ikikaa mbali sana na hawa wananchi ambao wanapata madhara haya na nisikitike kwamba hata kwenye misiba ya haya majanga yanayotokea Serikali haifiki. Mfano ninao kwa hawa wananchi waliofariki tarehe 30 katika kijiji cha Nyantugutu na kijiji cha Longalombogo, hata Mkuu wa Wilaya hakufika kwenye huo msiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana tunapozungumza kwamba kuna kifuta machozi kwa hawa wananchi mfuko wa maafa ambao uko kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu uhakikishe kwamba hawa watu wanapopata madhara kama haya na familia zao Serikali iweze kufumbua macho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili naomba nijielekeze kwenye mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria kwenda Mkoa wa Simiyu.

Waheshimiwa Wabunge walionitangulia kuchangia Mheshimiwa Raphael Chegeni na Mheshimiwa Mashimba Ndaki wamegusia sana kuhusu suala la huu mradi. Mradi huu umekuwa ni kizungumkuti katika Mkoa wetu na nasikitika kwamba naamini kabisa toka uhuru au toka dunia iumbwe wananchi wa Mkoa wa Simiyu hawajawahi kuonja maji ya Ziwa Victoria licha ya kwamba kuna wengine wanaoga kwenye Ziwa Victoria lakini hawajawahi kunywa maji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ieleweke kabisa kwamba mnamuaibisha Mheshimiwia Rais, tunapozungumza kwamba Mheshimiwa Rais anatoka maeneo hayo ya Kanda ya Ziwa Victoria halafu kwenye maeneno yake hakuna maji ni jambo ambalo tunasikitika sana. Kwa hiyo, ninaomba sana mradi huu uharakishwe kwenye bajeti hii ya Serikali muone umuhimu wa kuhakikisha kwamba mradi huo unawafikia, kwani kuwafikia mradi huu haitoshi tu kwamba watanufaika kunywa maji hayo, inatosha pia kuchochea maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji katika mkoa huu. Kwa hiyo, niombe sana Serikali ione umuhimu wa kupeleka mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bado narudi kule kuhusu barabara ya kutoka Bariadi kupitia Makao Meatu kwenda Karatu, Arusha; Serikali ihakikishe kwamba ule ujenzi unakamilishwa kwa wakati muafaka ili kuweza kuchochea maendeleo kwenye Mkoa wetu wa Simiyu kwa lengo la kupeleka maendeleo kwa kasi licha ya kuwa kwamba Mkuu wa Mkoa anapambana kadri Mungu ambavyo anamjaalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukisoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia sana kuhusu suala la kilimo, naomba nijikite kwenye suala la zao la pamba, kwenye zao la pamba lazima tukubaliane kwamba wananchi wamehamasika sana kulima zao la pamba sasa isitoshe tu kuhamasika kulima zao hili la pamba. Naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu itoe bei elekezi mapema ili wananchi hawa wajue kabisa kwamba mwaka 2018 watauza kwa bei ya shilingi ngapi katika zao lao la pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema kwa nini watoe bei elekezi kuna watu kwa sasa wanapita kwenye mashamba ya wakulima na kuwalaghai wananchi kwa bei ambazo wanaziona wao bila kujua kwamba wananchi hawa kuna muda itafika watauza kwa bei stahiki na watapata faida watanufaika na zao lao. Kwa hiyo, ninaomba mtoe kauli ya Serikali kwamba mwaka huu 2018 bei ya pamba ni kiasi gani lakini pia itoe kauli kwa wananchi ambao wanapita kwenye mashamba kwa ajili ya kuwalaghai wananchi hawa na matokeo yake wanashindwa kunufaika na pamba hiyo.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo nataka nichangie ni kuhusu Wilaya ya Itilima, Mheshimiwa Leah Komanya alisimama akauliza kuhusu swali la Hospitali ya Rufaa; mimi naomba nitoe masikitiko kwamba pamoja na kwamba Mheshimiwa mwenzangu anadai kwamba tupate Hospitali ya Rufaa, Mkoa wa Simiyu una Wilaya kama mbili mpya lakini nasikitika kwamba Wilaya hizi hazina hata Hospitali ya Wilaya, hazina Mahakama za Wilaya, hazina Vituo vya Polisi hususani Wilaya ya Itilima ambayo ni miongoni mwa Wilaya kubwa. Wilaya ina kata 22, ina vijiji 102, ina vitongoji 446, imegawanyika katika tarafa nne lakini cha kusikitisha Wilaya ya Itilima haina Hospitali ya Wilaya, haina Mahakama ya Wilaya na tatu, haina Kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi kilichopo kiko nje na Makao Makuu ya Wilaya kwa maana ya kata jirani na hata tarafa jirani. Kwa hiyo, ninaomba sana kwamba angalau kwenye bajeti ya 2018/2019 basi Serikali ione umuhimu angalau kutupatia kimojawapo kati hivi ambavyo nimevitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia kwa umakini sana ni suala la viwanda. Ukisoma kwenye mpango wa bajeti wa mwaka 2018/2019 katika ukurasa wa 12, kifungu cha (8), Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mpango ametueleza kwamba mpaka sasa Serikali ina viwanda 3,600. Pia ukisoma kwenye ripoti ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda ametueleza kwamba tuna viwanda 3,060 ukisoma kwenye ripoti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yeye anasema tuna viwanda 3,306. Sasa wapo watu wanahoji kwamba tunataka kujua viwanda vidogo ni vingapi na viwanda vikubwa ni vingapi, mimi nomba muhoji kwamba hii ni Serikali moja lakini kila mtu ana takwimu za kwake. Kwa hiyo, ni namna gani ambavyo huhitaji kuhoji maswali mengi unahitaji kupata majibu kupitia document na data zao ambazo wanazitoa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeongoza Taifa hili kwa miaka miwili na zaidi lakini naomba niseme kwamba kwa lugha nyepesi ni kwamba tumefanikiwa kuwa na hivi viwanda ambavyo tayari vina takwimu hizi ambazo ninyi mnaweza mkajumlisha mkaona kwamba Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mpango ame-miss vingapi na Mheshimiwa Waziri Mkuu ame-miss vingapi.

Mheshimiwa Spika, turudi kwenye historia ya Mwalimu Nyerere, Mwalimu Nyerere alitawala miaka 24 kwa taarifa ya Dkt. Neville Reuben katika Kigoda cha Mwalimu 2016 amesema kwamba Mwalimu Nyerere alifanikiwa kuwa na viwanda 414 kwa kipindi cha miaka 24 aliyotawala.

Ndugu zangu mnaweza mkaona kwamba hawa ndugu zangu wao wametawala miaka miwili na zaidi wako hapo kwenye hivi viwanda.

Mheshimiwa Spika, kuna Waheshimiwa Wabunge wanahoji kwamba viwanda vidogo ni vingapi na vikubwa vingapi! Waheshimiwa Wabunge nataka niwaambie mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Mazingira, hivi viwanda mnavyovihoji mimi Mjumbe sijawahi kuviona. Sijawahi kuviona kwa sababu hata kwenye ziara ya Kamati ilifaninkiwa kwenda kutembelea SIDO kwenye karakana za SIDO ambazo hata mashine zake zilizoko kule hata watumishi majina yake walishasahau zinaitwaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni namna gani Kamati haishirikishwi ipasavyo kwenye jambo la kufika kwenye hivi viwanda ingawa hivi viwanda ukimsikiliza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda anavijua kwa ufasaha mkubwa, hali kadhalika tumeona namna ambavyo Mheshimiwa Rais kuna maeneo anasema viwanda hivi vipo.