Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kemirembe Rose Julius Lwota

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ya kuzungumza asubuhi hii ya leo. Vile vile niungane na Wabunge wenzangu wote na Watanzania kwa ujumla kwa kukukaribisha tena kwenye Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Timu yake yote kwa hotuba zao nzuri ambazo wametuletea; vile vile nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara ambayo alifanya katika Mkoa wetu wa Mwanza, ziara ambayo imekuwa na mafanikio makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, sitatenda haki kama nitasimama kuchangia hapa leo nisiongelee masuala ya uvuvi ambayo yanaendelea kwenye Mkoa wetu wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla wake. Kumekuwa na tatizo kubwa sana la unyanyasaji wa wavuvi wa Kanda ya Ziwa. Nia ya Serikali ni njema kabisa wote tunafahamu ya kukomesha uvuvi haramu, lakini kinachofanyika sasa hivi ni kinyume na ni mambo ambayo hayapo kabisa hata kwenye sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze Mawaziri, kazi kweli nzuri wanafanya na kubwa lakini kuna watu ambao wapo huko site, kuna task force imeundwa. Hii task force kinachoendelea huko mikoani mwetu, naongelea Mkoa wa Mwanza ni hatari kubwa kabisa kabisa. Nia ya Mheshimiwa Rais wetu ni njema ya kuwaokoa na kuwasaidia wanyonge lakini kinachofanyika ni kuendelea kuwakandamiza na kuwaumiza na kufanya uvuvi usiwepo kabisa kwenye mkoa wetu.

Naomba niweze kukupa mifano ambayo inaendelea kwenye Mkoa wetu wa Mwanza. Ni kweli nyavu zimechomwa ambazo zilikuwa zinajulikana nyavu haramu sawa tumekubali. Hata hivyo, mpaka sasa hivi tunavyoongea hizo nyavu halali ambazo zinatakiwa ziwepo hakuna nyavu. Nyavu zimekuwa kama madawa ya kulevya. Sasa hivi nyavu zinauzwa kwa magendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa watu ambao wako huko site, hiyo task force ambayo naiongelea, wanashika watu, wanawanyanyasa watu, wanakuwa na maskari wanatoza faini ambazo hazipo kwenye sheria wala kanuni wala taratibu yoyote ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mifano; kuna baadhi ya wavuvi ambao wameshikwa na Mheshimiwa Waziri nimshukuru kwa sababu ni msikivu tumeongea naye na anasaidia baadhi ya mambo. Mtu anakamatwa kwenye gari ya samaki anaambiwa hauna koleo la plastiki. Faini ya koleo hili la plastiki ni shilingi milioni tano; na consistency haipo. Mmoja atashikwa leo ataambiwa faini milioni tano, mwingine atashikwa kesho anaambiwa ni shilingi milioni mbili, mwingine anashikwa kesho kutwa anaambiwa faini milioni kumi, tunakwenda wapi kama Taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tunajua ugumu wa ajira uliopo. Watu hawa ni watu ambao wengine niseme ni watu wa chini kweli wanaofanya kazi za uvuvi. Watu hawa wameamua kujiajiri lakini ajira imekuwa ya matatizo. Tumeongea sana humu ndani lakini hiyo operation bado inaendelea na inaendelea kwa nguvu na inaumiza wananchi wetu kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali, kuna haja na umuhimu wa kukaa na kuangalia haya mambo yanayoendelea huko, mambo yanayoendelea ni mabaya ni mabaya, ni mabaya na unyanyasaji wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuongelea suala ya madawa ya kulevya. Niipongeze sana Serikali, imeleta juzi hapa sheria ambayo tumeipitisha ambayo imesaidia kudhibiti na kupunguza madawa ya kulevya kwa kiasi kikubwa sana kwa upande wa Bara. Hata hivyo kwenye hii hotuba ya Kamati ya UKIMWI pia tumeiona kiwango kikubwa sana cha kudhibiti kwa upande wa Bara sasa hivi na kazi kubwa sana inafanyika na watu hawa wa Mamlaka ya Dawa za Kulevya. Hata hivyo kinachoendelea kwa upande wa ndugu zetu upande wa Zanzibar, wafanyabiashara hawa wengi wamehamia upande wa Zanzibar kwa sababu ya sheria kali ambazo zilizowekwa kwa upande wa Bara.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, naiomba sasa Serikali ifike mahali ikae na ndugu zetu wa Zanzibar, waweke sheria ambazo zitakuwa ngumu kwa pande zote mbili ili kama tumeamua kudhibiti na kukabiliana na madawa ya kulevya iwe kwa pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuongelea kuhusu suala la UKIMWI. Asilimia100 za fedha za maendeleo ya fedha za UKIMWI zinatoka nje, sisi kama nchi hatujatenga fedha yoyote ya masuala ya UKIMWI. Kuna haja sasa kama Serikali ifike mahali tuanze kutenga fedha za ndani ili tuweze kuwasaidia Watanzania hao wengi na hili ni janga la kila mmoja wetu. Nadhani kama hatujaguswa binafsi tutakuwa tumeguswa kwa ndugu zetu na familia zetu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kuna haja kama Serikali kujipanga na kutenga fedha za ndani ili tuweze kuendelea kudhibiti na kupunguza maambukizi mapya ambayo yanazidi kuongezeka kwa kasi.

Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali pia kwa kuanzisha huu mfuko wa UKIMWI. Tumeanzisha huu Mfuko na tukatenga fedha bilioni 5.5 kwa mwaka wa fedha 2016/2017, lakini mpaka dakika hii tunayoongea hakuna fedha yoyote ambayo imekwenda. Sasa hawa watu watafanyaje kazi bila kuwa na fedha. Kwa hiyo naona kuna shida na kuna umuhimu sana wa kuliangalia hili ili tuweze kusaidia Watanzania wengi kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, napenda niongelee tena kidogo kuhusu suala la elimu. Research nyingi ambazo zimefanyika, zinaonyesha kuna uhusiano mkubwa sana kati ya sayansi na maendeleo. Leo hii tunavyoongea, si maneno yangu hata ni juzi tu Rais wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamini Wiliam Mkapa amesema elimu yetu inaporomoka; na huu ni ukweli usiopingika. Tunahitaji mjadala mkubwa kama Taifa, tuweze kukaa na kutengeneza mfumo wa elimu.

Mheshimiwa Spika, nia na madhumuni ya nchi yetu ni kutengeneza Tanzania ya viwanda. Hata hivyo, hatuwezi kupata viwanda bila kuwa na wataalam, bila kuwa na Watanzania wenye uelewa mzuri wa kuweza kutimiza azma hii nzuri ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimniwa Spika, hali ya Walimu wetu sasa hivi ni mbaya, motivation ni zero. Wanafanya kazi kwa kwa sababu hawana options nyingine, lakini kiuhalisia wanaenda hawana wanachokifanya kwa sababu maslahi hayapo, maslahi yao bado ni duni, wana madai yao ambayo hayajalipwa kwa muda mrefu. Kwa hiyo ifike mahali sasa kama nchi tutengeneze mfumo mzuri ili kuweza kuwa-motivate hawa watu kwa vile hawa ndio wanaotufundishia watoto wetu.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa nia yake nzuri kabisa ya kuifanya elimu bure, ni kweli elimu bure imepatikana na leo hii tunavyoongea watoto wengi sana wameenda kwenye shule zetu. Hata hivyo wingi wa watoto hao pia umekuwa ni tatizo. Chumba kimoja kinakuwa na watoto zaidi ya mia mbili. Katika hali ya kawaida watoto hawa hawawezi kuelewa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika, tuna upungufu mkubwa wa madarasa, tuna upungufu mkubwa wa Walimu wa primary, tuna upungufu mkubwa wa Walimu wa sayansi. Kwa hiyo Waziri wa Elimu atakapokuja kutujibu hapa atueleze kuna mkakati gani wa Serikali wa kuweza kuyabadilisha haya mambo ili tuweze kuwa na elimu bora.

Mheshimiwa Spika, naomba kuzungumzia uwanja wetu wa ndege wa Mkoa wa Mwanza. Wote mnafahamu Mwanza ndilo Jiji la pili kutoka Dar es Salaam, lakini uwanja wetu wa ndege sehemu yetu ya kusubiria abiria kwa kweli inasikitisha, siyo hadhi ya Mkoa wa Mwanza. Naomba tuje tupate mkakati wa Serikali ni lini sasa uwanja huu utarekebishwa na tutatengenezewa kiwanja ambacho kitakuwa na hadhi ya Jiji la pili la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kuna lingine nataka kuzungumzia kuhusu masuala ya nishati ya mkaa. Wote tunafahamu zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanatumia mkaa majumbani kwao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.