Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Monduli
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nianze na suala ambalo limekuwa linazungumzwa sana Bungeni hapa leo, suala linalohusu Muungano wetu kati ya Zanzibar na Tanzania Bara. Inaonesha kabisa kwamba CCM wanataka kuvunja Muungano kwa sababu hawathamini kabisa kazi walizofanya Baba wa Taifa pamoja na Karume. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuamini, yapo matamko mabaya yanayotokea hapa kwa ajili ya kubeza Zanzibar kila siku. Watu tunasikia humu lakini hatujawahi kusikia hata siku moja kiongozi mkubwa wa Kiserikali wala Spika wa Bunge hili au Naibu Spika wamekemea jambo hili. Hili jambo ni hatari sana, watu wanalalamika ndani ya Bunge hili na sisi tumeungana kama Watanzania kwa sababu ya nchi mbili; Zanzibar pamoja na Tanzania Bara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba suala linalohusiana na Muungano wetu kati ya Zanzibar na Tanzania Bara ni vizuri tukaheshimiana ndani ya Bunge hili lakini pia tukawaheshimu wananchi wote; wa Tanzania Bara pamoja na wa Tanzania Visiwani. Wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anakuja kumalizia hotuba yake tunahitaji kauli ya Serikali, inatoa onyo gani kwenye Bunge hili ili kauli za kubeza upande mwingine zisitokee tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote hapa ni Watanzania, lakini tunahitaji kuheshimiana na kukaa pamoja ili kudumisha Muungano wetu. Hatuwezi kudumisha Muungano kama tutaendelea kuona watu wengine ni bora kuliko watu wengine. Jambo hili kwa kweli si jema na halifurahishi na halipendezi, naomba kila mmoja aweze kumheshimu mwenzake. (Makofi)
T A A R I F A . . .
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea taarifa hiyo kwa sababu nahitaji zaidi Muungano.
T A A R I F A . . .
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema mficha maradhi, kifo humuumbua. Sisi hatutaki kifo kituumbue na ndiyo maana tunazungumza, tunasema Muungano ni muhimu kuliko kitu chochote. Kama kweli taarifa anayoitoa ndugu yangu Mheshimiwa Lugola, siku zote wanavyoongea hapa kwa nini hataki kuwaambia Wabunge kwamba acheni kuzungumza maneno haya ni mabaya, mmekaa kimya humu mnashangilia mnafikiri ni jambo jema wakati wenzetu wanaumia na wananchi wa Zanzibar hawajisikii vizuri, kwa hiyo lazima tukemee jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kuzungumzia utawala bora. Katika nchi hii sasa utawala bora haupo kabisa. Huwezi kuamini katika nchi hii leo Waziri anaweza kumuagiza Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, tena kamuagiza kwa barua, lakini hawezi kutekeleza. Hii nchi imekuwa nchi ya namna gani, hakuna utawala bora kabisa yaani sasa hivi Mkuu wa Wilaya ana nguvu kuliko Waziri, Mkuu wa Mkoa ana nguvu kuliko Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mji wetu wa Tunduma kuna mgogoro ambao umekaa kwa muda mrefu sana; kuanzia Agosti, 2017 mpaka leo, Waheshimiwa Madiwani hawajakaa vikao kwa sababu ya amri ya Mkuu wa Wilaya. Wakati anakuja kuzungumza hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu atueleze, Mkuu wa Wilaya ana mamlaka gani ya kuzuia Baraza la Madiwani katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mmoja anajua ukisoma Ibara ya nane (8) kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utaona uanzishaji wa Serikali za Mitaa, ilikuwa ni kupeleka mamlaka na madaraka kwa wananchi wenyewe na ikaeleza kwamba kutakuwa na vyombo madhubuti ambavyo vitakuwa vinasimamia Serikali za Mitaa katika maeneo yao. Leo Mkuu wa Wilaya anakwenda kuzuia Baraza la Madiwani kwenye Mji wa Tunduma lisifanye kazi, Waziri ameandika barua kwamba Baraza la Madiwani liendelee kukaa, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wamegoma wamesema kwamba haitakiwi wakae.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujue sababu ni nini? Pia tunataka tujue kwa nini Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wanakuwa na mamlaka, wanatumia sheria gani? Waziri Mkuu anajua, Waziri wa TAMISEMI anajua, Waziri wa TAMISEMI ameandika barua mbili, zote akilitaka Baraza la Madiwani likae, lakini Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wanakataa. Leo mnasema kwamba utawala bora upo kwenye nchi yetu? Utawala bora hakuna kwenye nchi yetu na leo Mawaziri wengi hawaheshimiki kwa sababu Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wameshapewa madaraka makubwa kuliko Mawaziri wetu, jambo hili linatusumbua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Wakuu wa Wilaya sasa hivi wanawaweka ndani Waheshimiwa Wabunge, akiamua tu anamweka ndani. Juzi hapa Mheshimiwa Mnyeti alikuwa anamwambia Mbunge wa Kiteto kwani Mbunge ana mapembe kuliko wewe, muweke ndani, ukiwaweka ndani mimi najua kwa kuwapeleka. Hizi ni dharau kubwa na inaonesha jinsi gani nchi yetu imeshindwa kuheshimu utawala bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tena kwamba, tusifikiri tutapata uchumi kama hatutajenga demokrasia ya kweli katika nchi hii. Uchumi ni demokrasia, kama hakutakuwa na maafikiano kati ya Watanzania wote; wa Vyama vya Upinzani pamoja na Serikali iliyoko madarakani tusitegemee kwamba, tunaweza tukapata maendeleo katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni ya kwetu wote na si nchi ya mtu mmoja na si nchi ya chama kimoja, wote tuko sawa tunahitaji kupata haki sawa lakini tunashangaa leo Chama cha Mapinduzi wameonekana wao wana haki zaidi kuliko vyama vingine, wana haki zaidi kuliko mtu mwingine yeyote, kitu ambacho tunakuwa tunakosea sana. Tujenge demokrasia ya kweli katika Taifa hili, uchumi wa kweli utajengwa katika Taifa hili, lakini tukiendeleza zana za ubabe zinazoendelea katika nchi hii, tusahau kabisa uchumi wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viko vigezo vingi tunvyoviona sasa hivi. Ukijaribu ukiangalia hata bajeti ya mwaka 2017/218, ukienda kwenye kilimo imetekelezwa kwa asimilia 11, ukienda kwenye madini imetekelezwa kwa asilimia sijui tatu, ukienda kwenye maji imetekelezwa kidogo. Mpaka leo karibu bajeti nzima ya Serikali haijafikia hata ya mwaka jana ya utekelezaji wa asilimia 38 ya shughuli za maendeleo. Leo hii tumekaa hapa tunasema eti nchi inakwenda vizuri au inafanya vizuri wakati hakuna kinachoendelea. Tusifiche ugonjwa kifo kitatuumbua tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza ni kuhusiana na umeme. Nakumbuka sana wakati tunaanzisha gesi katika Taifa hili Serikali ilizunguka nchi nzima kutangaza kwamba kukatika kwa umeme sasa hivi tutasahau na mambo mengine, Watanzania mkae mkao wa kula, anzisheni viwanda umeme unakuja. Leo hakuna anayezungumzia umeme wa gesi tena, watu mmeanza kuleta mradi wa Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Rufiji ili uweze kutekelezeka na kuisha unahitaji shilingi trilioni saba, mwaka huu 2018 tumetenga shilingi bilioni 700 tafsiri yake ni kwamba mradi huu utatekelezwa miaka kumi. Je, Mheshimiwa Rais ambaye anaanzisha mradi huu atakuwepo miaka kumi ijayo. Mradi huu inawezekana ukatekelezwa ndani ya miaka 20 wakati huo shilingi inaendelea kushuka thamani kwa maana hiyo mradi huu unaweza kuja kutekelezwa kwa shilingi trilioni labda 20 mpaka 30, huu mradi tunataka kuharibu fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushauri wetu tulikuwa tunaomba mradi wa gesi ambao umeanzishwa Mtwara hizi shilingi bilioni saba badala ya kupelekwa kule Rufiji zikapelekwa Mtwara ili gesi ile isambazwe Dar es Salam, Morogoro, Tanga na maeneo mengine ili wananchi waendele kutumia umeme ambao unatumia gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakiniā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji.)