Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kipekee kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai aliyotupa sisi sote hapa. Nawashukuru sana wanawake wa Kilimanjaro walionituma kuwawakilisha huku Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri. Niseme hakika wote katika Wizara yake akiwepo Waziri wetu wa Nchi, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Makatibu Wakuu na Naibu Waziri wote wametutendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianzie kwenye ule ukurasa wa 14, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Imerodheshwa pale takribaini Mifuko mitano lakini tunaambiwa jumla programu na Mifuko mingine iko 31 ambayo inawezesha wananchi kwa kutoa mikopo. Hoja yangu ni kwamba, wananchi hao wanaopewa mikopo wakiwemo vijana, wanawake, wajasiriamali hawana elimu ya kukopa. Japo wanapewa hizi hela kwa mkopo lakini elimu yao ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana niliomba elimu kwa wananchi hawa wakiwemo wanawake wa Kilimanjaro na bahati zuri sana tuna Chuo Kikuu cha Ushirika, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu ione sasa ni wakati wa kuzungumza na chuo au na vyuo vinginevyo wakatoa elimu ya kukopa kwa wanawake au wajasiriamali wale wakati vijana wale wa chuo wanakwenda field. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna sababu mikopo inatolewa halafu hairejeshwi. Kuna mifuko ambayo mpaka sasa ikiwemo mfuko uliotoa mabilioni ya JK, hela zile hazikurudi na zile ni revolving funds, zimefika mahali zimekwama, hakuna ufuatiliaji. Niombe Kiti chako na nimuombe Mheshimiwa Spika imefika wakati sasa huku ndani iundwe Tume kufuatilia zile hela za revolving zimefia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nizungumzie usalama wa chakula. Bahati nzuri sana mvua zilizonyesha mwaka uliopita zilikuwa nzuri, chakula kimekuwepo, lakini uhifadhi wa chakula hiki siyo mzuri, wananchi wetu hawana maghala ya kuhifadhi chakula. Tunaambiwa kwamba ifikapo 2025 tutakuwa takribani Watanzania milioni 70 lakini tumejiandaa vipi kuzalisha chakula ambacho tunaweza kutumia na kingine tukahifadhi ili kulisha wananchi wetu? Niombe Wizara ya Kilimo iliangalie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye mifugo. Wananchi wengi wa Tanzania ni wafugaji lakini mifugo mingi ni ile ya kiasili (indigenous) hakuna kuboreshwa kwa mifugo hiyo. Mwaka jana tuliambiwa kwamba Serikali itasaidia mitamba bora na mitamba hii inaweza ikasambazwa kwa wafugaji wa hali ya chini. Naomba kujua mpaka leo tokea mwaka jana ni mitamba mingapi imetolewa kwa wafugaji hao ili tujue imeboreshwa kwa kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo ni mizuri lakini inapozagaa hovyo siyo mizuri kwa sababu inaharibu mazingira. Niipongeze pia Wizara ya Mifugo, Waziri aliyepo madarakani ameweza kudhibiti hilo na mpaka sasa hivi tumesikia migogoro kidogo sana kuhusu wafugaji. Naomba nimpongeze Waziri na Naibu Waziri wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie ujenzi wa viwanda. Kwa kweli tumepewa taarifa kwamba viwanda ni vingi na vinaendelea kuwepo lakini niseme kwamba tunapokwenda kwenye viwanda tuangalie pia teknolojia inayotumika. Sasa hivi imekuwa ngumu kufufua vile viwanda kama Machine Tools, Kiwanda cha Tanzania Bag kule Moshi kwa sababu ya teknolojia iliyokuwa imetumika huko nyuma haikuweza sasa kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana vile viwanda vya Kilimanjaro vifufuliwe na pia vinapokwenda kufufuliwa na kujengwa vipya tutumie sasa teknolojia ambayo ni ya kisasa zaidi. Ni wazi kwamba viwanda vile vinatoa ajira, Kilimanjaro wengi sana walikuwa wanategemea ajira hizo, vijana wetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.