Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dua William Nkurua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda ninukuu ule ukurasa wa 27 ambapo Serikali imesema; “Serikali imeamua kuweka mkazo maalum wa kuyaendeleza mazao matano ya biashara ambayo ni chai, kahawa, korosho, pamba na tumbaku. Lengo ni kuongeza mapato ya wakulima.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na wazo hili zuri la Serikali kwa sababu kama tutafanikiwa ni hakika kwamba tutakuwa tumewakomboa wananchi kwa sababu asilimia kubwa ya Watanzania wanategemea kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nina hofu katika eneo hili hasa katia zao la korosho. Ili korosho izalishwe, jambo kubwa kwa Serikali ni kuhakikisha kwamba pembejeo inapatikana kwa haraka na kwa wakati jambo ambalo kwa sasa nina mashaka halitafanyika kwa sababu ili korosho zipatikane mapema ni lazima mwezi wa tano wananchi waanze kupulizia sulphur, lakini mpaka sasa mimi kama Mbunge na wananchi hatujui ni lini sulphur itapatikana, itatolewa bure kama mwaka jana au itanunuliwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali haijaweka wazi namna gani wananchi watapata sulphur. Hilo ni tatizo ambalo nina uhakika lengo la Serikali ambalo limendikwa hapa halitafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kwamba, korosho ina utaratibu wake, sisi kama wakulima wa korosho, korosho inapokwenda nje inatozwa export levy na ile export levy ina utaratibu iliwekewa, 65% ya export levy inakwenda kuendeleza zao la korosho na 35% inabaki kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Lakini mpaka leo ile 65% ya wananchi haijaenda. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba, korosho mwaka huu hazitakwenda vizuri kwa sababu pesa ambayo ingekwenda kueneza zao la korosho haijaenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baya zaidi ile ni sheria ambayo ilitungwa katika Bunge hili kwamba 65% lazima iende Bodi ya Korosho, ili ikaendeleze korosho. Kwa hiyo, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu iangalie vizuri imuambie Waziri wa Fedha apeleke pesa 65% ya hizo ambayo ni shilingi bilioni 110 iende kwa wakulima wa korosho kwa sababu ni ya kwao kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, namkumbusha Waziri wa Fedha asivunje Sheria ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea hapa inakuwa kama tunakuwa na tamaa ya hizi fedha. Na hapa nakumbuka ile hadithi ya babu yangu aliyonieleza kwamba, kulikuwa na mzee alikuwa na shida ya fedha, alipomuomba Mwenyezi Mungu akampa kuku anayetaga yai la dhahabu kwa hiyo, kila siku alikuwa anapata yai la dhahabu. Huyu mzee akaingia tamaa akaamua kumkamata yule kuku na kumkamua, ili apate mayai mengi kuku akafa na ikawa ndio mwisho wa kupata fedha, kupata mayai ya dhahabu. Sasa hii tamaa ya Serikali ya kuangalia ile pesa itauwa zao la korosho; huo ni ushauri naomba Ofisi ya Waziri Mkuu izingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni suala la maji, Serikali kweli imekusidia kuhakikisha kwamba wananchi tunapata maji safi na salama hasa katka miji mikuu na vijiji vyetu. Lakini nataka niishauri Wizara ya maji, kule Nanyumbu Serikali ilishafanya upembuzi yakinifu wa kutoa maji mto Ruvuma mpaka Mji Mkuu wa Wilaya yetu ambapo ni Mangaka. Upembuzi yakinifu ulianza 2015 mpaka leo hatujapata majibu. Sasa kwa hali hii wananchi hawajui kinachoendelea na wananchi wanataka kujua Serikali yao itawatekelezea vipi huu mradi wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali, hasa Waziri wa Maji, ninakuamini sana katika utendaji wako na nilikupeleka mpaka kwenye chanzo cha maji pale Mto Ruvuma ambako maji yatatoka kuja Mjini Mangaka. Lakini mpaka leo wananchi wanashindwa kujua kitu gani kinaendelea, naiomba Serikali ihakikishe kwamba huu mradi mkubwa wa maji ambao Serikali inataka kuuleta pale Mjini Mangaka unaufuatilia vizuri na unausimamia na hatimaye wananchi wanapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni umeme; umeme, kama nchi tunasema kwamba, tunatembea kwa 60% labda, vijiji veytu vinapata umeme labda 60%. Sasa hofu yangu ni kwamba hatugawi huu umeme vizuri kwa mtawanyiko ulio sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri REA yafuatayo, kama inataka kuutawanya umeme vijijini tutembee kwa asilimia inayofanana, tukisema Taifa tumepeleka umeme vijijini kwa 60% basi tuwe tumekaribiana, lakini kwa mfano leo Nanyumbu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.