Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na usalama na leo tumekutana hapa tukiwa na afya njema ili kuweza kujadili masuala yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza sana Mtukufu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna anavyoiendesha nchi yetu mpaka sasa, kwa ukusanyaji mzuri na uongozi mzuri katika kipindi kifupi alichokua madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani zangu pia nizielekeze kwa ndugu yangu, Komredi, Mheshimiwa Waziri Mwigulu pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Olenasha, kwa kazi nzuri na hotuba nzuri waliyoiwasilisha leo asubuhi hapa. Combination yao ni nzuri sana na tunawategemea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee niendelee kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Jimbo langu la Mafia kwa kunichagua na kuendelea kuniamini niweze kuwaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Kwa kusisitiza hili, ninayo furaha kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba ile x-ray machine na ultrasound machine ambazo niliziahidi katika kampeni yangu, zimeshatoka bandarini na zinaelekea Mafia mwisho wa wiki hii, zitakuwa Mafia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nukta hii, namshukuru sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kuweza kutusaidia kupata vibali muhimu vya TFDA na leo x-ray machine na ultra sound, tayari zinaelekea Mafia mwisho wa wiki hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru pia Taasisi ya MIDEF ambayo ndiyo iliyo-donate mashine hizi kwa Jimbo la Mafia. Na mimi mwenyewe pia nijipongeze kwa ushindi mkubwa nilioupata kwenye uchaguzi na kwenye kesi iliyofunguliwa na mgombea wa chama cha CUF. Nimeshinda, akakata rufaa na nimeshinda tena. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia hotuba ya Waziri wa Kilimo.
Kwa upande wa Jimbo la Mafia, uchumi wa Jimbo la Mafia umebebwa na uvuvi na utalii. Kwa masikitiko makubwa sana kuna taasisi ya Serikali maarufu kama Marine Park, badala ya kuwa msaada kwa wananchi wa Mafia imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Mafia. Taasisi hii ya Marine Park, ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, naomba sana na utakapohitimisha nitahitaji kusikia kauli kutoka kwako kuhusiana na Marine Park.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wanatudhulumu watu wa Mafia kwenye mgao unaotokana na mapato ya watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 70 wanachukua Marine Park na asilimia 30 ambapo 10 zinakwenda kwenye Halmashauri na asilimia 20 inakwenda kwa vijiji husika ambavyo watalii wale wanakwenda. Mgao huu siyo sawa ukizingatia maeneo mengine kama Hifadhi ya Wanyamapori ambapo wananchi wa maeneo husika wanapata asilimia 60 na Serikali Kuu inapata asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inapokuja kwenye Marine Park, wamekuwa wakitudhulumu wananchi wa Mafia. Tumelisema sana hili! Kila ukiongea nao wanakwambia kwamba hii ni sheria, hii ongea na watu wa Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda sana wakati unahitimisha hotuba yako Mheshimiwa, ndugu yangu rafiki yangu Komredi Mwigulu ulitolee maelezo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea suala la Marine Park, watu wa Marine Park wametoka katika kazi yao ya msingi ya uhifadhi na hivi sasa wamekuwa madalali, wanauza ardhi. Visiwa vitatu vya Mafia vidogo vidogo sasa vimeshauzwa na Marine Park. Visiwa hivyo ni Nyororo, Mbarakuni pamoja na Kisiwa cha Shungimbili. Huu mchakato wa kuuza pengine siyo tatizo kubwa sana, tatizo kubwa sana kwa nini hawataki kufuata taratibu? Huwezi ukauza ardhi au kuibinafsisha bila kuwashirikisha wananchi husika wa vijiji vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, kwa masikitiko makubwa sana, watu wa Marine Park wamevibinafsisha visiwa hivi kwa kutengeneza mihtasari fake kuthibisha kwamba wananchi wameshirikishwa. Ukweli ni kwamba wananchi hawajashirikishwa na nyaraka walizo-forge ninazo hapa, nitakuletea kwako hapo ili uzione na uweze kuchukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mgao usio sawia wa maduhuli yanayotokana na watalii, vilevile pesa zinazotolewa pale kwa mujibu wa maelezo yao wenyewe Marine Park wanasema kwamba Marine Park ya Mafia ndiyo inaendesha Marine Park zote Tanzania. Mapato yanayotoka kule, sehemu kubwa yanaendesha Marine Park nyingine za nchi yote. Kisiwa kama Mafia kidogo chenye uchumi mdogo kwenda kukitwisha mzigo wa kuendesha Marine Park zote zilizopo Tanzania, kwa kweli hili siyo sawa. Hata huu mgao wa asilimia 70 wanautoa baada ya kutoa gharama zote, kwa maana ya gharama za uendeshaji. Hii tunaiona pia siyo sawa. Namwomba sana ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, hili nalo aliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tukirudi kwenye suala la uhifadhi wenyewe, Marine Park kazi yao ya uhifadhi yenyewe imewashinda ukianzia Moa, Pwani ya Tanzania mpaka Msimbati kule, mabomu yanapigwa usiku na mchana. Pale Dar es Salaam kuanzia Magogoni pale Ikulu kwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli mpaka Pemba Mnazi, mchana na usiku ni mabomu yanapigwa kama nchi iko kwenye vita. Tunashangaa uhifadhi gani wanaoufanya hawa wa Marine Park. Mheshimiwa Waziri Marine Park ni jipu na ninaomba sana ulitumbue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, mkononi mwangu hapa ninao waraka uliotolewa na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kilimo na Mifugo wakati ule Mheshimiwa John Pombe Magufuli, waraka wa tarehe 12 Agosti, 2008, ukitoa ruhusa kwa wavuvi ambao wamezuiwa wasitumie mitungi ya gesi migongoni mwao wanapokwenda kuvua katika kina kikubwa cha maji. Kina cha mita 50 mtu hawezi kuzamia kwa kuziba pua, ni lazima aende na mtungi wa gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana Marine Park wanawakataza wananchi na wanaendelea kuwakamata. Hivi ninavyozungumza, wapigakura wangu zaidi ya 20 wameswekwa rumande kwa sababu wamevua kwa ya kutumia mitungi ya gesi. Mitungi ya gesi Mheshimiwa Waziri, haiharibu mazingira, inamsaidia mvuvi aweze kwenda kina kikubwa zaidi kwenda kutoa nyavu zake zilizonasa. Haina uhusiano wowote na uharibifu wa mazingira, hata ndugu yangu Makamba anaweza akathibitisha hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo cha mwani, Marine Park...
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.