Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu katika maeneo machache ambayo napenda kupata majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ahadi ambazo Waziri Mkuu amezitoa bado kuna mgogoro wa wananchi wa Kata ya Mngeta, Kijiji cha Ikule na Vitongoji vyake na JKT Chita ambapo Jeshi limechukua ardhi kubwa ya kilimo bila maridhiano wala muhtsari wa Kijiji na JKT Chita kumiliki eneo lote kwa kulichukulia hati Wizara ya Ardhi na kujipa uhalali pasipo wanakijiji kushirikishwa na kusababisha umaskini mkubwa kwa wananchi hasa ukizingatia wote wanategemea kilimo na hawana ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu alinitamkia/ kuwatamkia wawakilishi wa Kijiji/Kata walipofika ofisini kwake Dodoma mwaka 2016 kuwa angeagiza mazungumzo yawepo ili kupata muafaka wa suala hilo ambapo alishauri katika eneo lenye mgogoro ni vema kila mmoja akapata na kupoteza na si kundi moja kutaka kutwaa eneo lote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi niandikapo hakuna utatuzi isipokuwa ni vitisho kwa wananchi. Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa na Waziri wa Ulinzi wameshindwa kusimamia utatuzi wa mgogoro huu isipokuwa ni vitisho. Hali ya wananchi inaendelea kuwa dhaifu kwa kukosa maeneo ya kilimo na kusababisha umaskini mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni tatizo la vijiji viwili vya Idandu na Miyomboni vilivyopo Kata ya Mofu na Namwawala, Jimbo la Mlimba kutoruhusiwa kufanya uchaguzi wa vijiji hivyo tangu mwaka 2014 kwa hoja kuwa eneo hilo ni la uwekezaji na toka wakati huo hakuna aina yoyote ya uwekezaji uliofanyika. Hii inasababisha wananchi kukosa uongozi wa kusimamia au kuhamasisha maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua ni lini sasa Ofisi ya Waziri Mkuu itakwenda kuyapatia ufumbuzi masuala hayo yanayoleta kero kubwa kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.