Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu hasa kwangu zaidi ni ushauri tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naiomba Serikali ichukue hatua ya kufuatilia miradi ya maji, kwa mtazamo wangu eneo hili lina ufisadi mkubwa sana. Miradi mingi inajengwa chini ya kiwango na wakati mwingine haikamiliki kwa wakati. Mfano, Mradi wa Maji Ntomoko, Wilayani Kondoa na Chemba ambapo licha ya Serikali kutoa trilioni mbili hakuna kilichofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni ule wa Kijiji cha Laloda ambapo mkandarasi amelipwa zaidi ya milioni mia tano (Sh.500,000,000) na hakuna hata chembe ya maji inayotoka. Niiambie Serikali ikiwezekana kuunda Tume Maalum kuchunguza miradi mikubwa na midogo ya maji kote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, naiomba Serikali iangalie kwa kina ukubwa wa Bunge letu, uwakilishi wake na dhana ya kubana matumizi. Nchi yetu ina Halmashauri mia moja themanini na tatu (183) na Wilaya zaidi ya 169, lakini idadi ya Wabunge ni 388. Zipo Halmashauri zina Wabunge zaidi ya mmoja na katika Wilaya yupo Mkuu wa Wilaya mmoja tu. Ushauri wangu ni kuiomba Serikali ipunguze utitiri wa majimbo na kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na Mbunge mmoja ili kupunguza gharama na kuhakikisha Bunge linakuwa active kuliko ilivyo sasa ambapo Bunge limekuwa kama mkutano wa hadhara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambasamba na hilo pia nashauri hata utaratibu wa kuwapata Wabunge wa Viti Maalum utazamwe upya. Ushauri wangu ni kwamba kila mkoa uwe na Wabunge wawili wa Viti Maalum na hii itasaidia kupunguza idadi ya Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wabunge kutoka Zanzibar ipo hoja ya kubadilisha utaratibu uliopo sasa na kufanya kila Wilaya ya Zanzibar kuwa na Mbunge mmoja anayewakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano na pia kuwaondoa Wabunge wanaowakilisha Baraza la Wawakilishi wanaohudumu pia Bunge la Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi sioni haja ya kuwa na Wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi kuhudhuria Mikutano ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi kwa wakati mmoja. Naamini kama ushauri huu utazingatiwa Serikali na Taifa litakuwa limepunguza gharama kubwa ya uendeshaji wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ni kuhusu viwanja vya michezo. Viwanja vingi vya michezo nchini vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM). Viwanja hivi vipo katika hali mbaya, nashauri Serikali ishauriane na CCM na ikiwezekana vikodishwe kwa majeshi kama Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo wanaweza kuviendeleza vikawa bora zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.