Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kwa unyenyekevu mkubwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika mahali hapa nami kuchangia hoja hii muhimu iliyoko mbele yetu leo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kama kiongozi wa nchi kwa namna anavyoliongoza Taifa letu katika kutuwekea misingi imara. Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu inatuonesha mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2018/2019, hotuba hii inakwenda kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoainishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuendelea kupambana katika vita dhidi ya rushwa nchini kwetu, hali ilivyo hivi sasa ni ya kuridhisha tofauti na hapo awali, kama taarifa inavyosema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 2017 hadi Machi, 2018, jumla ya majalada 325 yalifanyiwa uchunguzi na TAKUKURU na kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo 214 kati ya hayo yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ukilinganisha kwa idadi ya kesi zilizopelekwa mahakamani na kesi zilizoamuliwa na kwa idadi ya watuhumiwa waliokutwa na hatia, naweza sema bado tunahitaji kuongeza nguvu zaidi ili kuweza kufikia kiwango ambacho kitawafanya wapenda rushwa kuiogopa rushwa na kujikita zaidi katika maadili mema katika utekelezaji wa kazi za kila siku za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali adhabu katika makosa ya rushwa, watu wanapokutwa na hatia kisheria ya rushwa basi adhabu iwe kali ili iwe fundisho kwa watu wengine. Hata hivyo, naipongeza Serikali kupitia TAKUKURU kwa kufuatilia miradi ya maendeleo na kuhakikisha fedha za umma hazipotei na kutumika ipasavyo kama zilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vita dhidi ya madawa ya kulevya imekuwa kwa kiwango cha juu sana kipindi hiki kupitia mamlaka ya kudhibiti na kupambana na madawa ya kulevya na tumekuwa tukishuhudia taarifa mbalimbali za kukamatwa watuhumiwa mbalimbali na baadhi ya wengine hata kujaribu kutoroka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyowahi kuchangia katika Mabunge yaliyopita, vita ya kupambambana na madawa ya kulevya siyo nyepesi, ni vita ngumu sana inayohitaji kuwawezesha kwa namna ya hali ya juu sana Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya, maana watu wanaohusika na biashara hii wana uwezo mkubwa kifedha na wana njia nyingi sana wanazoweza kuzitumia ili tu kufanikisha jambo lao. Hivyo basi ni wajibu wa Serikali kuendelea na kuongeza nguvu katika vita hii iwe endelevu na kukomesha kabisa mtandao huu hapa nchini kwetu ili kuwanusuru vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya, 2015 yaliyofanyika yameleta tija kubwa sana. Niishauri tu Serikali pale itakapoona kuna hoja ya kufanya marekebisho mengine, basi sisi Wabunge tuko tayari kushiriki kwa lengo la kuhakikisha madawa ya kulevya yanakuwa historia katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha na kuongeza huduma ya watumiaji wa dawa za kulevya kwa kutumia methadone katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Temeke na Mwananyamala, ila naiomba Serikali kuongeza juhudi zaidi ili huduma hii iweze kufika mbali zaidi kwa waathirika wa dawa za kulevya wako kila kona ya nchi yetu kuanzia vijijini na maeneo yote ambayo hupatikanaji wa huduma hii ni mgumu, kufanya hivyo kutasaidia sana kuokoa maisha ya vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali katika kuimarisha ulinzi na usalama katika mipaka yetu, hii inatuweka katika usalama zaidi katika kipindi hiki ambacho dunia inapita mapito mbalimbali ya kitahadhari. Vilevile naipongeza kwa kuliwezesha jeshi la polisi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na majeshi yake mengine, bila kulisahau Jeshi la Wananchi kupitia Wizara ya Ulinzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie afya, kwanza niipongeze Serikali kwa kuboresha huduma mbalimbali za kiafya kwa kuanzia na utoaji wa chanjo nchi nzima. Upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba kwa kuongeza bajeti, upatikanaji wa tiba za kibingwa mfano upandikizaji wa figo, vifaa vya kuongeza usikivu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, upasuaji kwa kutumia tundu dogo na kufungua kifua katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa kuwezesha dawa kupatikana kwa wakati na muda wa kupata huduma ya mionzi kupungua, haya na mengine mengi ni baadhi tu ya maboresho katika Sekta ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kila kwenye kupiga hatua hapakosi kasoro mbalimbali, kama ilivyo katika sekta ya hii ya afya kuna changamoto mbalimbali ambazo Serikali haina budi kukabiliana nazo kwa kuzidi kuipa bajeti ya kutosha Wizara ya Afya na kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana nchi nzima na kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya maji nchini imekuwa kubwa sana, Wabunge humu ndani lazima tunakabiliana na changamoto hiyo, ingawa Serikali imeendelea kuweka nguvu kubwa katika sekta ya maji, lakini bado suala la upatikanaji wa maji sehemu mbalimbali za nchi hasa vijijini imekuwa changamoto kubwa sana. Kujenga na kupanua miradi mbalimbali ya maji vijijini itasaidia sana kukabiliana na changamoto hiyo, miradi 71 iliyokamilika bado ni idadi ndogo sana ukilinganisha na miradi inayoendelea kutekelezwa takribani miradi 366.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kuweka sekta ya maji katika vipaumbele vyake kwani inawagusa watu wetu wa hali duni hasa vijijini ndiyo wanaohangaika kukesha kusaka maji. Naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazoendelea nazo katika mipango yake ya kuhakikisha kwa mwaka huu 2018/2019 kukamilisha miradi yake ya maji ipatayo 387 kwenye halmashauri mbalimbali nchini na pia kuanza miradi mipya ya maji vijijini, ni jambo jema lazima tulisemee kwa namna ya kupongeza na kuipa moyo Serikali kwa kuonesha inatambua changamoto hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuziboresha bandari zetu nchi nzima ili kuziwezesha katika hali ya kufanya kazi kwa ufanisi, hasa bandari yetu ya Dar es Salam kuiweka katika ushindani mkubwa na kuiwezesha kupata meli nyingi kuja kushusha mizigo hapa na kuendelea kupokea watumishi kutoka nchi jirani kuitumia bandari yetu, uboreshaji huu ni katika Gati namba moja (1) mpaka saba
(7) kuongeza upana wa lango la kuingilia meli na eneo la kugeuzia meli, sambamba na kuboresha mtandao wa reli bandarini pamoja na kujenga gati maalum la kuhudumia meli zinazoshusha magari, hizi ni hatua nzuri, endelevu kwa manufaa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya Serikali kuja na mpango wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini ni mpango mzuri sana ambao umeweka mgawanyiko wa kimajukumu ,kwani sasa wananchi wa vijiji wamepata wakala wao ambao utakuwa unashughulika na miradi ya barabara za vijijini. Tuseme tu ukweli, wananchi wa vijijini wamekuwa wakisahaulika sana kwa kutokutupiwa jicho la upendeleo, miundombinu imekuwa ni mibovu sana hasa kwa hapa nazungumzia barabara, ambazo zimekuwa hazipitiki na ukiangalia wananchi hawa ndio wazalishaji wa mazao mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa mpango huu basi barabara nyingi za vijijini sasa zitakarabatiwa na kuwapa unafuu wananchi wetu. Hapohapo naipongeza Serikali kwa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) itakayokuwa na urefu wa kilometa 1,219, hadi sasa ujenzi wa kipande cha kutoka Dar es Salam hadi Morogoro kilometa 300 umeanza na unatarajia kukamilika Novemba, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuna mradi mwingine mkubwa ambao umezinduliwa hivi karibuni wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga. Bomba la mafuta hilo la kusafirishia mafuta ghafi litakuwa na urefu wa kilometa 1,445; kati ya hizo kilometa 1,115 zitajengwa nchini Tanzania. Mradi utakuwa na manufaa kwetu sisi kama nchi na wenzetu wa Uganda, hizi ni hatua za Awamu hii ya Tano kwa maendeleo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Elimu ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, tumekuwa tukiona taarifa mbalimbali zikizungumzia sekta hii na Serikali kuchukua hatua mbalimbali pia katika kutatua changamoto ya elimu, lakini lazima Serikali ikaangalia kwa jicho pana zaidi sekta hii ya elimu ili iweze kuendana na dhana nzima ya viwanda ya Serikali hii ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuja na matokeo chanya yenye tija juu ya mustakabali wa elimu yetu, basi itatuwia vigumu sana kufika malengo ya Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.