Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Charles John Tizeba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kwa kuanza kabisa niseme naunga mkono haja.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuunga mkono hoja naomba kwa haraka nitoe ufafanuzi wa baadhi ya michango ya Waheshimiwa Wabunge ambayo inagusa sekta ya kilimo na kwa muktadha huo nitazungumzia korosho, kahawa, pamba, ufuta, mfumo wa uingizaji wa mbolea kwa pamoja na soko la nafaka kama muda utakuwa unatosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwanza jambo la korosho katika namna mbili, moja ni kwa namna gani tumejipanga kuhakikisha kwamba kiatilifu aina ya surphur kinapatikana kwa wakulima wa korosho nchini. Mpaka hivi sasa ninapozungumza Serikali imekwishatoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kulipia advance ya suppliers wa sulphur kwa maeneo yanayozalisha korosho. Fedha hizi imelipwa Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC) ambao wao wataingiza tani 8,000; na sasa hivi wanayo order ya tani 5,000 ambayo itafika mapema mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambasamba na TFC Kampuni ya Bajuta pia imeshapewa zabuni ya kuingiza hiyo sulpha tani 10,000 na wataingiza tani 5,000 mwishoni mwa mwezi huu, tani 5,000 zingine zitaingizwa na kampuni ya dunia mwanzoni mwa mwezi wa tano au katikati ya mwezi wa tano. Kwa hivyo mpaka kufiia tarehe 15 Mei tuna uhakika tutakuwa na tani zisizopungua 15,000 ambazo hizi tutazitumia kwa maeneo ya Lindi ambako ndiko mwanzo kabisa wa upuliziaji unatakiwa kuwapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitoe taarifa tu kwamba ziko tani 4,000 sasa hivi nchini zilizomilikiwa na kampuni ya Expo Trading na tunafanya mazungumzo nao kuhusu bei ili tukikubaliana bei nayo ianze kugaiwa kwa wakulima hasa katika yale maeneo ambayo yanahitaji dawa hiyo haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla Serikali kupitia vyama vya ushirika itaagiza jumla ya tani 35,000 ya sulphur mwaka huu, na tuna hakika kiasi hicho cha sulphur kitawatosha wakulima kwa nini tunajiingiza kuagiza hizi sulphur sasa hivi, hii yote ni kutaka kudhibiti bei ya sulphur ili wakulima waweze kupata nafuu wanapokuwa wananunua dawa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la muhimu hapa nitoe tu taarifa kwamba sulphur mwaka huu kwa wakulima itauzwa na itauzwa kwa bei itakayokuwa controlled na Serikali, na ndio maana tunashiriki katika uagizaji wake ili tuje tuhakikishe kwamba bei itakayouzwa hii sulphur itakuwa inahimilika kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kwa wananchi waliouza korosho zao msimu uliopita na sasa hivi hawajalipwa. Moja ya sababu ya wananchi hawa kutolipwa ni mkanganyiko uliotokea baada ya kuwashawishi wafungue akaunti ili malipo yafanyike moja kwa moja benki. Wengine badala ya kufungua wao akaunti waliwabebesha ndugu na marafiki zao na hivyo wale walioingiziwa pesa kwenye akaunti zao kugoma kuwalipa wakulima hawa. Lakini lilitokea tatizo la Benki ya Covenant kufungwa ambayo vyama 14 vya msingi vilikuwa vinapitishia pesa katika benki ile. Sasa jambo hili ni la kisheria kwa hivyo suala la Benki Kuu na ile benki linaendelea kufanyiwa kazi na litakapokuwa limetatuliwa wakulima hawa watapewa fedha zao na wala hazitapotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwa haraka suala la masoko na namna ya kuuza kahawa na pamba kwa msimu wa mwaka huu. Serikali imeamua kusimamia ushirika wa nchi hii ili wakulima waweze kunufaika. Utaratibu uliokuwepo wa kuuza kahawa umekuwa hauna manufaa kwa wakulima walio wengi, lakini umewanufaisha zaidi watu wa katikati yaani watu wanaonunua na kuuza na si wakulima wenyewe. Neno linaitwa butura kwa watu wa Ziwa Magharibi wanafahamu maana yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwananchi analima kahawa, anapatwa na tatizo kidogo la shilingi 200,000; mtu mwenye pesa anakuja anampa shilingi 200,000 halafu anamuandikisha mkataba wa shilingi milioni tano na kusema hizo milioni tano wasipozilipa mpaka mwezi wa sita nyumba yake inauzwa; na kwa vile mwananchi huyu anakuwa na shida analazimika kuchukua hizo pesa kwa masharti ya kihalifu namna ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali imeona namna bora ya kuwasimamia wananchi hawa maskini kuwa ni kusababisha wauze kahawa yao kupitia mfumo rasmi mfumo wa ushirika. Kwa namna hii na nimesikiliza sana maoni ya Waheshimiwa Wabunge kwamba tutengeneze utaratibu ambao watau wenye shida kama hao katikati ya ushirika huo waweze kupata msaada. Ni kweli, Mbinga utaratibu huu unafanyika vizuri, vyama vya wakulima vya Mbinga vinao utaratibu ambao mwananchi akiwa na shida wanao mfumo wa kumsaidia na kwa hivyo tunapeleka huo uzoefu wa Mbinga katika maeneo mengine ili wananchi wa kule wasilazimike kuingia kwenye utaratibu ule usiokuwa na manufaa kwao isipokuwa wapitie ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, liko jambo la wauzaji wa kahawa moja kwa moja nchi za nje yaani direct export. Wauzaji wa namna hii sio wengi, kimsingi ni wale wenye mashamba makubwa ambayo ni kama asilimia 10 au tisa ya uzalishaji mzima hapa nchini. Sasa watu wa namna hii wamekuwa wanauza moja kwa moja na katika kuuza moja kwa moja hatupati takwimu sahihi za mauzo yao. Hawa pia ndio wamekuwa wanafanya hiyo kitu inaitwa butura, wananunua kwa wakulima, wana-aggregate halafu wanauza nje moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema kahawa hata kama imethibitishwa (satisfied) kwa ubora fulani ipeleke mnadani ili wanunuzi wengine pia wakaijue. Tunapofanya hivi tunazuia price transfer kwa sababu uuzaji wa moja kwa moja ambao hauwezi kudhibitiwa na bodi unakuwa unatoa mwanya mtu kutengeneza bei ya chini kwa sister company ili alipe kodi isiyostahili halafu fedha inayobaki anakwenda kukutana nayo huko nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, liko jambo la utayari wa ushirika kusimamia mfumo huu, tunalifanyia kazi, vyama vya ushirika vyenye matatizo tumesha vibaini na tunazungumza na mabenki kuona namna ambavyo navyo vinaweza vikapata fedha kwa ajili ya kulipa advance ambayo wamekuwa wanawalipa wakulima wao miaka yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kule KCU juzi ilisemekana KCU wametangaza bei ya shilingi 1,000 kwa kilo moja ya kahawa. Naomba nitoe taarifa rasmi kwamba jambo hilo sio kweli, wao walikuwa wanafanya bajeti ya chama chao cha msingi kwamba wachukue kiasi gani benki kwa ajili ya kuwa-advance wakulima kabla ya kupeleka kahawa ile mnadani na kamwe ile si bei ya kahawa ambayo wanatakuwa wananunua kutoka kwa wakulima wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamba pia tutauza kwa utaratibu huu huu, na tutapita na tunaendelea kupita maeneo yote ya pamba kujiridhisha kwamba vyama vya msingi vya wakulima wa pamba vipo in place na kama havipo basi uchaguzi ufanyike. Angalizo letu ni kwmaba wananchi wachague viongozi waadilifu wasije wakatumia kuchaguliwa kwao kwenda kuwaibia wananchi kama walivyozoea miaka ya nyuma. Nitahadharishe wale wanaogombea uongozi wa vyama hivi vya wakulima kwa lengo la kwenda kuuza wako mwili wao nusu uko jela, nusu uko bado mtaani kwa sababu hatutakuwa na huruma na mtu yeyote atakayejaribu kuiba mali ya wananchi kwa kisingizio chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la mfumo wa uingizaji wa pembejeo nchini. Katika hili tutafanya seminar ya Bunge zima kuelezea mfumo huu unafanyaje kazi.

Naomba Waheshimiwa Wabunge muwe na subira tutawapitisha katika mfumo huu ili uelewa uwe wa pamoja na tuko tayari kusikiliza maoni yenu pale mnapoona kwamba jambo hili haliendi salama.