Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuweza kutufikisha siku hii ya leo ambapo tunapata nafasi ya kuhitimisha hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya bajeti ya Ofisi yake lakini vilevile na Mfuko wa Bunge kwa bajeti ya mwaka 2018/2019 na baada ya kupitia pia utendaji kazi wa Serikali katika ofisi hii kwa mwaka wa fedha uliopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nasema hivyo kwa sababu Watanzania wamempambanua Mheshimiwa Rais wetu kama kiongozi mahiri, imara, shupavu na ni mzalendo wa kweli kabisa ambaye amedhamiria kusimamia maendeleo ya nchi yetu na kufanya mageuzi ya kisasa katika kuleta maendeleo ya Taifa la Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja naye nimpongeze sana Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na vilevile nimpongeze sana Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ally Mohamed Shein. Hawa wote wanafanya kazi nzuri sana katika kujenga Taifa letu, kudumisha Muungano na kuhakikisha kwamba misingi iliyojengwa na Waasisi wa Taifa hili inaendelea kufuatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya pekee nimshukuru sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miongozo na maelekezo ambayo amekuwa akinipatia mimi pamoja na watendaji wote wa Ofisi yake ili kuhakikisha kwamba tunachapa kazi na tunatekeleza maagizo ambayo tumekuwa tukiyapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu ni mchapa kazi na kiongozi mahiri na hiyo ameweza kujipambanua kabisa katika shughuli zake za Serikali ndani na nje ya Bunge. Tumwombee kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kumjalia afya njema ya kutekeleza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwapongeza hao niliowasema lakini kwa dhati nimpongeze sana Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde na Mheshimiwa Stella Alex Ikupa, Naibu Mawaziri katika Ofisi yangu. Hawa wamekuwa ni wasaidizi wangu wa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niwashukuru sana Bi. Maimuna Tarishi, Bw. Erick Shitindi, Profesa Faustine Kamuzora pamoja na Wakuu wa Taasisi zote, Wakurugenzi na wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa jinsi ambavyo tumepeana ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sina fadhila kama sitamshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Naibu Spika, Katibu wa Bunge, wafanyakazi wote wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi nzuri ambazo wamekuwa wakizifanya katika Bunge hili na hasa kutusaidia sisi Ofisi ya Waziri Mkuu kama waratibu wa shughuli za Bunge kuweza kutekeleza majukumu ya Serikali ipasavyo ndani ya Bunge lako. Shukrani zangu za dhati pia ziwaendee Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge ndani ya Bunge letu na Wabunge wote kwa ujumla kwa kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee niwashukuru sana Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ndugu yangu Mheshimiwa Jitu Soni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa na dada yangu Mheshimiwa Najma Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI ndugu yangu Mheshimiwa Oscar na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Dkt. Tisekwa na wajumbe wote kwa jinsi ambavyo wametusaidia sana kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee niwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Peramiho kwa kuendelea kuniamini, kuniunga mkono na kunipa ushirikiano mkubwa kutekeleza majukumu katika Jimbo letu na tunaona na kushuhudia maendeleo makubwa ya Jimbo la Peramiho. Naendelea kuwaeleza kwamba tupo pamoja na hasa kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu Hakuna Kulala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze katika hoja ambazo zimebakia, lakini kwa muda muafaka Mheshimiwa Waziri Mkuu atakuja kujibu hoja nyingine ili kuhitimisha hotuba yake. Hoja nitakazoanza kuzijibu ni hoja zinazomhusu Msajili wa Vyama vya Siasa na Ofisi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza ilikuwa ni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ifanye jitihada za kutosha kusuluhisha mgogoro katika Chama cha Wananchi (CUF) ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza katika Muungano na katika mgogoro huo. Naomba nichukue nafasi hii kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba mgogoro huu wa Chama cha CUF kwa sasa upo Mahakamani, kwa hiyo sitachukua nafasi hii kuujibu mgogoro huo ama kumuagiza Msajili wa Vyama kushughulika na mgogoro huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa ninachotaka kusema hapa ni hiki kifuatacho. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya siku zote wakati akiratibu na akitekeleza majukumu yake kama Msajili wa Vyama vya Siasa. Amekuwa akifanya kazi nzuri sana na sisi wote ni mashahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Msajili wa Vyama vya Siasa anafanya kazi hii kwa kuzingatia Sheria Na. 5 ya Vyama Vya Siasa ambayo ndiyo inayosimamia vyama vya siasa katika nchi yetu ya Tanzania. Sisi wote tumekuwa ni mashahidi, Msajili wa Vyama vya Siasa mpaka sasa amefanikiwa kusajili vyama vya siasa 19 ndani ya nchi yetu ya Tanzania ambavyo vimepata usajili wa kudumu lakini Msajili wa Vyama vya Siasa
ameendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni mbalimbali za vyama vya siasa katika nchi yetu ya Tanzania kwa weledi mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba tu niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na kutakiwa kusuluhisha migogoro hiyo ambayo nimeisema katika Chama cha Wananchi CUF, naomba niwashauri wenzetu wanaohusika na mgogoro ndani ya chama cha siasa cha CUF, ili mgogoro huu Mheshimiwa Msajili wa Vyama vya Siasa aweze kuushughulikia vizuri, uko utaratibu wa kisheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali anajua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunamtaka Msajili wa Vyama awe mediator katika mgogoro huo basi niwashawishi na kuwaomba waondoe mgogoro huu katika Mahakama ulikopelekwa mgogoro huo na Msajili wa Vyama anaweza akafanya kazi yake. Vinginevyo Msajili wa Vyama hawezi kuingia katika mgogoro huu kwa sababu mgogoro huo tayari umeshasajiliwa na upo katika Mahakama zetu na hivyo tumwache Msajili wa Vyama aendelee na shughuli nyingine ambazo hafungwi nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee na hoja nyingine. Waheshimiwa Wabunge na hasa Wabunge wa Upinzani wamelalamika sana na kusema kwamba suala la maandamano ni suala la Kikatiba na wamesema kwa sababu suala la maandamano ni haki ya Kikatiba wanafikiri upo msingi wa vyama vya siasa kuachiwa waendelee na maandamano bila kuzingatia sheria, hapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba suala la maandamano katika nchi yetu ya Tanzania linaratibiwa na sheria za usalama ndani ya nchi yetu chini ya vyombo vya usalama na hasa polisi na Katiba haiwezi kuchukuliwa kwamba ndicho kigezo cha kuviruhusu vyama kufanya maandamano bila kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa. Naomba sana kwa heshima yote niwaombe Watanzania wote, niviombe vyama vyote vya siasa katika nchi yetu ya Tanzania wahakikishe wanazingatia sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba yetu imeruhusu maandamano lakini maandamano yameratibiwa kisheria na kama yameratibiwa kisheria ni lazima tuhakikishe kwamba tunazingatia sheria katika kuratibu maandamano kwenye nchi yetu. Labda niulize kitu kimoja, tukiamka hapa siku moja asubuhi na kila mtu ameamua kuandamana; wakulima au wafanyakazi au kila mtu aamue tu kuandamana kwa sababu Katiba imesema, nadhani itakuwa siyo sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuviomba vyama vyote katika nchi yetu kuheshimu Katiba na sheria katika kutekeleza wajibu wao na siyo kuvunja sheria za nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo ilikuwa imetolewa na Waheshimiwa Wabunge ni kwamba chaguzi ndogo ambazo zimekuwa zikiendelea kwa sasa, zimekuwa zikigharimu sana fedha za Serikali. Baadhi ya Wabunge wakajaribu kulinganisha pia gharama ambazo zimekuwa zikitumika katika chaguzi hizi ndogo na utekelezaji wa majukumu ya Serikali na miradi mingine ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme demokrasia ni gharama. Hakuna demokrasia yoyote mahali popote ambayo haina gharama yoyote. Nasema hivi kwa sababu kama Jimbo la Uchaguzi kwa mujibu wa sheria na Katiba yetu liko wazi, hakuna jinsi, ni lazima tufanye uchaguzi. Kama ni Jimbo la Uchaguzi la Ubunge ama la Udiwani ni lazima kwa mujibu wa sheria na Katiba apatikane mwakilishi wa kuwawakilisha wale wananchi kwenye jimbo husika. Hatuwezi kufanya uchaguzi bila kutumia gharama, kwa hiyo, hiyo ni demokrasia ndiyo maana nasema ni gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, niseme neno moja, nina mfano tu mdogo. Jimbo la Songea Mjini baada ya kuwa wazi na uchaguzi kufanyika, Mbunge ambaye sasa hivi anawakilisha Jimbo la Songea Mjini, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, ameniambia kwa muda huu mfupi kwa sababu nafasi iliyokuwa wazi imejazwa ameweza kufanikiwa kupata fedha za Kitanzania zisizopungua bilioni sita kwa ajili ya ujenzi wa barabara na miundombinu ya stendi katika jimbo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, gharama tulizozitumia kwenye uchaguzi ni bilioni nne, lakini zimewawezesha wananchi wa Jimbo la Songea kupata bilioni sita kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Kwa hiyo, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba ni ukweli usiopingika kwamba demokrasia ni gharama na kama demokrasia ni gharamani ni lazima tuendelee kufanya uchaguzi kujaza nafasi wazi kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo hoja nyingine iliyozungumzwa, imesema kwamba kuna kila dalili ya Msajili wa Vyama kukusudia kuua Upinzani katika nchi yetu ya Tanzania. Naomba niseme yafuatayo:-

Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Ali Hassan Mwinyi, mwaka 1991 alimteua Jaji Nyalali kukusanya maoni ya Watanzania kuamua kama nchi yetu iende katika mfumo wa vyama vingi au ibaki katika mfumo wa chama kimoja. Watanzania asilimia 80 walisema hawataki mfumo wa vyama vingi, Watanzania asilimia 20 walisema wanataka mfumo wa vyama vingi, lakini ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi iliyofanya maamuzi magumu tuingie katika mfumo wa vyama vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu za kuingia katika mfumo wa vyama vingi zilikuwa wazi tu, ni kuwafanya Watanzania waone kwanza Chama cha Mapinduzi hakiogopi mageuzi na hakiogopi mfumo wa vyama vingi. Vilevile ilikuwa ni kuhakikisha kwamba demokrasia ya wachache waliochagua mfumo wa vyama vingi inaheshimiwa na wengi waliokataa mfumo wa vyama vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya niliyoyasema inajidhihirisha kabisa kwamba Serikali ya chama chetu ilifanya maamuzi ya kuingia katika Mfumo wa Vyama Vingi ili kufuata demokrasia, kwa hiyo hakuna sheria yoyote inayomruhusu Msajili wa Vyama kuvunja demokrasia na kufuta Mfumo wa Vyama Vingi katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Msajili wa Vyama aendelee kuchukua hatua stahiki kama Kamati ya Bunge ilivyotushauri kwa vyama vyote ambavyo havitaki kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria na taratibu tulizoweka ili kusaidia Mfumo wa Vyama Vingi katika nchi yetu uweze kuwa ni mfumo halisia ambao unaendana na matakwa ya kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nizungumze machache kuhusu Tume ya Uchaguzi. Kwenye Tume ya Uchaguzi imetokea hoja kwamba Tume hiyo imekuwa haina weledi, haizingatii sheria na taratibu katika kuendesha shughuli za uchaguzi na wakati mwingine imekuwa pia ikisimamia uchaguzi huo bila kuzingatia sheria na taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Tanzania. Tume ya Uchaguzi imeanza kufanya kazi ya kusimamia uchaguzi mwaka 1995 tulipoingia katika mfumo wa vyama vingi. Mwaka 1995 tumemaliza uchaguzi salama na Serikali imeingia madarakani na tumeendelea kufanya kazi. Vilevile mwaka 2000, 2005, 2010, 2015, Tume hii ya Uchaguzi ndiyo imesimamia uchaguzi wetu na hata sisi Wabunge ambao tuko ndani ya Bunge lako Tukufu tumesimamiwa uchaguzi wetu na Tume hiyohiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kushangaa sisi tuliposhinda, Tume hii ya Uchaguzi ilikuwa imefanya vizuri, hatukusema lolote na hatukuwa na malalamiko yoyote lakini leo tunasimama na kusema Tume hii haina weledi na haifuati utaratibu wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kukuhakikishia sisi kama Serikali tumeendelea kuisimamia na kuiratibu Tume ya Uchaguzi kwa kuzingatia Katiba kwa sababu Katiba inasema wazi Tume ya Uchaguzi ni huru na inafanya kazi zake kwa uhuru ulio kamili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa Katiba pale ambapo uchaguzi umekwishafanyika na kama chama chochote kinaona kwamba misingi ya kisheria haijafuatwa, chama hicho kimeruhusiwa kwenda mahakamani na kule mahakamani ndipo kutakapopatikana haki ya kisheria kwa chama chochote kinacholalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu, kwa chaguzi hizi ndogo zote zilizopita kesi zilizofunguliwa kwenye kata hizo takribani kama arobaini na kitu mpaka 50, kesi za uchaguzi zimefunguliwa kwa kata mbili tu. Kwa hiyo, naomba tuone kama kweli Tume hii ilikuwa haisimamii uchaguzi huo kwa haki naamini kabisa kata nyingi kesi za uchaguzi zingekuwa zimefunguliwa. Kwa majimbo yote ambayo Tume ya Uchaguzi imeshaendesha uchaguzi hakuna jimbo hata moja ina kesi ya kupinga uchaguzi katika jimbo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niseme kwamba Tume hii ya Uchaguzi inafuata utaratibu katika uendeshaji wa shughuli zake na kama mtu yeyote, chama chochote kina malalamiko naomba sana kifuate sheria na kiende Mahakamani. Niviombe vyama vyetu vya siasa visikimbilie kulalamika kwenye vyombo vya habari, ni vyema vyama vya siasa vizingatie sheria za nchi tulizonazo katika kuendesha chaguzi zetu tunazoendelea nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine kwa Tume hii ya Uchaguzi ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunaboresha daftari la wapigakura kwa wakati. Naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba shughuli ya kuboresha daftari la wapigakura tumeshaianza ndani ya Serikali kwa mujibu wa sheria na taratibu tulizonazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaanza kuhuisha kanzidata ya daftari la wapigakura katika nchi yetu ya Tanzania, tumeshaanza kutoa elimu na tumeshaanza kufanya shughuli zote ambazo zinatakiwa ili daftari la wapigakura katika nchi yetu liwe limeboreshwa na liendane na wakati kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliambiwa pia tuhakikishe kadiri iwezekanavyo watendaji wote wa Tume ya Uchaguzi ambao watakiuka maadili ya kisheria kama watendaji ndani ya Tume basi wachukuliwe hatua na ikiwezekana wapewe adhabu zinazostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kazi hiyo inafanyika vizuri wa sababu tunazo sheria, tunayo miongozo na tunazo taratibu ambazo zimewekwa bayana. Kwa hiyo, watendaji wote ambao wataonekana wanakiuka taratibu za kisheria katika kufanya kazi ndani ya Tume yetu ya Uchaguzi basi watachukuliwa hatua stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambazo zilikuwa zimejitokeza zilikuwa zinahusu mapambano dhidi ya UKIMWI katika nchi yetu ya Tanzania. Katika eneo hili mambo yafuatayo yaliongelewa kwa kiasi cha kutosha.

La kwanza, ilikuwa ni bajeti kuendelea kutolewa kwa wakati; la pili ilikuwa ni tozo ndani ya Serikali ili kutunisha Mfuko wa ATF (AIDS Trust Fund); la tatu ilikuwa ni kuhakikisha kwamba asilimia 10 ambayo iko kwenye own source ambayo inatumika kwa akinamama na vijana inatumika pia kwa ajili ya kuwahudumia wanaoishi na VVU lakini ya nne ilikuwa kuhakikisha kwamba upatikanaji wa dawa kwa ajili ya wenzetu wanaoishi na VVU unaendelea kuwa wa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako kwamba tumefanya kazi ya kutosha na Wizara zinazohusika. Bajeti ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania kwa mwaka huu wa fedha imeongezeka. Suala la tozo kwa ajili ya Mfuko wa Kudhibiti UKIMWI katika nchi yetu, tumeshapeleka mapendekezo yetu kwenye Ofisi ya Waziri wa Fedha na tunaamini kabisa wenzetu watatushauri njia gani ya kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwamba mfuko wenyewe kupitia bodi umeshaanza kufanya kazi ya kutosha ya kukusanya fedha ili kuhakikisha kwamba unakuwa na fedha na hiyo ni kujihami na upungufu wa fedha za wafadhili.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la asilimia 10, naomba mtuachie, tunachukua pendekezo hilo, tutalifanyia kazi kwa pamoja na wenzetu wa TAMISEMI. Tutakuja kutoa majibu tuone kama hiyo asilimia kumi tunaweza tukagawana hiyohiyo ama tunaweza kutumia Mifuko kama TASAF ama mifuko mingine kuhakikisha hawa wenzetu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI na wao wanaweza kusaidiwa ili kuweza kukidhi mahitaji yao na kuwafanya waweze kutumia dawa vizuri, lakini kuwasaidia waweze kuendelea kuishi wakiwa na afya njema. Naomba niseme hilo nalichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine lilikuwa ni suala la kuwezesha wananchi kiuchumi. Tuliambiwa kwamba kwenye miradi inayoendelea kwa sasa tujitahidi kuhakikisha kwamba Watanzania wazawa na wao wanapata nafasi za kazi ama wanakuwa ni wakandarasi washiriki katika miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie, kupitia mpango wetu wa local content ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tumeweza kuanzisha mpango mkakati mahsusi wa kuzungumza ndani ya Serikali kuhusu suala la local content kuhakikisha kabisa kwamba Watanzania katika miradi mikubwa ya kitaifa, lakini vilevile katika shughuli zinazoendelea katika halmashauri zetu na wao wanapata nafasi ya kushiriki kama washiriki wa uchumi katika nchi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka pia tulifanya hata marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ambayo inatupelekea kuwafanya Watanzania waweze na wao kuwa ni washiriki kwenye suala zima la maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya sekta ya hifadhi ya jamii, Waheshimiwa Wabunge wametushauri kwamba tutoe elimu kwa Watanzania kuhusu sekta hii. Naomba kukuhakikishia kwamba kazi hiyo inafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, walitaka tuhakikishe sheria mpya inaanza kutumika kwa haraka kwa kuwa na kanuni zake, naomba niwahakikishie kanuni ziko tayari na zinakamilishwa kwa hatua ya mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Wabunge walituagiza tupanue wigo wa hifadhi ya jamii ifike mpaka kwenye sekta isiyo rasmi. Naomba niwahakikishie kwa mabadiliko ya sheria tuliyoyafanya Bunge lililopita sasa sekta isiyo rasmi inatambulika rasmi katika suala zima la hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la BAKWATA, kwa nini wamefanya mkutano wao hapa Bungeni. Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, Serikali yetu haina dini, Serikali yetu inafanya kazi na taasisi zote za dini bila kujali ni aina gani ya taasisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, wala isiwe tabu kwa BAKWATA kufanya mkutano wao hapa, kama kuna taasisi nyingine inataka kufanya mkutano hapa Bungeni na wao walete maombi ili mradi tu wafuate taratibu na sheria. Vilevile mkutano wanaotaka kuja kuufanya hapa uwe ni mkutano ambao tutakuwa tumejiridhisha kwamba mkutano huo hauna madhara ndani ya Bunge na nje ya Bunge letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hakuna haja ya kuhangaika ni kwa sababu gani BAKWATA wamefanya mkutano hapa, ninachosisitiza ni suala la misingi ya kisheria na aina ya mkutano unaotakiwa kufanyika hapa, kama ni vitu ambavyo vinaelezeka na havina madhara kila mtu anaweza akafanya mkutano mahali popote ambapo pana ukumbi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala ambalo pia nataka nilizungumze kwa ufupi ni suala la dawa za kulevya. Nianze kwa kuipongeza Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya katika nchi yetu ya Tanzania kwa kazi nzuri. Imefanya kazi nzuri sana katika maeneo matatu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la supply (kudhibiti upatikanaji wa dawa); kwenye suala la demand (kudhibiti uhitaji) na katika kupunguza madhara (kwenye masuala ya harm reduction). Kwa hiyo, Tume imefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tukubaliane hapa kwamba suala la uhalifu katika nchi yetu ya Tanzania si la Muungano na wala suala la Mahakama si suala la Muungano, lakini suala la ulinzi wa Taifa ndilo suala la Muungano katika nchi yetu. Kwa hiyo, mamlaka hii kwa sheria tuliyonayo inafanya kazi upande wetu huku Bara lakini kwa sababu uhalifu hauna mipaka ndiyo maana tunasema ni lazima mamlaka hii ifanye kazi ya kutosha na mamlaka katika upande wa pili wa Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ni hali ya kawaida tu, kama upande mmoja ukifanya kazi, upande mwingine usipofanya kazi ni shida ama pande zote mbili tusipofanya kazi kwa pamoja itakuwa shida. Naomba niwahakikishie sisi wenyewe ndani ya Serikali jambo hili tunalifanyia kazi kwa pamoja pande zote mbili za Muungano kuhakikisha dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania zinakoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa nafasi uliyonipa, hoja bado ziko nyingi kiasi, tutazijibu kwa maandishi. Nichukue nafasi hii kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kuheshimu sheria na hasa katika kushughulika na shughuli ya vyama vya siasa katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kujibu hoja ambazo zimewekwa mbele yetu katika siku hii ya leo. Nakushukuru sana.