Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu. Kwanza kabisa napenda kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo amekuwa akitekeleza majukumu ambayo yamekuwa yakitatua shida mbalimbali zinazowagusa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili napenda niishukuru Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa namna ya kipekee ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na mimi Mbunge wa Jimbo la Kavuu kwa namna ambavyo wamekuwa wakijaribu kutatua matatizo ya wananchi wangu. Napenda kabisa niishukuru Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya TAMISEMI kwa kuweza kunipatia ambulance ambayo inaweza ikafanya shunting kati ya vituo viwili vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua jiografia ya Jimbo langu bado siyo nzuri, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI uniongezee ambulance itakayofanana na miundombinu ambayo nimepata. Hata hivyo, nashukuru sana kwa kile nilichokipata ambacho ni ambulance ambayo itanisaidia kutoka kituo cha afya cha Kibaoni kwenda kituo cha afya cha Mamba. (Makofi)
Mheshimiwa wenyekiti, napenda niendelee kushukuru kwa kuwa wameweza kuniwezesha kituo changu cha afya cha Kibaoni ambacho sasa kinaelekea kwisha lakini niwaombe katika Jimbo langu la Kavuu nina vituo vya afya vitatu; nina kituo cha afya cha Mamba na kingine cha Mwamapuli ambacho wananchi wameanza kujitolea namna ambavyo ya kuweza kutatua matatizo ya afya kutokana na jiografia ilivyokaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri atuongezee nguvu katika vituo hivi. Nimshukuru kwa namna ya pekee Dkt. Zainab ambaye aliweza kutupa mawazo akishirikiana na Katibu Mkuu Engineer Iyombe namna ambavyo tunaweza tukaanzisha hospitali ya Halmashauri ya Wilaya katika Jimbo la Kavuu na niwashukuru Wizara hii wametupatia kibali na sasa tunakwenda kujenga hospitali ya Wilaya. Ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee lingine limekuwa likiongelewa sana na limeongelewa na baadhi ya Wabunge hata jana kuhusu mchango wa chakula mashuleni. Ni kweli kwamba chakula mashuleni kinapunguza utoro, ni kweli kwamba chakula mashuleni kinasaidia wanafunzi kuwepo mashuleni na kinaongeza kiwango cha ufaulu. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwaomba wananchi wetu waendelee kuchangia kwa maana ya kwamba ni jambo lenye tija katika kizazi chetu kijacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tu; Mbunge wao wananchi wangu wa Jimbo la kavuu nimeweza kuchangia karibu hekari 30 kwa maana kwamba kila shule inapata hekari moja ya chakula na sasa tumeanza kuvuna. Kwa hiyo ni mchango wangu kwa chakula kwa maana naelewa umuhimu wa chakula mashuleni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali na niishukuru halmashauri yangu, Halmashauri ya Mpingwe imekuwa ni halmashauri ya pili kati ya halmashauri 185 ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika kutenga asilimia 10 kwa maana kwamba asilimia tano ya akinamama na asilimia tano ya vijana. Kwa hiyo, niwaombe, niko vizuri na Mkurugenzi wangu na nafanya naye kazi vizuri sana na anasimamia miradi vizuri mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, kama watafanya reshuffle mimi Mkurugenzi wangu waniachie pale, yuko vizuri. Kama kuna Wakurugenzi wengine hawako vizuri mimi wa kwangu yuko vizuri, anasimamia miradi vizuri, milioni 400 walizonipa kituo cha Kibaoni pale cha afya zimesimamiwa vizuri, pesa za Jimbo zinasimamiwa vizuri. Kwa hiyo, kazi inakwenda na maendeleo tunayaona na Jimbo la Kavuu sasa linaonesha mabadiliko chini ya Dkt. Pudenciana Kikwembe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru Serikali kwa namna ya pekee ilivyoondoa riba katika ule mkopo wa asilimia 10 kwa akinamama na vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi kwa TARURA. TARURA ni chombo ambacho kwa malengo yake ni mazuri sana, lakini naomba kiongezewe pesa, kiongezewe watalaam. Kutokana na mvua hizi zinazonyesha nilikwenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri na nikapeleka maombi yangu binafsi, maombi rasmi, maombi special kwa namna ambavyo sasa Jimboni kwangu hakuna hata njia moja inayopitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwomba pesa ya kutengeneza box culvert ya Mwamapuli-Majimoto ambayo inagharimu karibu milioni 160, nimeomba Majimoto daraja jipya la Msadya ambalo kwa wale wanaongalia vyombo vya habari waliniona nikienda kulitembelea. Sasa hivi kwa hela waliyotupatia nashukuru limeanza kupitika angalau wagonjwa wanaweza kwenda kutibiwa kituo cha afya kingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pesa takribani bilioni 1.7 kwa ajili ya kujenga daraja lingine, kwa sababu daraja lile linahudumia karibu Kata tano kwa ajili ya akinamama na watoto wanaokwenda hospitali. Kwa hiyo, ni maombi rasmi, naomba niyalete kwako hapa na kwa sababu nilishayaleta kwa maandishi naomba mnisaidie kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba drift mbili kati ya Ntibili na Kikonko ambako kumepata mafuriko na hivi ninavyoongea mvua bado zinaendelea, zimenyesha karibu siku nne mfululizo. Naomba pia box culvert kati ya Kata ya Mamba na Makuyugu ambayo inaweza kugharimu pia milioni 160.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia culvert ya Kibaoni-Chamalendi ambako pia barabara imekatika ambayo ni barabara moja hiyo hiyo inayoungnisha kwenda kwenye kituo cha afya cha Kibaoni. Naomba pia culvert lingine la Mabambasi kupitia Mwamapuli ambalo pia linaunganisha barabara hiyo hiyo kwenda kwenye Kata ya Kibaoni ambayo inakwenda kwenye kituo cha afya ambacho watu wanatumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la watumishi, watumishi wamekuwa wengi wakistaafu hawapati haki zao, kwa mfano, tuna wastaafu wa Magereza na Mahakama wapatao karibu 200 waliostaafu tarehe 1 Julai, mpaka leo hawjaalipwa haki zao kwa hiyo tulikuwa tunaomba walipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwa watumishi Walimu; Walimu wamekuwa kama ni wanyanyaswaji kwa sababu hawapandishwi vyeo vyao, hawalipwi pesa zao wanapokwenda likizo, hawalipwi pesa zao wanapohamishwa. Kwa hiyo, naomba malipo yao kwa kweli kwa mwaka huu yatiliwe mkazo. Walimu wetu ni wachache katika vituo vyetu, sasa tunapozidi kuwadidimiza, tunawapunguzia morally ya kazi kwa kweli naomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee lingine; Mwalimu anapotaka kuhama tunasema atafute nafasi eneo mbadala ili aweze kuhamishwa. Sasa unakuta kuna mwingine kaolewa ama mwingine kaoa kule mnakompeleka hana mume, hana mke, mnachotarajia nini? Kwa hiyo, niwaombe kama mume anataka kumfuata mkewe au mke anataka kumfuata mume wake basi waruhusiwe kwa sababu tunajua maambukizi mapya ya UKIMWI sasa hivi ni mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapowaachanisha vile inakuwa ni rahisi kuwaweka kwenye mitego ambayo wanaweza wakapata maambukizi. Kwa hiyo, tunaomba muwalipe malipo yao ya uhamisho na mambo yao mengine ambayo wamekuwa wakidai hasa wanapokuwa pia wanakwenda kwenye matibabu ambayo yako nje ya utaratibu wa bima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana suala la Walimu, kwa kweli ni tatizo. Mimi ni Mwalimu pamoja na kwamba ni Mbunge, lakini ninapokwenda Jimboni kwangu mimi naingia darasani kufundisha. Nafundisha kwa sababu ya uhaba wa Walimu. Kwa hiyo niwaombe sana, katika kasma ijayo ya waajiriwa mtupatie watumishi wa sekta ya afya pamoja na sekta ya ualimu, ni vitu ambavyo tunavihitaji sana hasa katika kuhudumia wagonjwa wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nahitaji zaidi Madaktari badala ya Makatibu wa Vituo vya Afya. Makatibu wanakaa ofisini na computer, nikipata nurse pale clinic atanisaidia zaidi kuliko Katibu wa Afya. Kwa hiyo, naomba hata tunapofanya allocation ya watumishi, tuangalie; Kituo changu cha Kibaoni kina Makatibu wa Afya watatu wa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naunga mkono hoja kwa asilimia zote.