Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na uzima kwa siku ya leo. Pia nampongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji wake wa kazi. Naomba ndoto yake ifike mahali ifikie mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nawashukuru na kuwapongeza Mawaziri wote; ndugu yangu Mheshimiwa Jafo; Naibu Mawaziri, ndugu yangu Mheshimiwa Kandege, Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Mkuchika. Nawapongeza kwa sababu kubwa, kwanza kwa hekima zao, busara, uwajibikaji, unyenyekevu, uzalendo na usikivu. Tunachoweza kuomba kwa Mwenyezi Mungu, aendelee kuwapa afya njema ili waendelee kulitumikia Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na utawala bora. Utawala bora ni pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi. Ili wananchi waweze kupata huduma bora, ni lazima wawe karibu na huduma. Nazungumza jambo hili kutokana na mazingira ya Jimbo langu. Jimbo langu lina jiografia mbaya na ni kubwa na limekaa vibaya na linawatesa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimchukua mwananchi aliyepo kule Ilambo ili afike Makao Makuu apate huduma, anatumia karibu nauli ya Sh.50,000/=; kwenda na kurudi Sh.100,000/=, nauli ya kutoka Sumbawanga mpaka hapa Dodoma. Sasa akiwa na mgonjwa, kukodi gari, lazima awe na shilingi milioni moja; au akiwa na kesi, anahitaji mashahidi watano, lazima awe na Sh.500,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linawatesa wananchi na sijajua ni kwa nini? Kwa sababau tumepeleka maombi mara kadhaa. Bahati nzuri wapo mashuhuda mbalimbali ambao wameshuhudia jambo hili na ukubwa wake, ambao nataka niwataje leo hii. Shuhuda wa kwanza ni yeye mwenyewe Mheshimiwa Mkuchika, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, anayafahamu mazingira vizuri mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shuhuda wa pili ni Mheshimiwa Ole Njoolay, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Shuhuda wa tatu ni ndugu yangu Mheshimiwa Stella Manyanya, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na jitihada alizianza yeye mwenyewe japokuwa hazijafanikiwa. Shuhuda wa nne alikuwa Zolote Stephen Zolote. Shuhuda wa tano ni Waziri Mkuu, ndugu yangu Mheshimiwa Majaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana, juzi alifika mpaka Mto Wisa mahali ambapo kuna changamoto kubwa sana. Shuhuda wa sita ni Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahman Kinana; yeye tena alitamka kabisa kwamba Jimbo hili lazima ligawanyike, Wilaya lazima ipatikane na Halmashauri lazima zipatikane. Huyo ni shuhuda wa sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shuhuda wa saba ni Waziri wa Uchukuzi, ndugu yangu Mbalawa, juzi amepita kule ameliona Jimbo jinsi lilivyo. Shuhuda wa nane ni Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu, alifika kule wakati wa kampeni, akashangaa kwamba hivi kweli eneo kama hili linakuwa na changamoto namna hii, linatengwa kiasi hiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, shuhuda wa tisa ni Waziri wa Mambo ya Ndani, ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, wakati wa kampeni alikuja kule akashangaa eneo jinsi lilivyo. Shuhuda wa kumi ni Waziri wa TAMISEMI ndugu yangu Mheshimiwa Jafo. Alikuja akakaa na Mkuu wa Mkoa mpaka akaanza kumpa jiografia, bahati mbaya hakuzunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shuhuda wa 11 ni Naibu Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Kandege, anajua hali halisi jinsi ilivyo. Shuhuda wa 12 ni Wabunge wote wa Mkoa wa Rukwa na Wabunge majirani wa Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Mbeya na baadhi ya Madiwani ambao wamefika katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shuhuda mwingine wa 13 ni Naibu Katibu Mkuu wa Elimu, ndugu yangu Zunda, alikuwa Afisa Tawala juzi juzi kwetu. Shuhuda wa 14 ni ndugu yangu Katibu Mkuu Iyombe, alikuwa Meneja wa TANROAD Mkoa wa Rukwa. Anayafahamu mazingira vizuri mno. Shuhuda wa 15 ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Warioba, alishawahi kufika maeneo yale. Alishangaa sana maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shuhuda wa 16 ni Waziri Mstaafu, ndugu yangu Pinda na alitamka hata hapa Bungeni kwamba kwa kweli Jimbo lile ni kubwa na jiografia ni mbaya. Shuhuda wa 17 ni wengine wengi Watendaji wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jamani, hata kama Serikali imesimamisha matumizi, wakati mwingine Rais wetu hamumwelezi hali halisi. Mheshimiwa Rais huyu ana huruma kubwa mno. Tunaona maeneo mengi anavyofika anatetea wanyonge. Angepata hali halisi, nami naomba Mwenyezi Mungu, huyu mtu siku moja afike kwenye Jimbo langu, atatamka pale pale kwa jinsi ninavyomfahamu Mheshimiwa Rais huyu kwa huruma yake, atatamka siku ile ile. Ila wana- by pass hawampii information hali halisi ya mateso ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli jambo hili linaumiza wananchi na bahati nzuri walio wengi najua wengi wanalijua Jimbo langu. Inaumiza sana hasa wananchi wangu wanashindwa kupata huduma sahihi. Hii maana yake nini? Naomba Mheshimiwa Jafo jambo hili alitolee ufafanuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzungumza ni suala la afya. Kwanza naishukuru Serikali, juzi juzi wametuambia wametutengea Sh.1,500,000,000/= kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya, tunashukuru sana, lakini vilevile walitupa Sh.400,000,000/= kwa ajili ya kupanua Kituo cha Afya cha Milepa, tunashukuru na kinaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba upanuzi wa vituo vingine vya afya kama Kituo cha pale Nkuhi; Naibu Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Kandege alienda pale akakutana na Watendaji na wananchi wa pale Nkuhi na akasema atalishughulikia. Naomba sasa jambo hili ndugu yangu Mheshimiwa Kandege, wananchi wa Nkuhi wanasubiri awasaidie, kile kituo kiingie kwenye upanuzi na vilevile Kituo cha Ilemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vingine ambavyo vinaendelea katika kumalizika katika hatua mbalimbali ni Muze, Kahoze, Kipeta na Kalambazito. Vilevile tunazo zahanati ambazo zilishafika katika hatua mbalimbali. Zahanati 21 zinahitaji tu kupewa fedha ili ziweze kumalizika na zianze kutoa huduma kwa wananchi. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni utaratibu wa upatikanaji watumishi katika Vituo vya Afya wa kada ya ulinzi, dobi na wapishi. Bado na lenyewe hili ni changamoto, halijulikani vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie kuhusu suala la elimu. Kwanza tunashukuru Serikali yetu kwa elimu bure, lakini vilevile zipo changamoto ukiacha Walimu wa Sayansi; na juzi nimepita Lahela pale wananchi wamelalamikia shule yao ile ya Uchile, hawana Walimu wa masomo ya sayansi, lakini vile vile zipo shule kadhaa ambazo zimeanzishwa na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hilo nataka nilizungumze, hizi shule mpya ambazo zinaanzishwa na wananchi, wanazianzisha kwa mahitaji ya watoto wao ambao wakati mwingine shule nyingine ziko mbali au kuna changamoto ya daraja wanaogopa watoto wao wasije wakapata madhara? Wanaamua wao wenyewe kujichangisha nguvu kazi kujenga shule mpaka wanafikia kujenga madarasa manne, ofisi, madawati, lakini changamoto ni namna ya kujisajili. Sijajua hapa kuna jambo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa wamejitolea wenyewe na sheria inasema shule mpya ya wananchi waliojitolea wenyewe; japokuwa tunapasha kuliangalia upya. Wananchi hawa wengi watoto wao watakosa elimu kwa sababu ni wachache wanaoweza kujitoa. Lenyewe hili nilitaka mliangalie vizuri. Pia shule yangu ya pale Kirando ambayo wananchi walishajitolea wakajenga, iko vizuri; na Shule ya kule Nhungwe, shule ya kule Nkuhi na Shule ya Mahenje kule Milepa Kinamo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naiomba Serikali ijaribu kuangalia fedha za ujenzi wa madaraja, nyumba za Walimu na Vyuo ambavyo zinasimamiwa na elimu. Nashauri fedha hizi ziende TAMISEMI. Wale wabaki na shughuli ya kusimamia taaluma. Ziende TAMISEMI waweze kusimamia fedha hizi. Kwa hiyo, naishauri Serikali iweze kuliangalia jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la barabara. Kwanza naishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi, namshukuru Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli, alipokuwa Waziri ni mara kadhaa nilikuwa nikimwomba juu ya fedha za kujenga daraja la Mto Momba na alikuwa akiniahidi. Nashukuru kwamba baada ya kuwa Rais, katika jambo ambalo alikuwa na kumbukumbu nalo ni kutoa fedha za ujenzi wa daraja la Mto Momba, ametupa shilingi bilioni 17.8 na daraja limeshaanza kujengwa, tunatarajia mwezi wa Saba litamalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba baada ya kumalizika daraja hilo, Serikali ianze sasa hatua nyingine za upembuzi yakinifu ya kuunganisha barabara kwa ajili ya lami kwa maana ya kutoka Kibaoni kuja Kilyamatundu kuungana na wenzetu wa Songwe kwa maana ya kutokea Mloo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile bado ina changamoto kubwa, ina madaraja mengi na ni eneo ambalo lina uzalishaji wa hali ya juu; mpunga, mahindi, karanga, mtama na kadhalika. Ile barabara ikikamilika, ndilo eneo ambalo tumetarajia hata viwanda vyenyewe vinaweza vikapatikana katika eneo lile kwa sababu mpunga unalimwa kwa wingi. Tunakosa kutangaza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)