Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niseme machache katika Wizara hii muhimu sana kwa maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba Mwongozo ulioombwa asubuhi na Mheshimiwa Waitara kuhusu Sekretariet ya KUB kuondolewa Bungeni ni Mwongozo ambao hautakiwi kuendelea kupewa siku. Hili suala linatakiwa lijadiliwe kwa dharura ili haki itendeke katika Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa afya ya Bunge hili ni vizuri mkafanya maamuzi mapema ili hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani iwepo Bungeni na Watanzania watendewe haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nategemea kubomoka sana. Sasa kabla sijabomoka, naomba nishauri machache ambayo nikibomoka baadaye hamtonisikia. Naomba nishauri kuhusu suala la TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba mna barabara nchi hii za kilometa 108,000 vijijini na mijini, lakini TARURA hii mpaka leo kwenye shilingi bilioni 230 mmewapelekea shilingi bilioni 98, wamejenga kilometa 4,000 tu kati ya 34,000. Naomba majibu, ni kwa nini tunatengeneza vitu halafu pesa hampeleki? Kuna uhalali gani wa ninyi kuendelea tu kwamba bajeti nzuri wakati ukweli ni kwamba fedha hazipo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nishauri tu kwa nia njema. Mfuko wa Bima ya Afya sasa hivi mtu mmoja hawezi akapata ile Bima kubwa akatibiwa kwenye Hospitali ya Rufaa kama Muhimbili na maeneo mengine, ni lazima awepo kwenye group. Naomba nishauri, ile Bima ya shilingi 76,000 muifanye kwa mtu mmoja mmoja angalau wananchi watibiwe, siyo lazima wawe kwenye group ili isaidie Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, nishauri kuhusu suala la elimu bure. Mmeanza elimu bure, elimu bila malipo, sijui kitu gani na kitu gani. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku- wind-up atuambie fedha za walinzi, maji, umeme wameziweka wapi? Kwa sababu kwa sababu walinzi wameacha shule zetu na madawati yanaibiwa na hata fedha za elimu bure bado hawajaziongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nashauri kuhusu mikopo ya vijana na akinamama. Wamefanya jambo jema kuondoa riba ya asilimia 10, ni jambo jema wala hatukatai. Hata hivyo, ni nani aliyewalalamikia kwamba tatizo ni riba? Tatizo ni Halmashauri kutokutenga fedha. Katika bajeti hii iliyopita, kati ya shilingi bilioni 61 ni shilingi bilioni 15 tu zimepelekwa, 9% ndiyo zimetengwa kwa vijana na akinamama. Tatizo siyo riba, tatizo ni fedha hazipelekwi na Halmashauri hawana vyanzo. Badala ya ku-tackle tatizo, mnakuja na maneno mazuri mazuri ya kufurahisha Watanzania, ham-solve tatizo! Atuambie kwa nini fedha hazipelekwi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, wazee wamewasahu. Wamewapatia walemavu, it is okay, nami nawapongeza; lakini akinamama na vijana wamebakiwa na asilimia nne nne. Ushauri wangu ni kwamba wachukue 2% wawapatie wazee ili na wao katika nchi hii waone kwamba wamewakumbuka, maana kipindi cha Awamu iliyopita ya Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete waliambiwa watapewa hata token amount kwa mwezi. Mpaka leo hawapewi, lakini hata kwenye hizi fedha hawakumbukwi. Sasa wawatengee na wao 2%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nibomoke. Utawala Bora katika nchi hii tunapoongea msituone maadui. Hii Tanzania ni ya kwetu sote. Tunatamani kila Mtanzania mmoja wetu aheshimike kwa nafsi yake, atendewe haki kwa nafasi yake; kila mmoja awajibike kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi hii ambazo tumejiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mbunge mmoja wa Mkoa wa Manyara anasema kifua kinamuuma. Wakati anachangia asubuhi, anasema mimi kifua changu kimejaa, kinauma, naomba tu mengine niya-save kwenye kifua. Naomba nisiumie kifua, leo nibomoke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Wakuu wa Mikoa ambao mmekuwa mkiwateua bila kuangalia ame-serve kwenye public service kwa muda gani mnawatoa kwenye Vyama vya Siasa, mnawaleta mnawapa nafasi za kuongoza Halmashauri na Wilaya zetu, wamekuwa wakifanya mambo ya ajabu haijawahi kutokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kwa Tunduma, siyo kwa Mkoa wetu wa Manyara, siyo kwa Hanang ambako hata mzee wetu, Mama Nagu anawekwa ndani, lakini ni Wakuu ambao wamekuja kufanya kazi ya siasa, siyo kazi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lilitokea tatizo kubwa sana katika Mkoa wetu wa Manyara. Stendi ya mabasi ambayo Mheshimiwa Waziri anasema kwamba tukusanye ushuru, ilikabidhiwa CCM mwaka huu. Stendi ya mabasi ambayo Halmashauri tunakusanya ushuru wa zaidi ya shilingi milioni 10, imekabidhiwa CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 13 Januari, 2018 tuliitwa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Kamati ya Fedha, Kamati ya Ulinzi na Usalama DC, pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa. Tukaambiwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, kuanzia hivi ninavyoongea na ninyi hapa tulipo, tumekaa tangu asubuhi na siku ile Mheshimiwa Lukuvi alikuja, akatuacha pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu asubuhi tumekaa, saa
8.00 anakuja anatuita anasema, nimeagizwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nendeni mkakabidhi Stendi Kuu ya Mabasi ya Babati kwa CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe. Huyo ni mama yangu, sina sababu ya kumjibu. Naomba niendelee tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyoitwa tukatakiwa tukabidhi stendi, labda nimsaidie tu, yeye haingii kwenye Baraza la Madiwani la Mji wa Babati. CCM hawajawahi kuomba kumilikishwa stendi, hata ombi tu, acha kumilikishwa, hawajawahi kuomba. Kwa hiyo, kilichotokea, tukatoka hapo tukarudi kwenye Halmashauri yetu. Terehe 2 Machi, wakati tumeondolewa hapo hatukuruhusiwa hata kuhoji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipohoji Barua ya Mheshimiwa Rais iko wapi? Tulijibiwa, Mheshimiwa Mkuu wa MKoa akasema, Mheshimiwa Mbunge, sifanyi masuala ya kitoto. Nikamwambia, Mheshimiwa Rais kama anataka kukabidhi stendi CCM, anaandika kwako. Tuoneshe hata tuone. Akasema atatuletea kwenye Baraza la Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Baraza la Madiwani, hatukuletewa barua wala Kumbukumbu Namba ya Barua ya Rais ya kukabidhi stendi, mali ya wananchi kwa CCM. Tukakatazwa kujadili kwenye Baraza la Madiwani. Nchi hii hakuna utawala bora. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyekiti wa Halmashauri akaandika barua tarehe 2 kumtaka Mkurugenzi Baraza Maalum, Waziri wa TAMISEMI anijibu, tangu lini Baraza la Madiwani linakatazwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi akakimbia akaenda kwa Mkuu wa Mkoa, akapeleka barua tarehe 5, anaomba mwongozo kwa Mkuu wa Mkoa kana kwamba hajui kazi yake kama Mkurugenzi. Mkuu wa Mkoa tarehe 6 akajibu akasema haoni mantiki ya Baraza la Madiwani kujadili amri ya Mheshimiwa Rais. Hivi mna utawala bora?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 8 Mwenyekiti akaandika mwezi wa Tatu tunaomba tukae tujadili, hiki ni chanzo kikubwa. Wakasema, shut up. Hakuna kujadili. Tukaomba, Mwenyekiti wa Halmashauri na Madiwani waende kwa wananchi kwamba stendi yetu imepokonywa na CCM. Polisi wakakataza wasiende kwa wananchi wawaambie kilichotokea. Kuna utawala bora? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kubomoka. Sasa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora mnijibu yafuatayo:-
Ni kwa nini barua ya Mheshimiwa Rais ninyi Mawaziri hamkupewa nakala? Kwa nini anaandikiwa Mnyeti? Hierarchy ya information katika nchi hii ninyi ni Mawaziri, kwa nini ninyi hamjaandikiwa, mnijibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kwa nini mmeshindwa kumshauri Mheshimiwa Rais kwamba CCM; maana sisi tulioitwa kwenye Baraza, mchakato wa muda mrefu, walitunyang’anya kwanza uwanja wa wanafunzi ekari nane tukaurudisha. Tena Katibu Mkuu wa TAMISEMI ananisikia yuko humu ndani. Barua yake ikapuuzwa, Mkuu wa Mkoa anasema hatambui barua ya Katibu Mkuu kwamba uwanja ni wa wanafunzi. Tulivyozuia uwanja, wakatunyang’anya stendi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini ninyi Mawaziri mnaogopa kumshauri Rais? Kama alivyosema Mheshimiwa Malocha hapa, kwa nini mnaogopa kumshauri Mheshimiwa Rais wakati amelishwa matango pori? Naomba mnijibu, ni kwa nini ninyi mnakubali chanzo kikubwa cha Halmashauri kama hiki kinachukuliwa na ninyi mkiwa mnaangalia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mnijibu yanayoendelea Babati, kwa sababu kengele imelia. Sasa hivi kinachoendelea, CCM walivyokabidhiwa stendi, wale wafanyabiashara ambao wana mkataba wa miaka 31 mpaka 2031 na Halmashauri wameambiwa ninyi sio wamiliki, wapangaji ndio wamemilikishwa. Sasa hivi kuna vita Babati kati ya wapangaji na wamiliki wa vibanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Mawakala wa Halmashauri wanaokusanya ushuru wa Halmashauri walifukuzwa kama mbwa, stendi pale CCM wamepeleka green guard. Huu ubabe wa CCM mpaka lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wamepeleka notice wiki ya pili wanaishtaki Halmashauri. Hiyo fidia ya kuwalipa wafanyabiashara kupoteza vibanda vyao tunatoa wapi? Mawakala wameishtaki Halmashauri wamepeleka notice ya mwezi mzima, according to sheria. Wiki ya pili sasa, mnategemea tutalipa hizi fidia kutoka kwenye chanzo gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba leo vyombo vya habari, usalama wa Taifa, mkamwambie Rais, Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kwamba Babati kumechafuka. Kwa sababu ninyi mnaogopa kumshauri Rais, tunamtaka Mheshimiwa Dkt. Magufuli aje ajibu Babati, ni kwa nini anachukua stendi ambayo tumemiliki tangu mwaka 2004 mpaka leo wanakabidhiwa CCM? Mungu alivyo mwema, Ofisi ya Mkoa CCM na Wilaya wameanza kupigana kwa sababu ya shilingi milioni 10. Vita vimehamia ndani sasa hivi wanagawana ruzuku. (Kicheko/Makofi)
T A A R I F A . . .
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nimesema wafanyabiashara na wapangaji wamegonganishwa; wamiliki wamenyang’anywa, wapangaji wamekabidhiwa vibanda, moto unafukuta, lakini inawezekana hata mali za wafanyabiashara zikachomwa moto kwa sababu waliotolewa wana uchungu na vibanda vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fukuto lingine, CCM wanagawana hiyo ruzuku ya shilingi milioni 10, moto umewaka kati ya mkoa na wilaya, wanapigana vikumbo. Vile vile Halmashauri imeshtakiwa na Mawakala kwa kuvunja mkataba; Halmashauri imeshtakiwa na wananchi kwa stendi yao kukabidhiwa CCM; na Halmashauri imeshtakiwa na wamiliki wa vibanda wenye mkataba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu hii hoja tunaambiwa ni barua ya Rais. Tunaiomba hiyo barua tupewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, group la wazee wa CCM na wananchi wa Babati walikuja kumwona Waziri Mkuu mwezi wa Pili…
T A A R I F A . . .
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, no research, no right to talk. Sisi ndio Baraza la Madiwani tunaopokea maombi ya yeyote anayeomba ardhi awe CHADEMA, awe CCM. Sasa wewe unayeongea huko ulikuwepo kwenye Baraza au kwenye Kamati ya Mipango Miji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawajawahi kuomba wala hawajawahi kumiliki. Naomba record iwe sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuja kumwona Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Halmashauri na Madiwani na wazee; akatukaribisha vizuri miezi miwili iliyopita, akasema atapeleka kwa Mheshimiwa Rais. Mpaka leo hakuna majibu. Maana yake kama inafikia hatua mpaka level ya Waziri Mkuu tunakuja hamtupi majibu, halafu tunaambiwa kuna barua ya Mheshimiwa Rais; hivi barua ya Mheshimiwa Rais kwa rasilimali ya nchi ni siri?