Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Tumbe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RASHID A. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia leo hii kusimama hapa nikiwa na afya. Pia, nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ndiyo roho ya nchi hii na Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wote wamo kwenye TAMISEMI. Nachukua fursa hii, katika uhai wangu wa miaka nane sasa ya Bunge, kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Naibu Mawaziri wake kwa kazi ambazo wanazifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, natoa ushauri kwamba wale Wakurugenzi wa Halmashauri wapewe nafasi ya kupewa zawadi maalum kwa wale wanaofanya vizuri na kama inawezekana kwa kila bajeti waweze kutangazwa Wakurugenzi ambao wamefanya vizuri katika Halmashauri zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni pongezi tu. Leo nitahamia kwenye utawala bora zaidi. Duniani kote tunahitaji utulivu, amani na demokrasia ya kuendekeleza uchumi wa Taifa. Kama hatutaweza kudumisha utawala bora, hatutaweza kabisa kuendesha Taifa hili. Utawala bora kwa tafsiri yake, umeenea kila pembe ya Taifa hili. Kwa umuhimu wa utawala bora, nimeamua leo nijikite kwa makusudi kujadili kwa undani zaidi kuhusu shughuli za Serikali yetu juu ya utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu wa utawala bora ndiyo maana katika Dua yetu tunayoliombea Bunge na Taifa huwa tunasema “Mjalie Rais wetu pamoja na wanaomshauri wadumishe utawala bora.” Hii imeingizwa katika Dua ili wanaomshauri wawe karibu kumwambia Rais ajitahidi kusimamia na kutekeleza utawala bora katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, niseme utawala bora ni kusimamia Katiba na Sheria ya nchi. Utawala bora ni kusimamia utawala Sheria; ni kusimamia demokrasia ya kweli; ni kusimamia misingi mikuu ya uchumi ili kuendeleza Taifa hili; na kusimamia haki, usawa na uwajibikaji. Tukifika hapo sote, basi tutakwenda vizuri, wala hakutakuwa na mivutano katika Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba yetu sasa kuna dalili zote za kuchezewa chezewa. Demokrasia hasa ya vyama vingi inapigwa vita na kushambuliwa kabisa. Yote haya yanaleta athari kwa Taifa letu. Kwa maana hiyo ile kasi ya maendeleo ya haraka inakwama sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu kwa heshima yako nisome maelezo ya aliyekuwa Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora wa 2014 na 2015 Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Mkuchika. Alisema hivi, migogoro ya ardhi, mauaji ya albino na vikongwe, wananchi kujichukulia sheria mikononi, rushwa pamoja na ujangili, vimesaidia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa Tanzania katika kiwango cha utawala bora duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aliendelea kusema kwamba Tanzania ilikuwa ikishika nafasi ya 10 katika miaka miwili iliyopita na kuongeza kwamba kuporomoka huko kumekithiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu. Aliendelea kusema kwamba duniani tuko katika nafasi ya 102 kati ya nafasi 176. Hii ni nukuu ya Mheshimiwa Mkuchika alipokuwa Moshi alipokuwa akitoa maelezo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimenukuu haya nikiwa najielekeza katika kitabu cha Mheshimiwa Mkuchika, kuona ni kiasi gani ameeleza katika kitabu chake hiki kuhusiana na matokeo mbalimbali yaliyotokea nchini mwetu. Jambo la kusikitisha kabisa katika ukurasa wa 112, alieleza mistari miwili tu tena katika majumuisho. Kwa hiyo, sidhani kama ile Dua tunayosoma, sijui kama inatakabaliwa au kuna wachawi humu ndani au vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na makundi yanayofanya utekaji. Makundi haya toka yateke watu sijaona hata siku moja mtu mmoja kufikishwa Mahakamani. Nchi ambayo ina usalama wa uhakika na wa kuaminika kabisa, ni juzi tu vijana wetu kule Mtambwe sita walitekwa wakaenda maeneo yasiyojulika, wamerudi watatu wako taabani, wamepigwa na kuteswa na watatu hadi leo hawajaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utesaji na uuaji. Vitendo hivi vingi vinatokea sana katika nchi ambazo zina dalili ya kukosa utawala wa sheria. Vitendo hivi vya kivamizi ni ukiukwaji mkubwa wa sheria, ni uvunjaji wa amani na ni kinyume na haki za binadamu na utawala bora. Watu mbalimbali wanaotekwa hutekwa kwa sababu ya maoni yao au kujieleza kwao; na haki hii imelindwa chini ya Katiba ya Ibara ya 18; lakini haki hii pia imelindwa chini Mikataba ya Kimataifa Ibara ya 19 inayoshughulikia haki za kiraia na haki za kisiasa za mwaka 1986. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia haki hii imelindwa katika Ibara ya (9) ya Mikataba ya Kimataifa kuhusu Haki za Binadamu ya mwaka 1986. Kwa hiyo, sioni sababu yoyote kama kuna watekaji wanaowateka Watanzania, kuna wauaji wanaowaua Watanzania, hakuna hata mmoja aliyehojiwa na kupelekwa Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza hapa, hatuzungumzi kwa vyama, tunazungumza kama Wabunge na tunapozungumza hapa, tunaiambia Serikali, wanakoelekea ni kubaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru una mipaka yake, lakini pale anapoonekana mtu amekwenda kinyume na sheria yoyote nyingine, sheria ichukue mkondo wake. (Makofi)
Hivi sasa kuna watawala, kuna wanasiasa hasa Wapinzani, kuna Wanahabari, kuna vikundi vya dini, kuna wafanyakazi...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)