Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisahihishe kidogo jina langu naitwa Mwalimu Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie na mimi kwenye Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na ninaomba nianze kwa kusema kwamba kwa muda mrefu sana wakulima Watanzania wamesahaulika sana. Takwimu zilizoonyeshwa hapa kwenye hotuba hii, wote nadhani tumesoma, tumeona kwamba sekta ya kilimo imeendelea kushuka mwaka hadi mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kwa mfano mwaka 2015 tumeambiwa kwamba kilimo kilikua kwa asilimi 3.1, lakini mwaka 2014 tunaambiwa kilikua kwa asilimia 3.4. Ikumbukwe kwamba siku za nyuma huko mwaka 2009, kilimo kimeshawahi kukua kwa asilimia hadi 5.1. Hivyo ni dhahiri kwamba wakulima wamesahaulika, japokuwa sasa Sekta hii ya Kilimo inaajiri Watanzania walio wengi, lakini wamesahaulika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaambiwa kwamba uzalishaji wa mazao ya nafaka, hivyo hivyo umeendelea kushuka mwaka hadi mwaka kama tulivyoambiwa kwamba mwaka 2015 mazao ya nafaka uzalishaji ulikuwa tani milioni 9.8, lakini hivyo hivyo tunaambiwa kwamba mwaka 2015 umeendelea kushuka.
Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba wakulima wamesahaulika na zaidi kwa nini tumefikia mahali hapa? Tumefikia hapa kwa sababu Serikali haijachukua hatua ambazo zinaweza kuwasadia wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Serikali imeshindwa kuwapunguzia wakulima wetu mbolea, wananunua mbole kwa bei kubwa sana na imefika mahali mkulima mwingine anaamua kuahirisha kulima kwa sababu mbolea ipo juu sana. Hali hii ikiendelea, wakulima ambao ndio wengi zaidi katika Taifa hili, siku moja wataungana na kusema sasa basi, inatosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Waziri wa Kilimo yuko hapa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na Naibu wake, naomba wakumbuke kwamba wako waliowatangulia mbele akiwepo ndugu yangu Mheshimiwa Wassira, lakini yuko aliyekuwepo Naibu Waziri Mheshimiwa Godfrey Zambi na mwingine Mheshimiwa Chiza; leo hawapo kwenye Bunge hili kwa sababu ya ugumu wa kilimo katika Taifa hili.
Mheshimiwa Waziri, kama hamtakuwa makini katika suala hili, kama hamtakuwa tayari kuwasaidia wakulima wa Tanzania, kupunguza bei ya mbolea, kutafuta masoko kwa wakulima wetu ni dhahiri kwamba hali itakuwa ni mbaya kweli kweli, na ninyi nadhani mpaka mwaka 2020, mnaweza mkafuata nyao za akina Mheshimiwa Wassira, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba nchi ndogo kama ya Malawi, imefika mahali inauza mbolea kwa bei ndogo sana; inauza mbegu kwa bei ndogo sana kwa wakulima wake, lakini mbolea hiyo inapita kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Ingekuwa ni jambo la busara sana kwenda kuiga kwa wenzetu wanafanya nini hadi mbolea yao wanauza kwa bei ndogo wakati wanaipitisha kwenye bandari yetu, wanatoa na ushuru wa bandari, leo wao wanauza kwa bei ndogo. Nadhani suala hili tungeweza kufanya utafiti tujue ni kwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana, ninaambiwa kwamba mwaka 2014 pesa kwenye mbolea zilitengwa shilingi bilioni 96, tukaambiwa mwaka 2015 zilitengwa shilingi bilioni 78 kwa ajili ya mbolea, lakini mwaka huu pesa zilizotengwa kwenye mbolea tunaambiwa ni shilingi bilioni 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna hii hatuwezi kusonga mbele! Hali ni mbaya kweli kweli na ni dhahiri Serikali hii haitaweza kwa kweli kuwasaidia wakulima na haina nia njema na wakulima wetu. Huyu Rais wetu anayesema kwamba mniombee Watanzania, ajue kwamba wengi wao ni wakulima. Sidhani kama wanaweza wakamwombea kama hatawasaidia kwenda kupunguza kodi katika mbolea na kuongeza fedha katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosikitika kingine ni kwamba tunaambiwa wenzetu zao lao la korosho wamepunguza ushuru; ushuru wa Chama Kikuu cha Ushirika, lakini kuna ushuru wa usafirishaji, ushuru wa mnyaufu, ushuru wa Bodi ya Korosho, ushuru wa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika; kwenye korosho wamepunguza ushuru huu na tozo hizi.
Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho atuambie na sisi wakulima wa kahawa kama mna mkakati wa kupunguza ushuru kwenye kahawa. Kwa sababu kumekuwa na mzigo mzito sana, imefika mahali mkulima wa kahawa anatozwa ushuru wa Bodi ya Kahawa, ushuru wa utafiti (TACRI) kule mkulima analipia, wakati Serikali ingeweza kabisa kuwasaidia wakulima hawa. Vile vile kwenye Halmashauri, wakulima wa Kahawa pia wanatozwa ushuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho, atawatangazia neema wakulima wa kahawa nchi nzima kwamba tumeamua tupunguze ushuru kwenye mazao haya, maana huu utakuwa ni ubaguzi wa hali ya juu sana kama utapunguza kwenye korosho halafu kwenye kahawa ukaacha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze suala linguine. Wakulima wa kahawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wanaomba Serikali ianzishe mnada kuliko ilivyo leo ambapo wanapeleka kahawa yao Moshi ambapo kuna mnada, wakati asilimia 90 ya kahawa inayouzwa kwenye mnada wa Moshi, inazalishwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo wakulima hawa wamenituma, wanaomba tuwe na mnada wa kahawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, watu wa Ruvuma na Mkoa mpya wa Songwe ikiwezekana waje Mbeya wauze kahawa yao pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakumbusha tu kwamba Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hili ni eneo la muhimu sana. Siku hizi tuna uwanja wa ndege pale Songwe. Kwa hiyo, mazingira yanaruhusu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho atatuambia kwamba suala hili atakubaliana na wakulima wa kahawa wa Kanda za Juu Kusini kuweza kuanzisha mnada wa kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la NFRA kutenga fedha za kununua mazao ya nafaka. Msimu uliopita wakulima wetu wamekopwa mahnidi na wengi hadi sasa walilipwa nusu imefika mahali hawawezi tena kununua mahindi, wamekosa mtaji kwa sababu Serikali kwa jitihada za makusudi kabisa imeamua kuwafilisi wajasiriamali.
Msimu huu tunapokwenda kununua mahindi, naomba Serikali isiwakope wananchi. Ikiwezekana itenge fedha kabisa ya kwa ajili ya kwenda kununua mahindi ya wananchi bila kuwakopa. Wakiendelea kuwakopa wananchi ambao ni maskini na wengi wao pesa wanakopa benki, tunawalipa nusu nusu, hatutafika na mwisho wa siku tutakuwa hatuwasaidii wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni la msingi zaidi japokuwa wengine wameshaligusia sana, ni mfumo wa kugawa voucher. Mfumo wa usambazaji wa voucher siyo rafiki kwa wakulima wetu. Imefika mahali watu wanagawa voucher wanaangalia, huyu ni ndugu yangu, huyu ni shemeji yangu, huyu ni nani! Leo Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani wamekosana na wananchi kwa sababu pia nao wanaambiwa kwamba mnapendelea na mnabagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mfumo huu wa voucher ikiwezekana tuufute kabisa na badala yake mbolea iweze kupunguzwa bei, tupunguze ushuru kwenye mbolea na baada ya hapo mbolea ipatikane nchi nzima kwa bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa tukifanya hivi wakulima wetu itafika mahali watafarijika na wataendelea vizuri kabisa, watalima, tutapata mazao ya biashara na chakula; lakini mambo yatakwenda vizuri kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia naomba niseme kwamba leo tuko mahali hapa, lakini nasikitika sana, kuna watu ambao bado hawajalipwa fedha zao za mahindi waliyopima.
Naomba kwa sababu Waziri yuko mahali hapa, ikiwezekana aonane na Mbunge wa Jimbo la Mbozi ili nimwambie ni akina nani hawajalipwa mahindi yao na ni kwanini Serikali inakopa wananchi mahindi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini inafika mahali inawadhulumu na wengine masikini? Hatuwezi kukubali kabisa! Tumesema kwamba sasa inatosha, lakini tukiendelea na utaratibu huu tutakuwa tunawaumiza wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.