Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru sana, pia nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi yake kubwa anayoifanya, ama hakika amepita Singida, amefungua kiwanda kikubwa sana cha alizeti na ni kiwanda kikubwa East Africa, niwaombe yale maelekezo aliyotoa sasa yatekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru pia na kumpongeza mzee wangu Mkuchika alivyoweza kuzingatia agizo la kuwarudisha wale watumishi wa darasa la saba, tunakushukuru sana. Nimshukuru kaka yangu Mheshimiwa Selemani Jafo na Naibu Mawaziri ama hakika TAMISEMI imetulia. Yapo mambo mengi sana ambayo wameyafanya sina sababu ya kuyaelezea, lakini mambo machache niwashukuru tumepata fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Sokoine na ujenzi unaendelea vizuri. Kama haitoshi mmekwenda mbali na hata majirani zangu mmewapa pia fedha za kujenga Hospitali za Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkalama mmewapa shilingi bilioni 1.5 wanajenga Hospitali ya Wilaya, lakini pia hata Singida DC wanajenga Hospitali ya Wilaya kule eneo la Ilongero, nawashukuru sana ndugu zangu mmetupunguzia mzigo mkubwa, ama hakika sasa mmepanua wigo wa watu kupata huduma ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la afya ndugu zangu Singida Mjini tunalo tatizo hatuna hospitali ya Wilaya, tumepewa fedha zaidi ya shilingi bilioni 2.3 za kujenga Hospitali ya Rufaa tayari fedha zile zimeshakwenda na Hospitali ya Rufaa inaendelea vizuri. Ninawaomba, hili nilishalieleza kwenye Wizara ya Afya kwamba majengo ama Hospitali ya Mkoa iliyoko pale sasa hivi itakapohamia kwenda Hospitali ya Rufaa ni vizuri yale majengo tukayatumia kama Hospitali ya Wilaya ikishindikana basi mtupe fedha ya kujenga Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende eneo lingine, katika hotuba ya Waziri ukurasa wa 58 umezungumzia programu za kujengea uwezo Halmashauri za Miji na tayari Halmashauri ya Manispaa ya Singida tumeshaweka mpango kabambe tunayo master plan. Ninaiomba Serikali iende mbali zaidi tunapoweka master plan nini malengo yake, malengo yake ni kuelekea kwenye Jiji, sasa mtupe mwongozo wa kupanua ule Mji wa Singida ili tuweze kuwa na Jiji. Mnajua tayari Serikali imeshahamia Dodoma sehemu ya kupumulia ambako ni karibu na Dodoma ni Singida. Tukuombe Mheshimiwa Waziri hili tuliwekee mkakati, Mkoa wa Singida uwe mkoa wa kimkakati kwa ajili ya kuisaidia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niangalie eneo lingine ambalo ni vizuri pia nikalielezea la asilimia 10; asilimia tano kwa vijana na asilimia tano kwa akina mama. Ninashauri eneo dogo, nishukuru Serikali imeondoa riba, lakini hapa tatizo kama ambavyo wamesema wenzangu haikuwa kwenye riba, tatizo ilikuwa ni utoaji wa hizi fedha.
Sasa naomba nishauri ni vizuri Serikali ikawa makini mtupe mwongozo na mzielekeze Halmashauri zifungue akaunti maalum ili kuweza kuweka fedha hizo moja kwa moja hili litatusaidia sana, lakini tuweke sheria kali kwa sababu hata marejesho yake, mpango wa kuleta marejesho ya zile fedha haueleweki na hii ndiyo inatupa mazingira magumu ya kuweza kuwapa na wengine fedha hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda haraka kwa sababu yako mambo mengi ya kuzungumza, tunalo soko kubwa la vitunguu. Nilishaomba awali hapa tujengewe soko lile na Serikali iliji-commit kujenga lakini mpaka sasa haijajengwa. Umezuka mgogoro, yako maelekezo ambayo wanaelekezwa wafanyabiashara wetu kwamba sasa waende wakafungashe ule mzigo (packing) shambani badala ya kwenye soko. Sasa tunataka kujua maana ya soko ni nini? Kama sasa watu wanaamua kwenda kufungasha shambani mwekezaji anatoka Kenya, Uganda aende shambani kwa mkulima, tunachojua akienda shambani maana yake atamuonea mkulima, tunataka mapato. Tunataka kuona maana ya soko yaani umuhimu wa soko uonekane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka nikuombe Mheshimiwa Waziri uje Singida, tufanye mkutano tuweze kuondoa mgogoro huu wa soko na ikiwezekana soko hili la vitunguu liweze kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko eneo lingine la Waheshimiwa Madiwani kwa kweli ni jambo jema sana na wanafanya kazi kubwa sana, ni vizuri Serikali ikafikiria namna ya kuwaongezea posho yao ili waweze kufanya kazi yao vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kuna eneo moja hapa ni vizuri nikawakumbusha Serikali, miaka minne, mitano nyuma alitokea Mzee Loliondo tulimwita Babu wa Loliondo, tulikuwa tunaenda kupata kikombe cha babu. Watanzania wote walielekea kwenda Loliondo na Serikali iliamua kuhakikisha inatengeneza miundombinu ya barabara inayoenda huko na kujenga minara ya simu, lakini hatukugundua tatizo nini la Loliondo. Hatukugundua tatizo ni nini Watanzania wameamua kuondoka kwenye hospitali zetu tulizozitegemea wamekwenda Loliondo. Anamtoa mgonjwa yuko ICU anapelekwa Loliondo!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitarajia kuiona Serikali inatathimini ni wapi tumefeli mpaka Watanzania wote wameamua kwenda kwenye tiba mbadala. Nataka kusema nini hapa, tumeamua sasa kuhakikisha kila kata iwe na kituo cha afya na kila kijiji kiwe na zahanati na Hospitali za Wilaya. Serikali imejikita kwenye Hospitali za Wilaya naomba ije na mkakati tusirudi kule kwenye tiba mbadala, ije na mkakati wa kuhakikisha kwamba huu utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambao tumeuelekeza ili uweze kutekelezeka kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajifunza hapa Loliondo ninajifunza pia na utawala bora leo. Nataka nilieleze kidogo eneo hili la utawala bora, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ametoa tamko na ameweza kufanikiwa akina mama wamekwenda pale zaidi ya 2000, jambo hili nilitaka Serikali itusaidie Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amefanya jambo jema sana.
Mimi nataka nimpongeze kwenye eneo hili, lakini nataka nifike mahali nishauri, ninampongeza kwa sababu ameonesha kabisa iko mifumo ya Serikali imeshindwa kufanya kazi yake. Kama tunayo Mabaraza ya Kata, tunalo Dawati la Kijinsia, tunao Ustawi wa Jamii mifumo hii yote imeshindwa kufanya kazi yake, tunazo taasisi za dini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akatokea mtu mmoja akasema na watu wakafika wakaitikia, hapa tunajifunza jambo, mifumo hii ime-collapse. Sasa Serikali inachukua hatua gani? Lakini nataka kujifunza jambo lingine, anapata wapi legal authority ya kuamua kutekeleza haya ambayo wanayasema leo. Kama ni jambo jema Serikali itusaidie, iamue sasa na Wakuu wa Mikoa wengine waamue kufanya utaratibu huo alioufanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kama ni jambo jema tumpe legal authority aweze kutekeleza kama ambavyo amefanya, lakini tukiacha hivi akafanya, maana yake tunataka kuwapa mzigo wanafamilia hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anatoa bima za afya, jambo jema sana lakini tunao watoto yatima hawana baba wala mama, hakuna mtu aliyetoka akasema watoto hawa nao wapewe bima ya afya. Niiombe sana Serikali iliangalie jambo hili, jambo hili litatuletea mgogoro mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa pili niwakumbushe pia alitokea mama mmoja wa Tanga, Mheshimiwa Rais aliamua kufanya natural justice ya kumsikiliza. Yule mama mjane alisikilizwa na alieleza mambo yake yote pale kwenye ule mkutano, lakini Mheshimiwa Rais hakuamua, alichokiamua ni kupeleka kwenye mfumo rasmi na leo yule mama yupo jela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiki kinachofanyika maana yake umeshawasikiliza watu, ukishawasikiliza warudishe kwenye mifumo rasmi iliyowekwa na Serikali, ikiendelea hivi ilivyo maana yake kila mtu atakuwa naamka leo anafanya jambo tumekaa kimya. Nataka niiombe Serikali kwenye eneo hili tuwe makini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu ameonesha uwezo mkubwa sana na hata wa kuendelea kusimamia matatizo ya wananchi. Ametambua utawala bora maana yake nini na ameweza kutekeleza. Sasa wasaidizi wake nao watambue utawala bora, ile mifumo hata kama ime-collapse na yeye ndiye anayoisimamia, arudi kwenye mifumo rasmi, awarudishe kule ifanyike natural justice wasikilizwe kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira mengine atusaidie pia, likiisha hili la akina mama lakini pia akina baba nao waliachiwa watoto akina mama wameondoka nao pia waitwe waweze kusikilizwa, tutakuwa tumeweza ku-balance suala la equality, tunazungumzia usawa. Usawa haupo upande mmoja tu, usawa upo pande zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niiombe Serikali kwenye eneo hili tusilichukulie mzaha, nchi leo kila mama leo ameelekea kule. Sisi tuliozaliwa na kulelewa kwenye single mother family tunajua uchungu wake. Kauli tu ya Mkuu wa Mkoa mama anashangilia hajapewa chochote, kauli tu ya kusikilizwa, maana yake mifumo yetu huku chini haisikilizi, mifumo yetu huku chini yawezekana haiwezeshwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.