Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa fursa hii nichangie hoja iliyopo mezani inayohusu Wizara hizi mbili, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli siyo kujipendekeza, sitaki kusema najipendekeza, nataka kusema kweli kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano imefanya mambo makubwa sana na kwa vile Wizara hii inayohusika ni Waziri ambaye ni Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, sifa nyingi zinazokwenda kwenye Wizara hii zinakwenda kwa Mheshimiwa Rais, Mawaziri wote wawili na Naibu Mawaziri wote wawili na watendaji wote wa Wizara hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na afya; Serikali imefanya kazi kubwa sana hasa kwenye Jimbo langu licha ya mambo makubwa kwenye Mkoa mzima lakini Jimbo langu limepata milioni 500 za kusaidia kituo cha afya, ime-upgrade vituo vitatu vya afya, lakini vilevile imetoa fedha za kukarabati zahanati zote katika Jimbo langu, kwa nini nisiseme ukweli kwamba wamefanya kazi, siyo kujipendekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie hata wale ambao wanasema tunajipendekeza wangepata fursa hii ya kupata hivi vitu ambavyo tumepata na roho nzuri kama za kwetu wangeshukuru. Hawa watu wana roho mbaya, wamepewa vitu, wamepelekewa maendeleo katika maeneo yao hawashukuru, wamekalia kusema mabaya. Serikali hii hakuna nafasi ya kuilaumu, iko nafasi ya kuipongeza tu basi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema mambo yanayohusu afya kwamba Serikali wamefanya nzuri sana Serikali, lipo jambo ambalo ndiyo sehemu kubwa ya uchangiaji leo. Suala la elimu; TAMISEMI imefanya kazi kubwa sana, wametoa elimu ya msingi mpaka sekondari bure nchi nzima, haijapata kutokea, kama ilitokea ni katika nchi nyingine siyo hapa kwetu. Sasa huku nako siyo kusema ukweli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama meli imeenda Zanzibar inafika na mawimbi yapo lakini inafika, sasa kama kuna mawimbi kwenye suala la kusomesha watoto bure, yapo matatizo sijui ya walinzi, imepungua sijui kufyeka majani, hayo ni mawimbi lakini hatuwezi kutoa meli kwenda Zanzibar kwa sababu tu kuna mawimbi. Iko haja ya kusimamia mfumo huu wa elimu bure katika kiwango ambacho kinatakiwa na mapungufu madogo haya yanaweza kusahihishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo moja kubwa ambalo nataka kuliongelea kuhusu elimu. Wapo wataalam wa lugha wanaweza kunisahihisha na kunisaidia, nchi yetu inasomesha watoto wetu kwa lugha ya kiingereza, kutoka shule ya msingi darasa la kwanza mpaka la saba wanasoma kiswahili, wakifika darasa la saba watoto wetu hawa wanabadilisha elimu kama mawimbi ya redio kutoka TBC 1 kwenda TBC 2, vilevile wanabadilisha mawimbi kutoka labda ZBC 1 kwenda ZBC 2, kutoka kiswahili kwenda kiingereza. Ulipoanza mfumo huu kulikuwa na kipindi cha watoto wa form one kukaa wiki nne shuleni, shule ya upili kabla ya kuanza masomo wakisoma lugha ya kiingereza, siku hizi mfumo huo haupo. Kwa hiyo, wanatoka shule ya msingi wanakwenda kusoma kiingereza, hawaelewi! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumewapa watoto hawa mizigo miwili; kwanza wajifunze lugha ya kufundishiwa, vilevile wajifunze masomo yale ambayo wanatakiwa wayasome kwa kiingereza. Tatizo hili limekuwa kubwa sana, lakini bila kujua kwamba tumeingizwa kwenye vita vya ukoloni mambo leo. Wapo watu na zipo nchi ambazo hazitaki tuwafundishe watoto wetu kwa lugha ya kiswahili ambapo wataelewa zaidi kuliko kiingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mfumo miaka iliyopita kwamba tutafundisha watoto wetu kwa lugha ya kiswahili na wataalam wakaandika vitabu. Mimi nilikuwa mmoja kati ya watu walioandika vitabu, niliandika vitabu viwili kwa ajili ya somo la umeme, nina kitabu kinaitwa Mwandani wa Fundi Umeme (Pocket Book for Electrical), nina kitabu kinaitwa Misingi ya Umeme na Sumaku (Basic Principles of Electronic and Magnetism). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitabu hivi vipo vya kiswahili, watoto wanapenda kuvitumia, lakini mitihani inakuja kwa kiingereza, matokeo yake vitabu hivi havitumiki. Wapo wataalam walioandika vitabu vya kemia na fizikia lakini vitabu vile watu wanakata tamaa, mimi mpaka nimezeeka nimakata tamaa sasa vitabu vyangu haviwezi kutumika na nimekuwa kama niliota na baadae nikaamka asubuhi hakuna kilichofanyika. Lugha ya kiswahili ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matumizi ya lugha ya kiswahili ni muhimu ili kuendeleza elimu yetu, na kwa kuwa kukandamizwa kwa matumizi ya kiswahili katika shule zetu sasa umefikia mwisho, na kwa kuwa sasa umefika muda nchi yetu itumie kiswahili ili kunyanyua elimu yetu, na kwa kuwa tunae Mheshimiwa Rais ambaye amekuwa anatoa maamuzi magumu kwa faida ya nchi yetu na kwa faida ya wananchi wa Tanzania; kwa mfano reli ya standard gauge aliisema imetekelezwa, amesema mambo ya ununuzi wa ndege imetekelezwa, amesema mradi wa umeme wa Rufiji, tumeambiwa tusiseme Stieglers Gorge tuseme Rufiji limetekelezwa, amesema ujenzi wa ukuta kule Mererani limetekelezwa na amesema tuhamie Dodoma limetekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Rais ambaye ndiyo Waziri wa Wizara ya TAMISEMI atolee uamuzi suala la kusomesha watoto kwa lugha ya kiswahili. Suala hili linahitahitaji utafiti na utafiti umefanyika, nimesikia kwenye redio wameongea wataalam wa kiswahili kwamba walikuwa tayari lakini kwa vile Serikali haikuonesha nia ya kwenda kwenye lugha ya kiswahili suala hili likawekwa kabatini. Nina hakika mambo yalikuwa madogo kuliko kujenga reli ya kati ya standard gauge, kujenga ukuta wa Mererani na kununua ndege cash. Mheshimiwa Rais ambaye ni Waziri wa Wizara hii akitamka tutumie kiswahili nina hakika litakuwa jambo dogo kuliko kuhamia Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende upande wa Wizara hii ya Mheshimiwa Mkuchika ya Utumishi na Utawala Bora. Kila mtu akisimama hasa upande wa pili kule kumekuwa na maoni ya kutokuwa na utawala bora hapa nchini, nawashangaa sana. Wamekuwa pia wanaisakama Idara ya Usalama wa Taifa wanasema Idara ya Usalama wa CCM, jambo hili ni baya sana. Kila mtu anaamka hapa na kufanya kazi vizuri kwa sababu kuna utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lawama hizi zinatokana na watu kujua na Mheshimiwa Mkuchika anielewe vizuri, kujua kazi za Idara ya Usalama wa Taifa. Siku moja amezisema humu ndani, huenda haitoshi ni bora ifanyike elimu ya semina kwa Wabunge wote juu ya kazi ya Idara ya Usalama wa Taifa, itasaidia kwa sababu tunawakilisha watu wote nchi nzima, watu wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamewakilishwa humu. Tukipata elimu ya Idara ya Usalama wa Taifa tutaenda kuisema kule na wananchi wote wataelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Usalama wa Taifa ni kuleta amani hapa nchini, umoja na mshikamano, haya yote tunayoyaona, utulivu huu umeletwa na Idara ya Usalama wa Taifa. Kwa hiyo, ni muhimu sana wale wote wanaolaumu wakauliza vilevile Mheshimiwa George Mkuchika, Waziri wa Utawala Bora ni bora ukaandaa semina, tulifanyiwa wakati wa Bunge la Katiba, tulifanyiwa semina tukaelewa sana na haikutupa taabu kuendeleza, kutunga ile Katiba Inayopendekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.