Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kweli kwa kuweza kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kutoa opinion yangu kwa kile ambacho kinaendelea Bungeni, naona kama hatuitendei haki nafasi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanasimama, wanapongeza sana hili la darasa la saba walioajiriwa kabla ya 2004 kurudishwa. Kuna watendaji wengi na watendaji wengine kama hawa watendaji ambao wamerudishwa hospitalini, madereva ambao wameajiriwa mwaka 2004 mpaka sasa hivi ambao kosa lao si tu kuwa darasa la saba kwa sababu waliowaajiri ni Serikali hii hii, imewaondoa kazini, haitaki kuwalipa mafao ya kuwaachisha kazi, halafu leo unasimama mtu anasema tunaipongeza Serikali sikivu, sikivu what?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wamefanya makosa hawa ambao wameajiriwa mwaka 2004 kurudi nyuma at the first place hawakutakiwa kutoka kazini, wanatakiwa tuwawajibishe kwa sababu kwa kuwaondoa kazini kuna Watanzania ambao wameathirika sana. Kuna Watanzania ambao wamekufa kwenye sekta ya afya, kuna Watanzania wengi ambao wameathirika halafu leo mnapiga makofi eti wamewarudisha watendaji kuanzia hapo kurudi nyuma, kwa kweli mimi nasikitika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iwajibike kuwalipa gratuity wale watendaji wote kwa maana waliokuwa katika hospitali na kwingine kote darasa la saba ambao iliwaajiri wenyewe na imewaondoa kazini. Kama hawana fedha wanajificha kwenye vyeti fake na utendaji kuwaondoa kazini waseme kwa sababu kitu kingine, wameondoa hawa watendaji makazini wameshindwa kuwa-replace ambao sasa wanasifa stahiki. Watu wanahangaika, mmewaondoa kwenye ajira hizi halafu mnashindwa kuwa-replace hapa inaonekana kabisa kwamba Serikali haina fedha ya kuwalipa hawa watu na ni dhambi sana watu wanakufa kuondolewa kwa ghafla makazini na kutokurudishwa kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utawala bora nilisema sitachangia kabisa, lakini kwa sababu mimi ni mwanamke na ni mwanamama na najua uchungu wa kuzaa na kuona kijana wangu anapotea kwa mazingira ya kutatanisha, watu wanauawa kwa mazingira ya kutatanisha, watu wanalemazwa lakini ukiongea watu hawasikii. Nikasema katika Biblia kuna phrase moja inasema; “chozi la mwanamke lina thamani mbele ya Mwenyezi Mungu.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale akina mama wote, mama yake Ben Saanane, mama yake Mawazo, mama yake huyu Diwani wa Kigoma, mama wa Watanzania wote waliopotea, mama yake watoto wote waliolemazwa na Serikali hii ambayo haitaki kuchukua hatua; mama yake wa Diwani wetu aliyeuawa pale Hananasif katika uchaguzi wa Kinondoni anapolia chozi lake Mwenyezi Mungu atakwenda kuyalipa hapa hapa. Na mimi naendelea kuungana nao hawa wanawake kulia chozi kwa sababu na mimi ni mwanamke najua uchungu wa kuzaa, najua thamani ya mtoto anakufa bila hatia, naendelea kulia na wanawake hakika Mungu atakwenda kutenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kuchangia, kwa sababu dakika ni chache nichangie kwenye TAMISEMI, Jimbo langu la Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiisoma hii hotuba ya Waziri anaeneleza kabisa kwamba upungufu wa madarasa kwa maana ya vyumba vya madarasa kwa mwaka Julai, 2017 mpaka Machi, 2018; kwanza nimpongeze, wanajitahidi pamoja na kwamba Serikali inashindwa kutambua kwamba TAMISEMI ilitakiwa kupewa fedha nyingi sana kwa sababu ndiyo inayobeba majukumu mengi. Kama ingeweza kutekelezewa vizuri basi maendeleo yangeonekana kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza hapa kwamba yamejengwa madarasa 2,278 na hivi vyumba vimejengwa kwa asilimia 80 na Watanzania waliokuwa wanajichangisha. Upungufu ni 264,594, na vyumba tulivyonavyo sasa hivi ni 123,044. Miaka 57 ya Uhuru tume-manage kujenga madarasa 123,044 yamebaki 264,594 ukigawa kwa yale tu ambayo yamejengwa 2,278 inaonesha Chama cha Mapinduzi kitachukua miaka 116 kuweza kutatua matataizo ya vyumba vya madarasa Tanzania. Ikizingatiwa wanakuwa na matamko mengi mengi, wananchi wanakuwa wanajitolea ikiwemo wa kwangu wa Jimbo la Tarime Mjini wamejitolea sana, wamejenga mpaka kwenye lenter Serikali wanaendelea wanakamilisha…

T A A R I F A . . .

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa nasikitika sana halafu wajina wangu eti ana shule na yeye ana-own. Hiyo taarifa yako inani-support in actual sense. Tangu uhuru mpaka leo mmejenga 123,000 bado vyumba 264,594 ukijua kabisa population ya Tanzania inaongezeka, mmeleta elimu bure, mnasajili wanafunzi wengi na capacity yenu ya kujenga madarasa ni ndogo sana halafu tunaongea nini? Hivi nini ni kipaumbele chetu? Taifa ambalo haliwekezi kwenye elimu, mtafanya mengine yote lakini hatutaona uchumi ukijionesha. (Makofi/Viegelegele/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea hapa hapa kwenye elimu ukija kwenye vyoo ni matatizo, na tunajua shule ambazo tunakuta hazina vyoo vya kutosha wanafungiwa wanafunzi wetu hawaendelei. Wananchi wanajitolea kwa asilimia kubwa ndiyo wanajenga hivi vyoo ambavyo wameweka hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna siku nilisema mwaka jana wakati nachangia ambapo mlisema mmefanya re- allocation ya shilingi bilioni 39 kwenda Chato. Nikasema kwanini hata msiangalie kipaumbele mkazipeleka kwenye elimu, mkazipeleka na kwenye afya ili angalau kutatua hizi changamoto ambazo tunaziona?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu hapo hapo, walimu hawana nyumba za kuishi, na jana wakati wanajibu swali hapa wakasema wako nyumba zao binafsi au wamepanga. Mnawapa hiyo hela ya kupanga? Iko nje ya mishahara yao? Mwalimu anapanga kwa mshahara mdogo ule ule mnaomlipa, anasafiri kutoka sehemu “A” kwenda “B” kwa mshahara ule ule halafu unategemea matokeo yawe mazuri. Lazima tuhakikishe tunaweka vichochezi vya kutoa elimu nzuri kabla hatujaanza kusema kwamba tunatoa elimu bure ambayo haina tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa Tarime muweze kunikarabatia sekondari ya Tarime ambayo ni kongwe, imefunguliwa mwaka 1973, na ni sekondari ambayo ni ya high school tu na inachukua zaidi ya combination saba. Mheshimiwa Waziri nimeshakwambia sana. Vilevile kulikuwa kuna gari pale land cruiser mmeliondoa tunaomba lirejeshwe wanafunzi wale wanateseka sana. Pia nilileta maombi kwa tarime muweze kutupandishia hadhi sekondari ya Mogabiri kwa mwaka huu wa fedha unaoisha lakini pia tuna sekondari ya Nyandoto ili iwe ya kidato cha tano na cha sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka sana, Waziri unatambua kabisa tatizo tulilonalo kwenye Hospitali ya Wilaya na Mheshimiwa Kandege ulikuja na Waziri Mkuu mlijionea uhalisia. Hatuwezi kuwa tunapata basket fund ya shilingi milioni 11 Hospitali ya Wilaya wakati mnapeleka shilingi milioni 42 katika Kituo cha Afya cha Nyalwana hii si haki kabisa na ukizungatia kwenye Halmashauri yangu sijapata kituo cha afya pamoja na kwamba nahudumia Serengeti na Rorya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kwenye Mnada wa Magena. Ukiangalia kwenye hiki kitabu mapato ya Halmashauri yameshuka sana kutoka shilingi bilioni 1.1 kwa mwaka jana baada ya kuondoa mapato ya mabango na property tax kwa mwaka huu tumekusanya shilingi milioni 586 tu. Mkiturudishia Mnada wa Magena tutaweza kukusanya mapato mengi kwenye Halmashauri yetu. Hii story ya kusema kwamba Tarime sijui wizi wa ng’ombe kwanza mnatukebehi sana. Sasa hivi Tarime ni salama na ndiyo maana kuna Mkoa wa Kipolisi unaojitegemea wa Tarime-Rorya. Tunaomba kabisa ng’ombe wanatoka Serengeti haziendi Kirumi, ng’ombe wanaotoka Rorya hawaendi Kirumi wanapita moja kwa moja na wale ambao wananunuliwa kwenye Mnada wa Kirumi wanapitishwa Tarime kwa nini wasiibiwe? Tunahitaji Mnada wa Magena ufunguliwe ili uweze kutoa ajira kwa watanzania wa Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye halmashauri yangu wamekaimisha sana Wakuu wa Idara kitu ambacho kina- affect utendaji. Miaka inapita Wakuu wa Idara ndiyo wale wale naomba napo pia waweze kunibadilishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa walimu wa sayansi. Tunasema Tanzania ya viwanda, uhaba wa walimu wa sayansi ni mkubwa sana, wananchi wakawa wanajichangisha ili kuwalipa walimu waweze kufundisha Rais akatoa tamko msichangishe, ipitie kwa Mkurugenzi. Wananchi wameacha, Serikali sasa hivi hakuna maabara wala vifaa, walimu wa sayansi hamna. Tunaomba kama mmeshindwa, kwa mfano Tarime tuko tayari kuchangisha na kuajiri walimu wa sayansi ili watoto wetu wasome vizuri. Tunaomba kabisa kama Serikali imeshindwa kutoa kipaumbele…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)