Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa hii. Naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na kuweza kusimama mahali hapa leo kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabla sijaanza kuchangia na kutoa mchango wangu katika Wizara hii na mimi niungane na wenzangu Wabunge wa Mkoa wa Manyara ambao wameshachangia kusema kweli, kutoa shukrani za dhati kwa mambo makubwa ambayo Mheshimiwa Rais wetu mpendwa katika ziara zake za hivi karibuni ametutendea katika mkoa wetu. Mheshimiwa Rais amesimamia kauli yake, yeye amesema hatabagua mpinzani kwa basis ya itikadi wala ya chama wala ya dini wala ya kabila. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mfano Jimbo la Simanjiro liko upinzani na ninategemea mdogo wangu Mheshimiwa James Ole-Miliya hapa atakaposimama amshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa maendeleo makubwa ambayo ameyafanya katika Jimbo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais tunamshukuru kwa mambo makubwa mengi lakini makubwa matatu naomba nichukue nafasi hii kumpongeza nayo; la kwanza; madini ya Tanzanite ambayo yalikuwa yananufaisha watu wengine na pengine hata nchi nyingine Mheshimiwa Rais ametuletea mfumo thabiti, mfumo rasmi kuhakikisha kwamba wanufaika wa kwanza wa madini haya watakuwa Watanzania na zaidi sana hata akina mama yeyoo wa Wilaya ya Simanjiro, hususan Mererani watanufaika na madini haya. Amesema atahakikisha kwamba ukuta uliojengwa hauwaathiri wale wanawake wanaochenjua madini haya, waliokuwa wanananufaika kidogo kidogo, bali atawatengenezea mfumo rasmi waendelee kunufaika, tunamshukuru Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Rais alipokuja Mererani tulimwambia tunakuomba baba yetu tenda miujiza kwa sababu shida ya maji katika Mji wa Mererani imedumu miaka nenda rudi. Aliwaangalia wale wanawake wa Mererani wanaoswaga punda toka asubuhi mpaka jioni wakisaka maji, akasema nimelichukua hilo. Baada ya muda mfupi ametuletea mradi mkubwa wa maji wa thamani ya shilingi milioni 780, sasa hivi baada ya muda mfupi shida ya maji itakuwa historia Mererani, tunamshukuru Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu, tulimlilia, wanawake wa Mererani walimlilia, baba tunaomba msaada sisi tukipata complication ya kujifungua tunakimbizwa kwenda Kilimanjaro KCMC ama Selian kwa kutumia magari ya polisi, tunakuomba utusaidie gari la wagonjwa. Mheshimiwa Rais bila kigugumizi, bila kumung’unya maneno aliwajibu palepale nitawaletea ambulance. Juzi amekuja kufungua ukuta amekuja na ambulance yetu mkononi, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mungu ambariki. Ni dhahiri kwamba huyu ni Rais wa wanyonge. Tunamshukuru kwa moyo wa dhati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na haya yote si kwamba, Mkoa wetu wa Manyara uko salama kwa masuala mengi. Wilaya ya Kiteto inasikitisha kwa suala la ambulance haina. Tunaomba Wizara iliangalie hili kwa sababu, tangu nikiwa Kiteto gari la wagonjwa linakwenda kumchukua mgonjwa linaharibikia huko huko linatafutwa gari lingine. Tangu wakati huo hadi leo hakuna gari la ambulance Kiteto. Naomba hili Mheshimiwa Waziri alibebe na atusaidie katika nyanja hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nizungumzie suala la uwezeshwaji wananchi kiuchumi. Kwanza kabisa naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mtaalam wa microfinance. Nimefanya suala la kutoa mikopo kwa wanawake na vijana kwa takribani miaka 20; kwa hiyo, ninaelewa ninachosema, lakini niipongeze Serikali kwa kututengea shilingi bilioni 61.6 kama asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zetu kwa ajili ya wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilikuwa naomba na nia yangu ya kuzungumzia eneo hili ni kuliboresha na kuhakikisha kwamba bilioni 61.6 zinaweka impact, si kwamba zitolewe tu kwa sababu sisi kama Wabunge kazi yetu kubwa ni kuhakikisha kusema kwamba hizi fedha zitoke, hizi fedha zitoke na bado ni kidogo, lakini hatuliangalii sana suala la kusema inaweka impact kiasi gani na wanufaika wanakuja kunufaika kwa kiwango gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikundi 18,000 vilivyotajwa katika kitabu cha Waziri je, ni vikundi vya watu wawili wawili, watu 10, watu 30, kwa sababu, hatuna uhakika wanufaika ni wananchi wangapi. Maana vikundi hivyo ni vikundi tu vya wanawake na hatujui kama ni vikundi vya wanawake pamoja na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iwekwe wazi, ili tuhakikishe kwamba, fedha hizi zinazotoka kwenye Halmashauri zetu zinaweka impact sahihi na zitanufaisha wanawake na vijana, na pia nadhani tuweze kujua kwamba katika wanawake na vijana, je, hawa vijana ni pamoja na vijana wa kike ama ni vijana wa kiume? Na umri wa hawa wanawake sasa unaishia wapi, ili wao wawe wanawake wanaonufaika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina wanawake wengi wakulima na wafugaji. Sasa hawa ni wale waliowekwa pembeni na mfumo rasmi wa ukopeshaji. Je, hii asilimia 10 fedha hizi shilingi bilioni 61 zinawanufaishaje wanawake wakulima na wafugaji, ili nao waweze kunufaika na asilimia hizi zinazotoka kwenye halmashauri yetu? Nadhani Mheshimiwa Waziri atakapo wind up atatueleza. Vilevile pengine si vibaya tukajua ni criteria gani inayotumika kuwapata hawa wanawake na vijana, kila mtu anaweza akakopa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hizi fedha kama ni mikopo ni lazima zifuatiliwe, katika bajeti ya ufuatiliaji, bajeti ya kuunda vikundi, bajeti ya kuweka criteria wanawake gani wakope, inajumuishwa katika hiyo bilioni 61 ama kuna bajeti ya pembeni ya kuhakikisha kwamba fedha hizi zinafuatiliwa vizuri? Na nani wanaofuatilia, ni maendeleo ya jamii ndani ya Halmashauri ama kuna kundi la watu ambao wanaweza wakafanya kazi hii kwa ufanisi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tungeweza kuweka wazi suala la urejeshaji. Kama hizi fedha zinarejeshwa kwenye halmashauri sijui ni kwa nini basi tuendelee kutenga asilimia 10 kila mwaka? Fedha zinazorejeshwa naamini kwamba, kama ni mfuko wa kuzunguka ina maana kwamba ni fedha zinarudi ili ziweze kukopeshwa. Kwa hiyo, nina hakika kwamba zinaweza zikapunguza hii asilimia inayotolewa kwa kila mwaka kwa Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwa kifupi sana pia suala la Makao Makuu ya Wilaya yetu ya Mbulu Vijijini; Wilaya ambayo ni halmashauri mpya ambayo tunaishukuru Serikali yetu kututengea na kutupa wilaya mpya. Hata hivyo tunaelewa kwamba suala la Makao Makuu ya Wilaya ni suala la kisheria, lakini kumekuwa na kigugumizi cha kuhakikisha wananchi wanagongana vichwa kwa sababu kila mtu anatamani Makao Makuu ya Wilaya yawe mahali fulani. Sisi wananchi hatujali wa Manyara, mimi binafsi ninayechangia, ili mradi TAMISEMI ituambie, kwamba Makao Makuu ya Wilaya ya Mbulu Vijijini yawe Dongobesh kwa sababu, kwa sensa ya mwaka 2012 ina idadi ya watu 239,637 wakati Haydom iko pembezoni sana na ina idadi ya watu 80,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa masuala haya ni ya kisheria, kama Serikali ina sababu ya kuridhisha, inataka kuweka Makao Makuu Haydom, ruksa. Ilimradi wananchi sasa wawe watulivu, taarifa hii itolewe rasmi na TAMISEMI ili wananchi wetu watulie na waendeleze shughuli zao za maendeleo badala ya kuwaza usiku kucha Makao Makuu yanaweza kuwa wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nimepanga kuzungumzia kwa nguvu haya. Naendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa juhudi kubwa aliyotupa maendeleo katika Mkoa wetu wa Manyara, naomba Mwenyezi Mungu ampe maisha marefu na tunamuombea Mungu azidi kumbariki, asante sana.