Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa
Naibu Spika, awali ya yote kwa sababu ndiyo mara ya kwanza nikihudumu katika nafasi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba unipatie fursa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijaalia kusimama leo kuchangia na kutoa baadhi ya ufafanuzi katika hoja zilizoletwa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba uniruhusu kipekee nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Joseph John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kubwa kwangu kuniteua nihudumu katika nafasi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Tatu, naomba niishukuru familia yangu, mke wangu na watoto wangu kwa namna ambavyo wamekuwa wakiniwezesha kuweza kuhudumu katika nafasi hii. Nafasi ya nne, si kwa umuhimu ni kwa Chama changu cha Mapinduzi, wapiga kura wangu wa Jimbo la Kalambo kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakishirikiana nami katika kuhakikisha kwamba tunaweza kuhudumu katika nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ufinyu wa muda naomba uniruhusu niwatambue Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao mizuri ikiongozwa na Kamati yetu chini ya uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Dkt. Jasson Rweikiza na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Mwanne Mchemba, kwa maelekezo na ushauri ambao wamekuwa wakitoa katika Wizara yetu, hakika ni hazina kubwa sana kwa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite kufafanua baadhi ya hoja kabla Mheshimiwa Waziri hajaja kufafanua hoja zitakazokuwa zimebaki. Katika michango ambayo imetoka kwa Waheshimiwa Wabunge ukianzia na Kamati kuna suala zima la ushiriki wa Waheshimiwa Wabunge katika vikao kwa maana ya DCC, Mabaraza pia na kikao cha RCC.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba pale ambapo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakipata fursa ya kushiriki katika vikao hivi, michango yao imekuwa ya muhimu sana, imekuwa ikileta tija, tunahitaji sana uwepo wa Waheshimiwa Wabunge kushiriki katika vikao hivi. Ndiyo maana Ofisi ya Rais, TAMISEMI imetoa waraka ikiwaelekeza Makatibu Tawala na Wakurugenzi kuhakikisha kwamba ratiba zao ambazo wanazipanga ni zile ambazo zitazingatia ratiba za Waheshimiwa Wabunge kuweza kushiriki katika vikao hivi ili michango yao ya maana ambayo tunahitaji iweze kuchukuliwa, kwa sababu wao ndiyo wawakilishi wa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi ni pamoja na suala zima ambalo liliongelewa kwenye Kamati, hapa Bungeni halikutokea sana, lakini ni ukweli usiopingika kwamba Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakihitaji na jambo ambalo ni la muhimu kuhakikisha kwamba hata ziara za viongozi wa Kitaifa wanapata taarifa ili washiriki, maana wao ndiyo wawakilishi wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Nabu Spika, kuna hoja iliyojitokeza kuhusiana na suala zima la asilimia 10 ya mapato ya ndani kutengwa kwa ajili ya kwenda kwa akina mama pamoja na vijana. Waheshimiwa Wabunge, pia kwa wakati fulani waliongelea juu ya kuanzisha asilimia mbili kwa ajili ya kwenda kwenye kundi la watu wenye uhitaji maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mujibu wa sheria iliyopo sasa hivi ambayo haioneshi dhahiri, umeandaliwa utaratibu wa kuhakikisha kwamba kwa kupitia Finance Bill ya mwaka 2018/2019 kipengele hicho ambacho kinampa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kuingiza katika sheria hiyo kipengele ambacho kitazitaka Halmashauri zote kuhikisha kwamba wanatenga na wasipotenga Wakurugenzi wachukuliwe sheria safari hii kitaweza kwenda kuwekwa humu. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba pesa hizi zinakwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Waheshimiwa Wabunge wengi walichangia juu ya suala zima la kuwawezesha akina mama na vijana kupata elimu ya ujasiriamali. Ni ukweli usiopingika kwamba ukienda kukisaidia kikundi bila kuwa na elimu ya ujasiriamali ni sawa na unapeleka fedha ambayo una uhakika kwamba haitatumika na kuleta mapinduzi makubwa ambayo tunatarajia yapatikane kwa vikundi hivi kwa maana ya akina mama, vijana lakini pia na kundi maalum la hawa watu wenye uhitaji maalum. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba jambo hili linaenda kutekelezwa na ninaamini Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha jambo hili pia atalifafanua kwa uzuri zaidi ili nia njema ambayo imekusudiwa na Serikali iweze kutimizwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa suala zima ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kuhusiana na uanzishwaji wa TARURA. Tunashukuru kwa pongezi ambazo zimetolewa kwa maeneo ambayo TARURA imeanza kufanya kazi vizuri matunda yake dhahiri yanaonekana. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba chombo hiki ambacho kimeanzishwa kinaenda kufanya kazi ambayo tunatarajia ili yale maombi ambayo Waheshimiwa Wabunge walikuwa wakitoa/wakiomba baadhi ya barabara zao za kwenye halmashauri zao zipandishwe hadhi yanaenda kusita kwa sababu watakuwa wanaridhika juu ya utendaji wa chombo hiki cha TARURA ambacho kimeanzishwa hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Waheshimiwa Wabunge waendelee kukiamini chombo hiki, chombo hiki bado ni kipya. Tunahitaji kukiunda vizuri na Waheshimiwa Wabunge ni mashuhuda kwamba wakati TARURA inaanzishwa tumelazimika kuchukua watumishi waliokuwa kwenye Halmashauri ndiyo hao ambao wakaajiriwa. Lakini naomba niwahakikishie, vetting inaendelea kufanyika ili tuhakikishe kwamba wale tu ambao wana sifa na weledi ndiyo ambao watabaki kuendelea kutumika katika chombo hiki. Ni azma yetu kuhakikisha kwamba wale tu ambao wana ufanisi ndiyo ambao wataendelea kufanyakai TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hoja ambayo imesemwa na juu ya suala zima la kuongezea pesa TARURA. Tunakubaliana na hoja hizi ambazo zimetolewa na Serikali katika kipindi ambacho Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati fulani akiwa anatoa ufafanuzi, alisema ni vizuri tukatazama ndani ya Serikali namna bora ya kuweza kuhakikisha kwamba tunakiwezesha chombo hiki, lakini pia tukiwa na uhakika kwamba chombo hiki kinaenda kufanyakazi iliyokusudiwa na Waheshimiwa Wabunge na siyo suala tu la kuwa na bajeti kubwa ambayo haiendi kufanya kazi iliyokusudiwa. Kwa hiyo, tunaomba tukipatie fursa chombo hiki, tukijenge, tukiimarishe maana mwaka mmoja si umri mrefu. Naamini kadri siku zinavyokwenda chombo hiki kitasimama vizuri na tumepata pongezi kutoka maeneo mbalimbali ambapo TARURA imeanza kufanya kazi nzuri. Naomba nipongeze sehemu zote ambazo wamefanya kazi vizuri na wale wengine ambao wanaenda kwa kusuasua wajirekebishe, wahakikishe kwamba kile ambacho tumekusudia ndani ya Serikali kinaenda kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima ambalo limejitokeza kuhusiana na ujenzi na ukamilishaji wa zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali za wilaya. Ni ukweli usiopingika kwamba Watanzania wana kiu kuhusiana na suala zima la kupata huduma iliyo bora ya afya, kutokana na Ilani yetu ya CCM tumeliweka hili kwamba ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba kila kijiji inaenda kujengwa zahanati kwa kushirikisha wananchi lakini pamoja na kushirikisha Serikali, kila Kata tunakuwa na kituo cha afya na pale ambapo hamna hospitali ya wilaya, hospitali ya wilaya inaenda kujengwa.

Naomba niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba azma hii ya Serikali ni thabiti na ninatambua kabisa kwamba kila Mheshimiwa Mbunge sehemu ambayo hakuna kituo cha afya au hakuna hospitali ya wilaya angetamani hata leo au jana iwe imejengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, safari ni hatua, ni vizuri tukakubaliana kwamba nia njema ya Serikali ambayo imeanzishwa ya kuhakikisha kwamba tunajenga vituo vya afya, zahanati tunaenda kuifanya. Katika nafasi hii nikiwa nahudumu nimepata fursa ya kutembelea maeneo mengi, muitikio wa wananchi kuhusiana na suala zima la ujenzi wa vituo vya afya haitiliwi mashaka, muitikio ni mkubwa sana, naomba niendelee kuwaomba wananchi kuendelea kushiriki katika kutoa nguvukazi yao na kusimamia kuhakikisha kwamba kila shilingi ambayo inatolewa inaenda kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kufafanua hayo machache, naomba kipekee nimshukuru Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri wangu Mheshimiwa Selemani Jafo, Naibu Waziri mwenzangu Mheshimiwa George Kakunda kwa ushirikiano na maelekezo ambayo nimekuwa nikipata katika kazi yangu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee naomba nimshukuru Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu spika, Wenyeviti wote wa Kamati na Wabunge kwa ujumla kwa ushirikiano ambao kwa kweli hata siku moja sijapungukiwa. Hakika Mwenyezi Mungu atasimama pamoja na ninyi kwa sababu dhamira ya kuwatumikia Watanzania iko dhahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana.