Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuanza kutoa maelezo yangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge letu kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge na kuhitimisha hoja za Makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kwa mara nyingine tena kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa maelekezo yake yanayoniwezesha kutekeleza majukumu ya kusimamia menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora, eneo ambalo ni mtambuka katika utawala wa nchi na utendeshaji wa shughuli za Serikali. Napenda pia kuwashukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa maelekezo na ushauri wao ambao unatuwezesha kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukushukuru wewe binafsi pamoja na Mheshimiwa Spika, Wenyeviti wa Bunge, Katibu wa Bunge na uongozi wote wa Bunge kwa ushirikiano mkubwa mnaoipatia Ofisi yetu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani zangu ziwaendee viongozi na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa maoni na ushauri walioutoa ambao umesaidia katika utekelezaji wa majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo kwa awamu zilizotangulia, Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kutekeleza sera na mipango ya taifa kwa muda mrefu iliyobuniwa kuwaondolea wananchi umaskini na kuwaletea maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa sera, mikakati na mipango hii unahitajika watumishi wa umma wenye weledi, uadilifu, uchapakazi na umakini kwa kuwa utumishi wa umma ni nguzo muhimu katika maendeleo ya Taifa letu. Ikumbukwe kuwa kila taasisi ya umma imejengwa na watumishi wa umma, na bajeti zilizoombwa leo hapa zitakazopitishwa, wizara zote utekelezaji wake kwa kiwango kikubwa unategemea watumishi wa umma ambaye mimi ndio Waziri wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuendelea kuiboresha sekta ya utumishi wa umma, kuhimiza misingi ya weledi (professionalism), kuweka mifumo ya menejimenti inayowezesha watumishi kuwajibika na kuwa na maadili ili watoe huduma kwa wananchi na wadau wengine kwa kufanya kazi kwa ufanisi, bidii na kuzingatia matokeo na hivyo kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, utumishi wa umma lazima uongozwe na kusimamiwa ili kuhakikisha kuwa unaboreshwa kulingana na mahitaji ya wananchi bila kuathiri misingi yake. Ili kulinda misingi Serikali imekuwa ikifanya mabadiliko katika usimamizi wa utumishi wa umma mara kwa mara ili kuendana na misingi niliyoieleza hapo awali. Kama ilivyo kwa awamu zilizotangulia, Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuuboresha utumishi wa umma ili uendelee kuwa na manufaa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanza kwa Serikali ya Awamu ya Tano, hatua mahususi za kusimamia sera na mifumo ya menejimenti, matumizi ya teknolojia na habari na mawasiliano, nidhamu, mapambano dhidi ya rushwa, uadilifu na uwajibikaji imeendelea kuchukuliwa. Tunaamini kuwa kwa kuzingatia mambo haya watumishi wa umma watafanya kazi kwa weledi na bidii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia Wizara yangu; Wabunge 74 wamechangia hotuba yangu kwa kuzungumza hapa ndani ya ukumbi wa Bunge na Wabunge 17 walichangia kwa maandishi. Wabunge hawa wakiongozwa na Mheshimiwa Jasson Rweikiza, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa na Makamu wake Mheshimiwa Mwanne Mchemba wametoa michango na ushauri ambao tutauzingatia wakati wa kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyoona hii ni idadi kubwa ya Wabunge waliochangia, napenda kuwashukuru sana, muda ungetosha ningewataja mmoja mmoja, lakini kwa sababu ya muda naomba wanisamehe. Napenda kuwashukuru sana na kuwaahidi kuwa maelezo kwa kila hoja iliyotolewa yatapatikana kabla ya mkutano huu wa Bunge kumalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja katika Wizara yangu zilijikita katika maeneo mahusisi yafuatayo, yaani yale yaliyozungumza kama unataka kufanya majumuisho mengi yamegusia maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza upungufu wa watumishi hasa katika sekta ya afya na elimu ambayo imechangiwa na Wabunge 39, upandishwaji vyeo iliyozungumzwa na Wabunge wengi, watumishi kukaimu nafasi na madaraka kwa muda mrefu kama ilivyojitokeza kwenye maoni na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, umuhimu wa kuboresha maslahi ya watumishi ambapo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imelitolea maoni na ushauri. Aidha Wabunge wawili nao wamelizungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mapambano dhidi ya rushwa, masuala ya utawala bora ikiwemo wasiwasi na usalama wa wananchi wetu na shughuli za Idara ya Usalama wa Taifa, suala ambalo lilichangiwa na Wabunge 17 na leo nitalitolea ufafanuzi; vita dhidi ya umaskini kama lilivyojitokeza katika maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa na michango ya Wabunge waliochangia kuhusu shughuli za TASAF, MKURABITA na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majina ya Waheshimiwa Wabunge wote kama nilivyosema yaingie kwenye hansard kwa kumbukumbu sahihi za shughuli za bajeti za Wizara yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, masuala haya ni sehemu kubwa ya ajenda ya Serikali ya Awamu ya Tano kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2015/2020 na napenda kuchukua nafasi hii kuyazungumza kwa kifupi hasa kwa kuwa muda hautoshi kujibu hoja zote kama zilivyotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Nitajitahidi kujibu hoja kwa kadri muda utakavyoruhusu, na naomba nianze na suala la ajira katika utumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na rasilimali ya kutosha na yenye weledi katika kutekeleza majukumu yake kulingana na vipaumbele vyake. Hata hivyo, ajira katika utumishi wa umma hutegemea uwezo wa bajeti ya Serikali, pale bajeti inaporuhusu Serikali imekuwa ikitoa nafasi za ajira. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga nafasi za ajira 49,356 ikiwemo nafasi 16,000 za walimu wa shule za msingi na sekondari, nafasi 15,000 kada ya afya na kada nyingine za kilimo, uvuvi, mifugo, vyombo vya ulinzi, magereza, uhamiaji na nafasi 15,245 kwa ajili ya kada nyinginezo wakiwemo Watendaji wa Vijiji, Mitaa na Kata, Wahasibu, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, Maafisa Tarafa, Maafisa TEHAMA, Ugavi, Utawala na Utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili lililochangiwa na Wabunge wengi ni lile la upandishwaji vyeo. Kama ilivyo kwa ajira, upandishwaji vyeo na uteuzi hutegemea sifa za muundo na utendaji mzuri, bajeti ya kugharamia mishahara na kulinda tange kwa kada husika ili kuwepo uwiano wa utendaji wa wasimamizi mahali pa kazi. Kutokana na misingi hii katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga nafasi 162,221 za kuwapandisha vyeo watumishi wenye sifa stahiki katika kada mbalimbali. Katika nafasi hizi, nafasi 2,044 zimetengwa kwa ajili ya kujaza mapengo mbalimbali ya vyeo vya uteuzi katika ngazi ya madaraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, uteuzi huu katika nafasi ya madaraka utapunguza kero ya kukaimu nafasi hizo kwa muda mrefu kama ilivyobainishwa na Waheshimiwa Wabunge katika kuchangia hoja yangu. Kutokana na kutolewa fursa hii, natoa rai kwa mamlaka za ajira na mamlaka nyingine zinazohusika, kuhakikisha kuwa zinaanzisha michakato hiyo mapema na kwa kuzingatia vigezo vilivyobainishwa katika miongozo mbalimbali iliyotolewa inayohusu uteuzi wa watumishi kushika madaraka. Pale ambapo hakuna watumishi wanaokidhi vigezo hivyo, waajiri wasisite kuomba kuhamishiwa watumishi wenye sifa stahiki kutoka maeneo mengine katika utumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la nyongeza ya mishahara nalo limezungumzwa na wachangiaji wengi, suala hilo nalo ni la kibajeti na limeangaliwa kwa mapana yake.

Kutokana na umuhimu, Serikali inakusudia kutoa nyongeza ya mwaka kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine lililozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge ni kuhusiana na mapambano dhidi ta rushwa. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itaendelea kuimarisha vita dhidi ya rushwa. Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha uadilifu, kuhakikisha viongozi na watumishi wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viapo vya uadilifu na kuwajibika kwa matokeo ya kazi na maamuzi yao ili kuondokana na matumizi mabaya ya madaraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua hizi, Serikali itaendelea kuiwezesha TAKUKURU kutekeleza majukumu yake kwa kuwajengea uwezo watumishi wake, hasa katika maeneo ya uchunguzi, uendeshaji kesi za rushwa na ufisadi na kujenga ofisi hatua kwa hatua katika Wilaya mpya ambazo hazina ofisi za taasisi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maadili ya viongozi, Serikali itaendelea kujenga mifumo mbalimbali ya taratibu za kazi zinazoendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kuwa ndio msingi mkuu wa uboreshaji wa utawala bora. Tutaendelea kuimarisha mfumo wa kufuatilia tabia na mienendo ya viongozi wa umma kwa njia ya kisasa zaidi ili waweze kujiepusha na vitendo vizivyo vya kimaadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa viongozi wote kuwa mienendo bora ya uzalendo na hali ya juu kwa kuwa maendeleo yanatokana na mwelekeo bora wa viongozi. Viongozi wajenge tabia ya kujiuliza katika kila jambo kuwa wayafanyayo hayaleti mgongano wa maslahi?

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Wabunge waliochangia walionesha wasiwasi kuhusu usalama wetu na shughuli za Idara ya Usalama wa Taifa. Idara hii hutekeleza majukumu kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Taifa Namba 15 ya mwaka 1996. Kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha sheria hii, majukumu ya msingi yaliyoainishwa ni kukusanya taarifa, kuchambua na kuishauri Serikali ipasavyo juu ya hatua za kuchukua ikiwemo usimamizi wa rasilimali za nchi. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 5(a) Idara hii haihusiki na usimamizi wa sheria (law enforcement) kwa kuwa kwa mujibu wa mgawanyo wa majukumu, miongoni mwa vyombo vya ulinzi na usalama jukumu hili ni la mamlaka nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa naomba nichukue nafasi hii kufafanua Sheria ya Usalama wa Taifa inasema nini. Usipojua kazi za Idara ya Usalama wa Taifa utawapa lawama kwa shughuli ambazo si zao. Nataka kurejea sheria inasema nini, kifungu cha 5(1)(a), nataka kusoma kwa kiingereza halafu ntaeleza maana yake nini kwa kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa ya Usalama wa Taifa kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Bunge hili inasema hivi; “To obtain, correlate, and evaluate intelligence relevant to security, and to communicate any such intelligence to the Minister and to persons whom, and in the manner which, the Director-General considers it to be in the interests of security.”

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ndiyo kazi kubwa ya chombo cha usalama nchi yoyote ile; kukusanya habari na kuishauri Serikali iliyopo madarakani. Sasa yale mnayosema wanatukamata ovyo, wanafanya hivi, nataka niseme mafungu mengine mawili sheria inasema nini. Namba mbili inasema; “It shall not be a function of the Service,” haitakuwa shughuli ya Idara kufanya mambo yafuatayo, moja; “To enforce measures for security,” (haitatumia mabavu kumkamata mtu ili ku-enforce security), sheria ndivyo inavyosema. Pili, nilikuwa nawasikiliza muda wenu basin a mimi mnisikilize. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili inasema haitakuwa kazi ya Idara ya Usalama, kwa kiingereza; “to institute surveillance of any person or category of persons by reason only of his or their involvement in lawful protest, or dissent in respect of any matter affecting the Constitution, the laws or
the Government of Tanzania” (haitakuwa kazi ya Idara ya Usalama kufuatilia mhalifu, haitakuwa kazi ya Idara ya Usalama).

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niiseme hiyo kwa sababu mazungumzo mengi yaliyozungumzwa hapa yameelekezwa huko. Mtu ameuawa it is a police case, mtu amepotea it is a police case, hakuna nchi ambayo Idara ya Usalama inashughulika kukamata wahalifu. Inawezekana mnatumia hayo kujenga hoja zenu, lakini sheria ndivyo inavyosema. Kama mnataka wawe wanafanya hayo mnayoyataka leteni sheria hapa mbadilishe watafanya. Mimi mtumishi wa Bwana nitatenda kama Bwana anavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Idara hii hutekeleza majukumu kwa mujibu wa Sheria ya Usalama kama nilivyosema. Kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha sheria hii majukumu ya msingi yaliyoainishwa ni kukusanya taarifa, kuchambua na kuishauri Serikali ipasavyo juu ya hatua za kuchukua ikiwemo usimamizi na rasilimali za nchi. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 5(2)(a) Idara hii haihusiki na usimamizi wa sheria (law enforcement) kwa kuwa kwa mujibu wa mgawanyo wa majukumu miongoni mwa vyombo vya ulinzi na usalama jukumu hilo ni la mamlaka nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mgawanyo huu si sahihi kuihusisha Idara hii na matukio ya uhalifu yanayotokea kwa nyakati tofauti. Aidha, uhalifu kama huu hauikumbi Tanzania peke yake bali upo katika mataifa mengine na uchunguzi wake huchukua muda. Ipo mifano hai inayodhihirisha ugumu katika kubainisha wahalifu kwa kuwa wao hutumia mbinu mbalimbali. Waheshimiwa Wabunge watakumbuka jinsi Serikali ilivyokabiliana na uhalifu kama huo katika Wilaya ya Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuiunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya uhalifu wa aina yoyote na wajiepushe kutoa matamko yanayoweza kuchochea uvunjifu wa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ofisi yetu inazo programu mahususi zinazochangia jitihada za Serikali katika kupambana na umaskini. Programu hizi hutekelezwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Programu ya Kurasimisha Rasilimali za Wanyonge (MKURABITA) na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea. Serikali itaendelea kutekeleza programu hizi ili kupunguza kiwango cha umaskini nchini. Aidha, Serikali itaendelea kuhakikisha wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini ili kuhakikisha kuwa wanaonufaika ni wale tu wanaostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza maelezo hayo kwa utangulizi, ninaomba sasa kupitia hoja sitozipitia zote ambazo zimejitokeza katika mjadala wa Wizara yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wajumbe wamesema kuna ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa kutumia macho, vitendo vya mauaji, utekaji nyara, kupigwa watu na upendeleo mwingi. Hapa majibu tunasema Serikali haiungi mkono vitendo vyote vya ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na ndiyo maana kila vitendo hivi vinapojitokeza Serikali huchukua hatua mara moja kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika hivyo, Serikali inaomba wanasiasa na wananchi kwa ujumla kuunga mkono hatua za Serikali zinazochukuliwa katika Jeshi la Polisi lenye dhamana ya usalama wa raia. Jeshi lenye dhamana ya usalama wa raia ni Jeshi la Polisi, si Idara ya Usalama. Hata hivyo, ni jukumu la kila raia kutoa taarifa sahihi kwa Jeshi la Polisi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi na Katiba ya nchi, mfano kuzuia mikutano ya hadhara, kukosekana kwa uhuru wa mawazo, wanaokosoa Serikali au kuishauri wanapata misukosuko na wengine wanapoteza, watumishi wa kiroho kupata misukosuko baada ya kudai kuwepo kwa Katiba Mpya au Serikali kukosolewa kwa maslahi, magazeti kufungiwa na waandishi kutozwa faini kwa sababu ya kutoa taarifa zisizopendeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hapa napenda kujibu hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, si kweli kuwa Serikali inakiuka sheria ya nchi na Katiba katika kutekeleza majukumu yake. Mtu yeyote au taasisi inayoona inanyimwa haki ya kisheria na Kikatiba ina nafasi ya kupeleka malalamiko yake kwenye vyombo vinavyotoa haki ambayo ni mahakama. Aidha, pamoja na uhuru huo kuwepo, ufanyike kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu magazeti kufungiwa, hufanyika kwa mujibu wa sheria zilizopitishwa na Bunge. Tena Sheria ya Magazeti ilikuwepo ya mwaka 1976 tukailalamikia, Bunge hili limepitisha Sheria ya Magazeti, ndani ya Sheria ile ya Magazeti kuna chombo kinaitwa Content Committee ya senior citizens, kazi yao wao ni kufuatilia vyombo vya habari, yule ambaye amekwenda kinyume na maadili anaadhibiwa. Wale watu wameadhibiwa na Content Committee, Waziri anashauriwa na Content Committee, anapofunga Waziri anafungia kwa mujibu wa sheria na waliomshauri wamo ndani ya Sheria ya Vyombo vya Habari iliyopitishwa na Bunge hili linaloendelea leo hapa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la watumishi wa kiroho kupata misukosuko, Serikali haina ushahidi wa jambo hilo; na mimi nasema suala la watumishi wa kiroho ningependa sana nilichangie lakini sitaki kuchangia, ila niseme tu kifupi; ukitaka kumshauri mzee wako huitishi mkutano wa hadhara ukasema ninamshauri baba, hakuna njia ya kumfikia huyo baba yako kimya kimya? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la watumishi wa kiroho kupata misukosuko, Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa uhalifu wowote bila kujali umefanywa na nani.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine lililozungumzwa sana, ni sheria ipi inayowapa mamlaka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwaweka watu ndani saa 24 na ni hatua zipi zimechukuliwa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya inapobainika kwamba wananchi wamewekwa ndani kimakosa na hili nataka nilieleze.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wamepewa mamlaka ya kisheria, Regional Administration Act ya mwaka 1997 (Sheria ya Tawala za Mikoa mwaka 1997) imewapa madaraka kumuweka mtu yeyote ndani anayebainika kutenda kosa lolote lenye kuhatarisha amani na utulivu wa jamii husika. Anayeona hakutendewa haki, kwamba hakuwekwa kwa misingi hiyo ana ruhusa ya kulalamika kwa wakubwa wake wa kazi, hakuridhika, ruhusa kwenda mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwa kuwa Mkoa wa Kigoma umekuwa ukitoa malalamiko yake kwa Serikali na yamekuwa yanapuuzwa, hususani kupotea kwa Diwani na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo bila maelezo yoyote, wananchi watajichukulia hatua na kufanya wanavyoona inafaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nadhani ndugu yangu Mheshimiwa Zitto pale ulikuwa unatuhimiza tu kwamba jambo hili tulifanyie kazi, lakini ninavyomuelewa Mheshimiwa Zitto alivyo msomi, kijana, anaipenda nchi, ana akili, simuoni Mheshimiwa Zitto anahamasisha watu kuchukua sheria mkononi, yale maeneo aliyaweka tu kutuhimiza watu wa Serikali kwamba please take action. Point noted, tumeipokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo yake, majibu yake; Serikali haipuuzi malalamiko ya upotevu wa watu nchini ikiwemo Diwani na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo kama anavyodai Mheshimiwa Mbunge. Suala la kupotea kwa Diwani huyo lilisharipotiwa katika Jeshi la Polisi na uchunguzi unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, na tena hapa mimi nataka nimpongeze ndugu yangu Mheshimiwa Zitto, huyu Diwani anayemtetea tumtafute mpaka tumpate, wala sio wa chama chake ACT, ni Diwani wa CCM, inaonesha jinsi alivyo mzalendo anavyopenda haki itendeke kwa kila mtu, sasa uendelee hivyo hivyo mdogo wangu Mheshimiwa Zitto, usiyumbe katika mengine, endelea hivyo hivyo. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasisitiza mwananchi mwenye taarifa kuhusu jambo hili ajitokeze kusaidia polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. Kama nilivyosema mwanzo, this is another police case, kesi nyingine ya polisi, si ya vyombo, kesi nyingine ya polisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Selasini; kuna mwandishi wa habari aitwaye Cyprian Musiba amekuwa akitoa matamko hatarishi katika vyombo vya habari yakiwemo na magazeti anayoyafanyia kazi lakini Serikali ikiwemo na Idara ya Usalama wa Taifa imekaa kimya na haijatoa tamko lolote la kubeza, hivyo wananchi waelewe vipi kama matishio hayo yana kibali cha Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Selani, nataka nikueleze kuwa sheria iliyotungwa na Bunge hili inataka Idara ya Usalama wa Taifa ifanye kazi zake kwa faragha. Kwa hiyo, hii hoja uliyoitoa kwamba hata Idara ya Usalama wa Taifa imekaa kimya, nilishawahi kueleza humu ndani siku moja, hautawahi kusikia hata siku moja taarifa imetolewa na Msemaji wa Idara ya Usalama wa Taifa. Kwa hiyo, suala la wao kuwaita watu na kusema jamani sisi tumeishauri Serikali hivi, huyu bwana tumemchukulia hatua hii, si kazi yao, kazi yao ni kukusanya habari, kuishauri Serikali, wamemaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa mujibu wa sheria ya nchi Jeshi la Polisi ndilo linalopewa dhamana ya kufanyia uchunguzi matamko yote yenye kuhatarisha usalama wa raia na ambayo ni makosa ya jinai na pale inapojiridhisha huwapeleka wahusika mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Idara ya Usalama wa Taifa kukaa kimya ni utekelezaji wa sheria, kama nilivyosema, wanafanya kazi yao kwa faragha. Hujawahi kuwasikia na hutawasikia wanaita press conference. Hata hivyo, mtu yeyote ambaye ataona ameathiriwa na matamko hayo ana haki ya kuyapeleka malalamiko yake kwa Jeshi la Polisi ili hatua zaidi ya uchunguzi wa kisheria iweze kuchukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Almas Athuman Maige; Idara ya Usalama wa Taifa itoe semina kwa Waheshimiwa Wabunge ili waweze kupata uelewa juu ya kazi na shughuli za Usalama wa Taifa. Mimi nakushukuru sana ndugu yangu Mheshimiwa Maige, kama nilivyoeleza tangu mwanzo, ukifuatilia maelezo yangu juu ya Idara hii utaona kwamba tunawauliza maswali inawezekana wakati mwingine kwa kutokufahamu na mimi tangu nimeingia katika Wizara nilipoliona hivyo, ombi limepokelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali ilishapeleka maombi Ofisi ya Spika kuhusu kufanyika kwa semina hiyo katika kipindi hiki cha Bunge linaloendelea ili tuelewane wao wanafanya nini. Mpate muda wa kuuliza maswali, mjiridhishe ili tuendelee kuwahoji yale yanayowahusu, yale yasiyowahusu tushughulike na wanaohusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, utawala bora safari hii ilikuwa ni Idara ya Usalama tu; utendaji kazi wa Idara ya Usalama wa Taifa hauridhishi, je, inacho Kitengo cha Economic Intelligence ambacho kingeweza kutoa ushauri kwa Serikali juu ya masuala mbalimbali ya kiuchumi yakiwemo ya usimamiaji wa miradi na mikataba ya uwekezaji? Ameuliza ndugu yangu Mheshimiwa Ngwali hapa, ametoka, basi lakini atasikia. Mheshimiwa Ngwali alikuwa Mjumbe machachari kwenye Kamati yangu, safari hii sijui amehama, sijamuona, na anatuhamasisha watu wa Serikali kufanya mambo mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, muundo wa Idara ya Usalama unatokana na majukumu yaliyobainishwa katika Sheria Namba 15 ya mwaka 1996 inayounda taasisi hiyo. Moja, anasema Usalama wa Taifa


hauridhishi; nataka nimhakikishie ndugu yangu Mheshimiwa Ngwali, nchi hii iko salama, jahazi linakwenda, limeshikwa na nahodha madhubuti, kazi yake yeye ajishikilie tu mawimbi yakija asije akaanguka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kama nilivyosema, shughuli zao hufanyika kwa faragha. Sasa muasisi wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Mao Tse-Tung alisema hivi; “no research, no right to speak”. Jambo ambalo hujalifanyia utafiti, huna uhakika nalo usiliseme. Ndugu yangu Mheshimiwa Ngwali una uhakika gani kwamba hayo unayoyasema kwenye idara hayapo? Umeshawahi kuingia kule? Lakini kwa sababu shughuli zao wanafanya kwa faragha siwezi nikakujibu kwamba kitengo wanacho au hawana kwa sababu mila na desturi ya chombo cha usalama ni kufanya kazi kwa faragha. Lakini jibu la uhakika tu nililokupa ni hilo moja kwamba nchi iko salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi kwa TAKUKURU na Usalama wa Taifa, ndugu yangu Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa, nakushukuru. TAKUKURU na Usalama wa Taifa waendelee kutumia utaalam na weledi kuishauri Serikali katika kukusanya mapato na matumizi ya fedha za umma; ushauri umepokelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine miradi ya maji Handeni Vijijini ina ubadhirifu wa rushwa. Tumeeleza hivi; Serikali imedhamiria kutokomeza rushwa nchi hii, kuondoa umaskini na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, TAKUKURU imekuwa ikifuatilia miradi ya maendeleo na nataka nikuhakikishe mpwa wangu, Mheshimiwa Mboni Mohamed Mhita, kwamba jambo ulilolitaja TAKUKURU ina taarifa nalo, inalifanyia kazi muda mwafaka ukifika tutachukua hatua. Tukiwaona kwamba baada ya utafiti hawana hatia tutawaacha, tukiona wana hatia hatua zitachukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, TAKUKURU wawezeshwe kuwa na ofisi nzuri na vitendea kazi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi. Ndugu yangu Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, nakushukuru kwa kututetea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ofisi za Serikali ziwe na ushirikiano na TAKUKURU ili kuepuka matumizi mabaya ya fedha za umma. Maelezo yake ni kuwa Serikali itaendelea kuiwezesha TAKUKURU kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kuwapatia vitendea kazi na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kadri bajeti ya Serikali itakavyoruhusu. Hata hivyo, kwa mwaka huu wa fedha Serikali imepanga kujenga ofisi saba za Wilaya na mwaka 2018/2019 zitajengwa ofisi kumi. Kwa hiyo, ninaomba tu Waheshimiwa Wabunge na ndugu yangu Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia na Mheshimiwa Emmanuel Papian basi mtuunge mkono, mpitishe bajeti hii ili ofisi zijengwe kama mnavyokusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine inasema Serikali iandae utaratibu wa kuingiza somo la maadili katika mitaala ya elimu ya msingi na sekondari ili kujenga kizazi chenye maadili na uzalendo ambacho kitaelewa, kitachukia na kupinga vitendo vya rushwa. Nataka nishukuru kwa ushauri huo. Somo la maadili limeingizwa katika mitaala ya elimu ya msingi na masomo yanayofundishwa ni uraia na maadili. Kwa upande wa shule za sekondari somo la maadili linajitokeza katika masomo ya general studies na civics (uraia).

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mchakato wa kuanzisha mitaala ya somo la rushwa kwenye shule za sekondari unaendelea. Vilevile katika kuimarisha elimu ya maadili shuleni na vyuoni kumefunguliwa na vilabu vya maadili katika shule na vyuo mbalimbali. Ushauri tumeupokea, tunaufanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine, Sekretarieti ya Maadili inapowataka viongozi kuwasilisha fomu waeleze pia nyaraka nyingine zote zinazotakiwa kuwasilishwa ili ziwasilishwe kwa pamoja. Hoja tumeipokea hitaji la nyaraka na mali za madeni ya viongozi wa umma hujitokeza pale sekretarieti inapotaka kufanya uhakiki wa matamshi ya rasilimali na madeni ya viongozi wa umma baada ya kupokea fomu hizo ili kuthibitisha ukweli wa tamko lililotolewa na kiongozi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Zoezi la kutambua na kuandikisha kaya maskini katika maeneo ambayo hayakufikiwa katika awamu ya kwanza na mradi wa ruzuku kwa kaya maskini ifanyike mapema ili kaya maskini katika maeneno hayo yanufaike na mpango wa ruzuku. Takwimu zinaonesha yapo maeneno ya vijiji 4,408; mitaa 1,189; shehia 96 ambayo haijafikiawa katika awamu ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo ni kuwa utaratibu wa kufikia vijiji vyote ambavyo havijafikia umeandaliwa katika sehemu ya pili ya mpango wa kunusuru kaya maskini tunaotarajia kuanza mwaka 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwamba Serikali ianze maandalizi ya kuwezeza mpango wa ruzuku kwa kaya masikini kuwa endelevu; ushauri umetoka kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala ushauri umepokelewa. Hata hivyo TASAF inakitengo maalumu cha kukuza uchumi wa kaya ambacho kinaandaa kaya na walengwa kutoka kwenye mpango wakiwa tayari na stadi na kuendelea na maisha yao pale mpango ukapokwisha au watakapohitimu kwenye mpango ili kuwapisha wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni kwamba Halmashauri zitumie maofisa maendeleo ya mamii ili kuelimisha wanufaika wa mpango wa ruzuku wa kaya maskini namna wanavyoweza kutumia sehemu ya ruzuku hiyo kujikwamua.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika baadhi ya maeneo walengwa wamenufaika kwa kuanzisha kilimo na ufugaji wa kutumia sehemu ya ruzuku. Maelezo ya Serikali ushauri tumeupokea, kwa kiasi kikubwa mpango wa kunusuru kaya maskini unafanya kazi na Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao wengi wao ni waratibu wa mpango katika ngazi za Halmashauri. Serikali itahakikisha kuwa katika maeneo ambayo bado hayaajanza kuwatumia watumishi hao wawashirikishe katika shughuli za mpango.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni kwamba Serikali iwafuatatilie kwa karibu viongozi wanasiasa katika vitongoji, vijiji na kata kwani yako malamiko ya baadhi ya wananchi kuwa baadhi ya viongozi wanasiasa wanatambua na wahitaji kwa upendeleo bila kuzingatia vigezo. Maelezo ya Serikali, utambuzi wa kaya maskini katika maeneo yaliyoko kwenye mpango hufanywa na wananchi katika mikutano ya hadhara ambayo inasimamiwa na viongozi wa vijiji, miji na Halmashauri. Hata hivyo yanapotokea malalamiko uhakiki hufanyika na kuwaondoa wasiokuwa na vigezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hao wanaonufaika sasa na mpango wa TASAF, tulipoanza utekelezaji baadhi ya maeneo wananchi walilalamika, tukatumia vyombo vya Serikali katika ngazi zinazohusika na walipothitisha kwamba ni kweli wameongopa wametolewa katika mpango wa TASAF. Vilevile watumishi wa Serikali waliokuwa wamewasajili watu ambao wanajua hawakuwa na sifa ya kusajiliwa na wao wamechukuliwa hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba Serikali iongoze bajeti ya MKURABITA na kutoa kikamilifu na kwa wakati ili kuongeza kasi ya upimaji na urasimishaji wa ardhi na biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Serikali ni kuwa Serikali imeendelea kuona umuhimu wa shughuli za MKURABITA na kuendela kutenga fedha katika bajeti kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga bilioni 4.3 ambapo hadi kufikia jumla ya shilingi bilioni 2.4 sawa na asilimia 57 zimepokelewa na kutumika. Aidha, mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga shilingi bilioni 4.4 kwa ajili ya shughuli za MKURABITA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutoa fedha kama zinavyotengwa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine; katika utekelezaji wa shughuli za MKURABITA ambao umewanufaisha wengi wakiwemo wananwake bado vijana hawajanufaika kwa kiwango cha kuridhisha na mpango huu. Serikali ifanye utaraibu utakaowezesha vijana wengi kunufaika. Maelezo ya Serikali katika mwaka wa fedha 2018/2019 MKURABITA imejipanga kutumia fedha ya kituo kimoja cha urasimishaji kuwawezesha vijana kuwa wabunifu kuchangia katika upatikanaji wa ajira na hivyo kuwa wameshiriki katika kujenga uchumi wa Taifa. Aidha, jumla ya vituo vitano vya usafirisahji biashara vitaanzishwa Tanzania Bara na viwili Tanzania Zanzibar, vituo hivyo tumevitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine, benki na taasisi za fedha zikielimishwa kuhusu ardhi na hati ya haki miliki za kimila kutumika kama dhamana ya mkopo zitatoa mikopo kwa wananchi wanaomiliki ardhi kwa hati hizo. Maelezo ni kuwa kwa sasa benki na taasisi nyingine za fedha zinakubali hati miliki za kimila tutumika kama dhamana ya mkopo na pale itakapotokezea kwamba kuna benki inakataa Waziri wa Nchi anayeshughulika na masuala ya Utumishi na Utawala Bora nikiletewa habari nitafanyia kazi.

Mhehsimiwa Naibu Spika, Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa inasema Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) uwezeshwe kifedha kutanua wigo wa shughuli zake nchini na hivyo kuwafikia wanawake na vijana. Majibu ya Serikali ni kuwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imeongeza bajeti ya maendeleo ya Mfuko wa Rais wa Kujitegemea kutoka shilingi milioni 500 mwaka 2017/2018 hadi shilingi bilioni 1.7 mwaka wa fedha 2018/2019 ili kutatua wigo wa kuwafikia wanawake na vijana wengi zaidi. Aidha, Serikali itaendelea kuuwezesha mfuko huu kulingana na uwezo na itaendelea kushirikiana na mamlaka ya Seriakli za Mitaa na wao waendelee kutoa mikopo kwa walengwa waliopo katika eneo lao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine inasema Serikali kupitia Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) itoe mafunzo ya uongozi na utawala kwa viongozi walioteuliwa ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria kanuni na miongozo ya kiutendaji, na hivyo kuepusha migogoro isiyo na lazima ambayo inaweza kuibuka. Hii imetoka kwenye Kamati ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa. Majibu ya Serikali ni kuwa Serikali kupitia taasisi mbalimali ikiwemo Uongozi Institute ina jukumu la kutoa mafunzo ya uongozi na utawala bora kwa viongozi wanaoteuliwa ikiwa ni pamoja na viongozi wa Mikoa, Wilaya, Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria kanuni na miongozo ya kiutendaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miezi nane iliyopita mafunzo yaliyohusisha mahusiano ya kiutendaji kati ya viongozi wa siasa na watendaji, utawala bora na uwajibikaji maadili na kujenga sifa binafsi za kiuongozi yalitolewa kwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kupitia Taasisi ya Uongozi. Aidha, taasisi imeandaa mafunzo ya aina hiyo kwa ajili ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa. Serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa viongozi wanaoteuliwa pale inapohitajika kwa lengo la kuimarisha uhusiaono wa kiutendaji wa kuboresha huduma za jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni ile inayohusu kwamba Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kiwezeshwe kukamilisha awamu ya mwisho ujenzi wa jengo ambalo linaendelea katika campus ya Tabora. Maelezo ya Serikali ni kuwa Kamati inatambua umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa jengo lililopo katika campus ya Tabora, ujenzi huu unatekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani ya chuo. Aidha, katika mwaka wa fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kimetengwa, shilingi milioni 800 kwa mwaka wa fedha zimetengwa kwa ajili ya mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niihakikishie Kamati inayonilea hapa Bungeni ya Katiba na Utawala kwamba mimi Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii nitasimamia na kuhakikisha kuwa jengo lile linakamilika ili Tabora Secretarial College ambayo ndiyo Secretarial College ya kwanza ya Serikali katika nchi hii kuirudishia hadhi yake. Ndiyo maana hata katika mafunzo ya degree ya ma-secretary tumeanza Dar es Salaam, lakini tunafanya maandalizi Tabora ili Tabora Secretarial College itoe degree ya u-secretary kwa sababu ndicho chuo cha mwanzo cha ma-secretary cha Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine Serikali iangalie uwezekano wa kuridhia Mamlaka za Serikali za Mitaa kuajiri bila kibali na kuziachia kuendesha mchakato wa ajira kwa watumishi wa kada za afya. Maelezo ya Serikali ni kuwa kuajiri watumishi baada ya kupata kibali na matakwa ya Sheria ya Utumisha wa Umma Namba Nane ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake. Aidha, Bunge katika Sheria ya Mabadiliko Sheria Mbalimbali (Written Laws Miscellaneous Amendment Namba Mbili ya mwaka 2013 iliifanyia marekebisho Sheria ya Utumishi wa Umma Namba Nane ya mwaka 2002. Katika mabadiliko hayo Katibu Sekretarieti ya Ajira amepewa mamlaka ya kukasimu uendeshaji wa mchakato wa ajira kwa waajiri katika tangazo la Serikali la mwaka 2014 ambapo Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekasimiwa kuendesha mchakato wa ajira wa kada za chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachosema kwamba ombi hili limepokelewa na Serikali, Halmashauri zimekasimiwa kufanya huo mchakato wa mahojiano mpaka ajira, lakini kila inavyotokea hivyo, kwa sababu kule Wilayani tunafahamiana huyo mtoto wa mjomba, huyu mtoto wa fulani, Sekretarieti ya Ajira inatuma wawakilishi katika mchakato huo ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka. Kwa sababu haki isipotendeka lawama si Halmashauri lawama ni ya Waziri mwenye dhamana ya Utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine imelezwa kwamba kuna upungufu mkubwa wa watumshi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hususani kada ya walimu wa shule za msingi, walimu wa masomo ya sayansi, hisabati, watumishi wa kada ya afya, watendaji wa vijiji, watendaji wa mitaa watendaji wa kata, maafisa ugani wa kilimo na mifugo na watumishi wa kada nyinginezo. Majibu ya Serikali ni kuwa katika kila mwaka wa fedha Serikali imekuwa ikitenga nafasi za ajira mpya kulingana na mahitaji yake pamoja na vipaumbele vyake hususani katuka maeno ya elimu kilimo, afya, mifugo na uvuvi kutokana uwezo wa kibajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia Machi, 2018 Serikali imeajiri watumishi zaidi ya 18,000 ili kukabiliana na upungufu wa watumishi katika sekta za kipaumbele na zenye upungufu mkubwa kwa watumishi. Aidha, Serikali imepanga kuajiri watumishi 52,436 katika mwaka wa fedha 2017/2018 wengi wao wakiwa wa idara ya elimu afya na serikali za mitaa. Hawa tunaowaajiri mlishapitisha katika bajeti iliyopita, ni tofauti na wale 49,000 tunaotaka kuwaajiri katika bajeti inayokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo katika mwaka wa fedha 2018 Serikali imetenga nafasi ya ajira jumla 49,536 na hapa Waheshimiwa Wabunge kwa faida ya Bunge letu na faida ya wananchi wapate kufahamu; ni kwamba zoezi la ajira lilisimama wakati umeanza mchako wa kuhakiki vyeti. Ilionekana si busara unampandisha mtu leo halafu kesho unaambiwa cheti fake unaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi lile la kutambua vyeti fake limekamilika ndiyo maana Serikali ikaanza kuwaajiri watu mbadala wale waliondolea zoezi hilo nalo sasa karibu limekamilika tutaendelea na ajira mpya kama nilivyosema, 52,000 wa mwaka jana 2017 na mwaka ujao Serikali imejipanga kuwaajiri 49,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ya msingi sana, kwamba Serikali ifungue milango ya uhamisho kwa watuishi ambao wanahitaji kuungana na familia pale mwenza mmoja anahamishwa ili kuondoa usumbufu wa familia. Aidha, kumekuwa na usumbufu mkubwa wa mtumishi anapotaka kuhama na kuambiwa atafute mtu wa kubadilishana naye, na kwamba asipopatikana huyo mtumishi anakosa haki ya kuhama. Je, huo ni wajibu wa mtumishi au Serikali kutafuta jinsi ya kujua ni wapi mtumishi huyo atapangwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo ya Serikali ni kama ifuatavyo; Serikali haijafunga milango ya watumishi wale wanaotaka kuhama ili kuungana na familia zao au kwa sababu nyingine zozote zile za msingi. Aidha, maelekezo yametolewa kwa waajiri kupitisha maombi ya watumishi yaliyowasilishwa kwao ili mradi yamezingatia taratibu zilizopo kwa kuwa si sera ya Serikali kuzuia uhamisho wa watumishi katika utumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu naomba nitoa maagizo haya kwa mamlaka zote za Serikali za ajira katika nchi hii. Malalamiko makubwa waliyonayo watumishi wa umma ni kwamba wakiomba kuhama anapotakiwa kupitisha barua kwa mkubwa wake wa kazi wanawakatalia! Wanawakatalia! Sasa naomba kulieleza Bunge hili tukufu, mwenye mamlaka ya kumkatalia uhamisho ni yule anayeandikiwa barua, wewe uliyeandikiwa pale kupitia kwa, kiswahili sanifu kabisa kupitia kwa, wakishasema kupitia kwa wewe si mwamuzi wa mwisho, ndiyo maana inaandikwa kupitia kwa, peleka barua kwa mwajiri ili mwajiri apate kuamua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natembelea mikoani nimekwenda mkoa mmoja naambiwa hii ofisi yetu haijapitisha barua ya mtu kuhama hata siku moja.

Mimi ninasema, mimi ndiye Waziri wa Utumishi wa Umma, nikibaini kuna kiongozi wa utumishi anakataa kupitisha barua isinifikie mimi isimfikie Katibu Mkuu Kilimo, isimfikie Waziri Mkuu nitamshughulikia kwa mujibu wa sheria na taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitafanya hivyo kwa sababu mtu huyo amejichukulia madaraka yasiyo yake, hukuandikiwa wewe barua umeandikwa kupitia kwa, sasa kupitia kwa wewe ndiyo unaamua? Sasa mimi niliye juu hapa nitafanya kazi gani kama wewe unaniamulia?

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja imetolewa hapa na Mheshimiwa Ahmed Juma Ngwali, sasa rafiki yangu mwenyewe yuko wapi, amenikimbia? Anasema Serikali ilete muswada wa sheria wa kuibadili eGA kuwa mamlaka ili kuwa na nguvu za kisheria kusimamia na kudhibiti utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, majibu kuhusu Serikali Mtandao na je, Wakala wa eGA umetengewa kiasi gani kukabiliana na teknolojia inavyobadilika? Swali zuri na ushauri umepokewa ndugu yangu Mheshimiwa Ngwali, mchakato wa kutunga sheria ya kuibadili Wakala wa Serikali Mtandao kuwa mamlaka tayari umeanza Serikalini, na hapa mimi nataka niishukuru Kamati yangu ya Utawala na Serikali za Mitaa, wao wamejenga hii hoja ndani ya Kamati wamenishauri mimi Waziri ninayehusika tuanze mchakato wa kuibadili kuwa mamlaka ya Serikali mtandao.

Mheshimiaw Naibu Spika, kazi hiyo imeshaanza mimi natekeleza kama nilivyoagizwa na Kamati yangu; mimi mtumishi wa Bwana, nitatenda kama Bwana anavyotaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 Fungu 22 Wakala wa Serikali Mtandao imetengewa kiasi cha fedha shilingi bilioni nne kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Fedha hizi pamoja na mambo mengine zitaanzishwa kituo cha utafiti, ubunifu wa maendeleo ya Serikali Mtandao Makao Makuu Dodoma ili kukabiliana mabadiliko ya kiteknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho katika hoja ambazo naomba kuzisemea leo, kwamba Serikali iwezeshe kikamilifu Idara Kumbukumbu ya Nyaraka za Taifa kwa ajili ya kufanya tafiti, kukusanya na kuhifadhi taarifa na kumbukumbu muhimu katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Miongoni mwa njia ya kukusanya taarifa hizo ni kutembelea na kuhoji watu wenye umri mkubwa ambao wameshuhudia mambo mengi ambayo ni muhimu kwa taifa na vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo ya Serikali ni kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kukusanya na kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka ili kuhifadhi urithi andishi kwa ajili vizazi vya sasa na vizazi vya maendeleo ya Taifa letu. Katika kutekeleza jukumu hili Serikali imekuwa ikitenga fedha kupitia bajeti ya kila mwaka kulingana na uwezo wa kifedha kwa lengo la kuiwezesha idara kutekeleza majukumu yake. Kutokana na fedha hizo idara imekuwa ikitekeleza kazi mbalimbali ikiwemo kufanya tafiti kutambua, kukusanya na kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka zenye umuhimu kutoka taasis za umma katika sekta mbalimbali na za watu binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni katika maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasemea. Taratibu na mila za Bunge zinataka niyasome majina ya watoa hoja nilikuwa na mashaka ya muda, ukiruhusu nitawasoma waliotoa hoja, usiporuhusu nitawaweka wataingia katika kitabu chetu cha kumbukumbu ya Hansard…

NAIBU SPIKA: Waweke waingie kwenye kumbukumbu kwa sababu kanuni zetu haziruhusu kutaja majina, usiwaite kwa sababu kanuni zetu haziruhusu waingine kwenye Hansard.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelekezo, wote mliotoa hoja hizi majina yenu tutayaingiza kwenye Hansard.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge kama mtakavyoona tumejitahidi kuangalia maeneo yapi Wabunge walitaka maelezo, maeneo yapi lazima yafanyiwe kazi. Mimi nataka niseme kwa naiba ya Serikali nataka niwashukuru Wabuge wote kwa michango yenu.

Mimi Waziri hii ndiyo bajeti yangu ya kwanza, lazima niseme nimenufaika sana na michango mliyotoa Wabunge imetuwezesha, mmetuboresha, mmetuweka kuwa imara ili utendaji wa kazi ndani ya Serikali ya Tano uweze kuwa na ufanisi zaidi.

Sasa naomba kuhitimisha maelezo yangu kwa kuomba Waheshimiwa Wabunge kuunga mkono hoja hii ili kuiwezesha ofisi yangu kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na taasisi zake kwa ufanisi katika mwaka ujao wa 2018/2019. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.