Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafsi hii ili niweze kuchangia katika Wizara ya Katiba na Sheria. Katika kuchangia Wizara hii ya Katiba na Sheria, naomba kuchangia kuhusiana na masuala ya utoaji haki kwenye Mabaraza ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi yalianzishwa kwa sheria ya mwaka 2002 Sura ya 114, lakini Mabaraza haya ya Ardhi yalianzishwa ili kuweza kusaidia kutatua migogoro mingi ambayo inajitokeza katika umiliki wa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza haya yamekuwa yakikumbwa na changamoto mbalimbali. Changamoto mojawapo ni kwamba Wenyeviti wa Mabaraza haya ya Ardhi hawana uelewa wa kutosha kwa upande wa kisheria na hivyo kushindwa kuitatua vizuri migogoro ya ardhi na kusababisha wananchi kukosa haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia changamoto nyingine katika Mabaraza haya ya Ardhi ni kutokana na posho ambayo wanalipwa kwamba ni ndogo sana na wakati mwingine posho ambayo wanalipwa Wenyeviti hawa wa Mabaraza ya Ardhi inacheleweshwa. Kwa hiyo, inasababisha Wajumbe hawa wa Mabaraza ya Ardhi kukosa ari ya kufanya kazi vizuri na hivyo kusababisha kushindwa kutatua migogogro ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali kwamba ilete mabadiliko ya kisheria ili kuweza kufanya mabaraza haya ya ardhi kutokufanya kazi zake kwa sababu wameshindwa kufanya kazi zao katika kutatua migogoro ya ardhi. Kwa sababu hapo kabla, migogoro ya ardhi ilikuwa inatatuliwa katika mfumo wa kimahakama. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali iweze kufanya marekebisho ya sheria ili kurudisha kesi hizi za migogoro ya ardhi kufanyika katika mfumo wa kimahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu katika Mahakama, mawakili wetu hawa wanao uwezo mkubwa wa kisheria kuweza kutatua migogoro ya ardhi. Pia mawakili wanakuwa na maadili kiasi kwamba wana uwezo wa kutatua migogoro ya ardhi na hivyo kupunguza kabisa migogoro ya ardhi au kuimaliza kabisa katika nchi yetu ya Tanzania ambayo inaongoza pia katika Bara la Afrika katika akuwepo kwa migogoro ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la kesi la mirathi pamoja na kesi za ndoa. Wanawake wengi ndio wamekuwa waathirika katika kesi za mirathi pamoja na kesi za ndoa. Naishauri Serikali itusaidie kuleta sheria ya kuwa na Mahakama Maalum ambayo inaweza ikasikiliza kesi za mirathi pamoja na kesi za ndoa. Kwa sababu kutokana na jamii yetu sijui kubadilika au kupata uelewa mkubwa zaidi, sijui inakuwaje, migogoro ya mirathi na ndoa imekuwa ni mingi sana, imekuwa ikilundikana katika mahakama zetu. Tunafahamu kabisa tuna upungufu wa watumishi katika mahakama zetu na hivyo kufanya kesi kuludikana na kushindwa kufanyika vizuri. Kwa hiyo, naishauri Serikali kuleta sheria ili paweze kuanzishwa Mahakama Maalum ambayo itakuwa inasimamia kesi za mirathi pamoja na kesi za ndoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea suala la Uandishi wa Sheria kama inavyoonekana katika Kitabu cha Wizara ya Katiba na Sheria. Kwa muda wa miaka miwili na nusu nimekuwa ni Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo.

Katika uchambuzi wa sheria ndogo tumekuwa tukiona makosa mbalimbali yamekuwa yakifanyika katika uandishi wa sheria ndogo. Makosa hayo yalikuwa ni makosa ya kiuandishi na makosa ya kikatiba. Cha kushangaza sana, tunao watendaji ambao ni wanasheria katika Halmashauri zetu ambao wanaziandika hizi sheria lakini bado makosa yamekuwa yakipatikana kwa takribani asilimia 60 katika sheria hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, hiyo inasababisha watu kunyimwa haki zao. Kwa sababu unakuta kabisa kama sheria inakiuka Katiba, moja kwa moja mtu atakuja kukosa haki yake. Hivyo basi, ninashauri pawepo na semina mbalimbali. Pamoja na kwamba Serikali inafanya jitihada mbalimbali, lakini naomba semina ziweze kufanyika katika Halmashauri zetu kwa wale wanasheria ili wafahamu namna ya uandishi mzuri wa kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ipewe uwezo, watumishi waongezwe na pia watumie teknolojia mpya katika uandishi wa kisheria ili kuepuka makosa mbalimbali ambayo yanatokea hususan katika uandishi wa sheria ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nijielekeze katika suala la kuomba mabadiliko ya sheria mbalimbali. Katika Bunge hili Waheshimiwa Wabunge, na mimi nikiwepo wa kwanza tumekuwa tukiomba mabadilko ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na Serikali imekuwa ikitoa ahadi mbalimbali, kuna siku nilisimama hapa tarehe 5 Mei,2016 nikiitaka Serikali kuleta mabadiliko ya Sheria ya Ndoa na Serikali ilitoa ahadi kwamba mwezi Septemba katika mwaka huo 2016 wataleta Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Ndoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza sana, Serikali mpaka sasa imekaa kimya, ukiuliza kuhusiana na suala la sheria, wanaanza kusema mabadiliko ya Sheria ya Ndoa Serikali haina majibu sahihi, lakini hiyo ilIkuwa ni ahadi ya Serikali. Hivi tunataka kusema kwamba wananchi wasiiamini tena Serikali yao kwa sababu inatoa ahadi za uongo? Naomba tusifike huko, wananchi bado wanayo imani na Serikali. Kwa hiyo, ninaitaka Serikali kutimiza ahadi yake ya kuleta Muswada wa Mabadiliko ya Sheria hii ya Ndoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoitaka Serikali, kuna sababu mbalimbali. Serikali baada ya kusema kwamba italeta huo Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ya Ndoa, hawakuleta. Matokeo yake, wanamitandao wametumia upenyo huu au wametumia mwanya huo kwenda kuishtaki Serikali mahakamani na hatimaye Serikali wakashindwa katika kesi hiyo. Mahakama ikatoa ruling kwamba kifungu cha 13 na 17 viondolewe kwa sababu vinaleta ubaguzi katika Sheria hii ya Ndoa. Serikali ikakata rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kukata rufaa, mimi sitaki kuingilia muhimili wa Mahakama, mimi niko katika muhimili mwingine kabisa wa Kibunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabisa Serikali sasa iangalia na ione kwamba umefika muda muafaka, Watanzania wote wanataka Sheria ya Ndoa iweze kufanyiwa marekebisho kwa sababu watoto wetu wanateseka sana. Ukiangalia sheria hiyo, inaenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 12 (1) ambayo inasema: “Binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa.” Vilevile
(2) inasema, “Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa.” Mtoto huyu wa kike naye anastahili kutambuliwa na kuheshimiwa na kupewa uhuru wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la usawa katika utaungwaji wa sheria, lakini sheria hii ya ndoa imetungwa kibaguzi, imeenda kinyume kabisa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania. Ibara ya 13 inasema, watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki mbele ya sheria, lakini sheria hii inambagua mtoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 16 inatafsiri maana ya ndoa. Inasema, “Muungano lazima uwe wa hiari.” Sasa muungano huu unafanywa na wazazi, ndio wanaotoa ridhaa ya mtoto wa kike kuolewa chini ya umri wa miaka 18. Kwa maana hiyo basi, sheria hii ya ndoa iko kinyume, yaani yenyewe inaji- contradict yenyewe kwa yenyewe. Kwa maana hiyo, ninaitaka Serikali kuangalia vifungu hivyo ambapo vina contradiction yenyewe kwa yenyewa na pia na Katiba iweze kufanyia marekebisho sheria hii ya ndoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo hapa nchini Tanzania, pamoja na makubaliano ya Kimataifa ambayo tumekuwa tukiyasaini, tunaenda kinyume kwa sababu gani? Hizi ndoa ambazo zinafungwa za hawa watoto ambao wako chini ya umri wa miaka 18 zinaenda kinyume na hichi kifungu cha 16. Kwa maana hiyo, sheria hizo zote ni batili. Kwa hiyo, ninaitaka Serikali kutoa tamko na kusema kuwa watoto walioolewa chini ya miaka 18, ndoa hizo ni batili na waweze kurudi katika kazi zao, waende wakasome waweze kuwa kama sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mngenipata mimi…
(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)