Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumve
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii, lakini naomba uniruhusu nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Profesa Kabudi kwa taarifa yake nzuri sana na mimi nitatoa ushauri, lakini pia nitakuwa na maombi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika watu ambao nawaamini sana ni pamoja na Profesa Kabudi ambaye ni mbobezi wa mambo ya sheria kama ulivyo wewe Mwenyekiti wetu Mtemi Andrew John Chenge na ndiyo maana wamekuweka leo makusudi ili utusaidie baadhi ya mambo fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwenye maeneo mawili. Ushauri wangu wa kwanza, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aongeze pesa kwa ajili ya kugharamia mashahidi ili kusudi mashahidi hawa wanapokwenda kutoa ushahidi wao, waweze kuukamilisha mapema kwa sababu pesa hizi zinapochelewa au zinapokuwa kidogo, mashahidi hawaendi na kesi zinachelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, naomba sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG) iangalie namna nzuri zaidi ya kuwa na wataalam kwa maana ya makada ambao wataweza kusaidia hasa katika masuala ya kesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, inaweza ikatokea kesi ya mambo ya fedha, lazima kuwe na mtaalam wa mambo ya fedha, lazima kuwe na mtaalam kwa kesi hizi, lazima kuwe na mtaalam wa mambo ya ujenzi, mambo ya benki lakini la lazima kuwa na mtaalamu wa mambo ya IT. Kwa sababu kwa kufanya hivyo, kesi hizi wakati mwingine zinachelewa kwa sababu wataalam kutoka Ofisi ya AG katika fani hizi ni wachache. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu ili kesi hizi ziweze kwenda haraka daima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, kama nilivyotangulia kusema kwamba namwamini sana Profesa Kabudi, naomba nilete ombi kwako Mheshimiwa Waziri. Wilaya ya Kwimba tunazo Mahakama za Mwanzo kumi. Tunayo Buyogo, Nyambiti, Nyamikoma, Ngula, Bungulwa, Malya, Nyamikoma na Kikubiti. Mahakama hizi hazina Mahakimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mahakama za Mwanzo kumi zilizoko Wilaya ya Kwimba na jiografia ya Kwimba inajulikana, tuna Mahakimu wanne tu wa Mahakama za Mwanzo. Wanne tu kati ya Mahakama kumi. Sasa hili ni tatizo kubwa, kwa kufanya hivyo, hao Mahakimu hao huwa wanazunguka, lakini katika kuzunguka wakati mwingine wanachelewa kwa sababu hawana usafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri ninayemwamini na ninazungumza kwa upole kabisa. Kwa sababu suala hili tumekuwa nalo kwa muda mrefu. Nakuomba sana Mheshimiwa Profesa Kabudi, Mahakama kumi hizi bila kuwa na Mahakimu, ni kesi ngapi mnasema kwamba kesi ndani ya muda fulani ziwe zimeshapitiwa na kutolewa maamuzi, lakini Mahakimu wanne kwa Mahakama kumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine namwomba Mheshimiwa Waziri, kulikuwa na ahadi ya muda mrefu sana, tangu enzi za Mheshimiwa Waziri Mwapachu, akaja Mheshimiwa Migiro, akaja Mheshimiwa Nagu, Marehemu Mheshimiwa Kombani, Mheshimiwa Chikawe One na Chikawe Two, leo upo wewe kuhusu ukarabati wa Mahakama za Mwanzo katika Mahakama ya Nyamikoma na Kikubiji. Mahakama hizi ni za siku nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na tumeshaandika kwa maandishi. Pia Mahakimu hawa, hawana hata karatasi kabisa za kuandikia. Pia pamoja na upungufu wa Mahakimu, makarani hawapo, waliopo ni wahudumu. Sasa angalia, Mahakimu hawapo, makarani hawapo, sasa hebu niambie maana ya kuwa na Mahakama pale ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu mkubwa, sitaki kusema kwamba Mahakama hizo amezitelekeza kwa sababu siyo tabia yake. Sitaki kusema kwamba Mahakama hizo hazipendi au hazitaki, siyo tabia yake.
Namsihi sana mwana wa Singida, hebu Mahakama hizi sasa ambazo zilipangiwa kukarabatiwa muda mrefu kama ilivyoandikwa kwenye vitabu hivi, Mahakimu basi wapatikane, nyumba na majengo hayo yakarabatiwe na watu walioko kule ambao ni watumishi walioko chini yake, basi vifaa ambavyo wanavihitaji viweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante sana.