Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniapa nafasi na niungane na wenzangu wote kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wawili, Naibu Mawaziri wote wawili na Watendaji wao wote katika Wizara zao. Pamoja na pongezi zao hizo kipekee naomba niwapongeze madereva wao wote, wahudumu wao wote, na masekretari wao wote ambao wamefanya kazi hadi na wao wakaweza kuwakilisha hapa sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu naomba nianze na Usalama wa Taifa. Mwaka jana wakati nachangia nilizungumzia suala la Usalama wa Taifa na hoja kuu ilikuwa suala la kutekwa nyara, nilisema hapa kutekwa nyara siyo mchezo, wengine wanajifungia ndani halafu wanapiga simu wametekwa nyara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikasema naomba sehemu hii iongezewe pesa ili waweze kupata mafunzo zaidi na kununua vifaa zaidi vya kisasa, nafikiri kwa kufanya hivyo tutaweza kupunguza suala la kupekuliwa pekuliwa asubuhi, kuvuliwa nguo, kuvuliwa viatu na hata kufikia kwenye sehemu ya kwamba tunakuwa na wasiwasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za karibuni tumejionea jinsi watu wanavyojiteka nyara wenyewe na kufanya hii Idara ionekane kwamba haifanyi kazi wakati Idara hii inafanya kazi vizuri. Niombe Idara hii iendelee kuongezewa pesa ili wapate mafunzo zaidi na vitendea kazi ambavyo hata sisi vitatusaidia kutovuavua mikanda pale mlangoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, napenda nichangie kuhusiana na maadili ya Viongozi wa Umma, Sekretarieti ya Viongozi wa Umma wanafanya kazi vizuri sana wamekuwa wepesi sana wa kutukumbusha kujaza fomu ni vizuri pia. Katika kutukumbusha kujaza fomu basi kama kuna kitu kinatakiwa basi wakiingize kabisa pale ili tunavyorudisha zile fomu twende nazo sambamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekretarieti hii iongezeke zaidi badala ya kuangalia tu zile fomu twende kwenye neno kamili Maadili ya Viongozi, kama watavuka kufikia huko nafikiri hakuna Kiongozi atakayeitwa na Mheshimiwa Makonda hapa, hakuna Kiongozi atakayepelekwa Ustawi wa Jamii, hakuna Kiongozi tutakayemwona huko mitaani anatangazwa kwenye magazeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wajitanue zaidi wapewe pesa wajitanue zaidi watufuatilie kweli Viongozi maadili ni kweli au ni fomu tu hizo za kuhakiki mali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa. Idara hii imekuwa inafanya kazi vizuri, niipongeze Serikali kwa kuboresha majengo yao yote, wamefanya kazi vizuri sana, sasa hivi majengo yale matunzo yanaonekana, vifaa vinatunzwa kisasa na wafanyakazi wako kwenye amani. Hata hivyo, hawana pesa za kutosha kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali na kuweza kupata kumbukumbu mpya na nyaraka mpya ambazo nyingine ziko mikononi mwa watu huko vijijini. Kuna watu wana historia ya nchi hi, kuna watu wana kumbukumbu nzuri lakini wanashindwa kuzileta. Ni vizuri basi wakaongezewa pesa ili wafanye utafiti wa kina na kwenda kwenye maeneo mbalimbali ili tuweze kupata kumbukumbu nyingine na kupata nyaraka nyingine ambazo bado ziko mikononi mwa watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusiana na suala la utawala bora. Kazi imefanyika vizuri niwapongeze sana, lakini kuna baadhi ya Halmashauri kazi haziendi. Vikao vya Halmashauri vya kikanuni haviendi vimekuwa vikikatizwa mara kwa mara na wengine wanaitwa tu kipindi cha kupitisha bajeti sasa hii imekuwa ni tatizo. Tatizo la posho liko palepale, Diwani anaidai Halmashauri, Diwani utaidaije Halmashauri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naona Halmashauri zijipange, tunategemea kwamba tuna Wakurugenzi wazuri ambao ni wabunifu, basi waendelee kubuni mbinu mbalimbali ya kujipatia pesa ili kuweza kuziendesha zile Halmashauri, pia kuondokana na migogoro ya madiwani. Posho ya Madiwani pia ni ndogo, tunazungumza mara nyingi jamani mishahara ya watumishi tuongeze lakini haijazungumziwa Madiwani. Madiwani ni muda mrefu wanafanya kazi na posho ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki miezi mitatu yote Wabunge tuko Bungeni, lakini Madiwani bado wako na wananchi, shida za wananchi wanazo Madiwani, lakini bado posho iko vilevile, nimwombe Mheshimiwa Waziri waliangalie hili kuhusu posho ya Madiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine tena ambalo limezungumziwa juu ya kujipanga kwa ajili ya chaguzi za Serikali za Mitaa 2019. Nimefurahi kwamba mmeliona mapema na mmejipanga. Hata hivyo, wakati tunalipanga hili tuangalie kuna Kata nyingine, Mitaa mingine na Majimbo mengine ni makubwa kuliko tunavyofikiria. Kuna mitaa ambayo ina watu 10,000, nikitolea mfano katika Kata ya Msongola kuna mtaa wa Yangeyange una watu zadi ya 10,000, kuna mtaa wa Mbondole una zaidi ya watu 6000, sasa huo unakuwa mtaa au unakuwa kata. Ni vizuri basi wakati tunapanga uchaguzi huu wa mwaka 2019, basi waangalie jinsi gani ya kupunguza baadhi ya mitaa baadhi ya Kata na baadhi ya Majimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusiana na uchelewaji wa fedha za maendeleo katika Halmashauri, kwa kweli hiki ni kikwazo kikubwa sana ambacho hata Wabunge tunapoenda kwenye miradi mbalimbali kukagua huwa tunashikwa na butwaa kwamba tumepitisha pesa, wale wako tayari kufanya kazi lakini pesa haziendi. Basi ni vizuri tunavyoidhinisha kwamba pesa fulani ziende basi ziende kwa wakati na ikiwezekana ziende zikiwa zimekamilika ili miradi ile iweze kukamilika mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la TASAF na MKURABITA;, TASAF na MKURABITA imesaidia sana wananchi, sasa hivi wako katika mazingira mazuri sana, tumeangalia katika awamu ya tatu ya TASAF uwezeshaji wa wananchi kiuchumu wananchi sasa hivi wengi wameweza kupeleka watoto shule, wameweza kupeleka watoto kwenye zahanati na wameweza kubuni miradi mbalimbali ambayo inawaongezea kipato na hivyo kuwanyanyua kiuchumi. Ni vizuri basi hii sehemu ya TASAF ziongezewe pesa na ziende kwa wakati ili waweze kufanya kazi vizuri wananchi waweze kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika MKURABITA kazi imefanyika vizuri na akinamama wengi safari hii wameweza kunufaika na MKURABITA. MKURABITA vijana hawajanufaika, naomba utaratibu upangwe ili vijana nao waweze kunufaika katika mradi mzima wa MKURABITA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nizungumzie kuhusu TARURA niipongeze kwanza TANROADS kwamba imefanya kazi nzuri katika barabara kuu, barabara ni nzuri zinapitika, lakini huku kwenye TARURA bado pesa ni ndogo za kufanyia kazi barabara zile ni nyingi na fedha ni ndogo, kama ingewezekana tufanye mageuzi mazuri TANROADS wapewe asilimii 30, TARURA wapewe asimia 70 ili zile kazi za TARURA ziweze kuonekana kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia kuhusiana na taulo za kike. Taulo za kike limekuwa gumzo, lakini wachache ambao wamekubali kuwa wawazi, wapo akinadada ambao ni wasichana wanashindwa kabisa kwenda shule wanapofikia katika siku zao kutokana na kukosa taulo za kike. Wengine wanaamua kujistiri hata kwa majani au matambala mabovu ilimradi tu aende shule, yule mwenye moyo mdogo akifikia hali ile anaamua kotokwenda shule kabisa na hivyo kufanya mtoto wa kike ashindwe kuhudhuria masomo na kupoteza mwelekeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kupitia Wizara yake azishauri Halmashauri, tunayo mikoa ambayo inalima pamba na kama inalima pamba na sasa hivi tuna Tanzania ya viwanda, kwa nini ile mikoa isitengeneze viwanda vidogovidogo vya kutengeneza hizo pamba angalau za kuwastiri akinadada halafu ziuzwe kwa bei nafuu au ikiwezekana zitolewe bure kwa wanafunzi ili waweze kushiriki vizuri masomo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nitoe shukrani zangu na pongezi kwa Wenyeviti wangu wa Kamati wote wawili, wameonesha ushirikiano mzuri, kubwa zaidi kwa kuwa mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, niseme kwamba Mawaziri wetu wanashaurika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.