Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami nichangie katika hotuba mbili za Mawaziri wawili wa TAMISEMI pamoja na Utawala Bora. Naomba uniruhusu niwashukuru sana Viongozi wangu wakiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu, Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunipa salaam za pole baada ya kupata msiba wa marehemu mama yangu, nawashukuru sana kwa pole hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, niruhusu niwapongeze sana Mawaziri hawa wawili kwa maana ya Mheshimiwa Selemani Jafo pamoja na Mheshimiwa Kapt. Mst. George Mkuchika ni Mawaziri wanaochapa kazi zao vizuri na hotuba zao kwa kweli zinajielekeza wazi. Mchango wangu nitajikita sana katika kushauri na kuomba, lakini namwomba Mwenyezi Mungu anijaalie ili niishauri vizuri Serikali nisiende kwenye mkumbo ule mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa kwanza, nivipongeze sana vyombo vya usalama, vyombo vyetu hivi vinafanya kazi nzuri sana Usalama wa Taifa, pia TAKUKURU wanafanyakazi nzuri sana na niwaombe viongozi wao wakuu tunapoambiwa kwa mfano, makusanyo kuanzia Julai mpaka Machi kupitia TRA tumeweza kukusanya shilingi trilioni 11.78, nina uhakika kwamba TAKUKURU, Usalama wa Taifa wao ni wadau wakubwa sana kwa sababu mianya mingi ambayo imekuwa ikijitokeza wao wamekuwa jicho la kwanza kuiona na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili twende mbele zaidi, nawaomba sana wenzetu hawa wa Vyombo vya Usalama na TAKUKURU, katika nchi yetu hii ninyi ni watu muhimu kweli hasa kwenye suala zima la uchumi wa nchi yetu na usalama wa nchi yetu. Kwa hiyo, ombi langu kwenu ni kwamba endeleeni kuwa wazalendo kwa nchi hii ili kuweza kuokoa rasilimali za nchi yetu. Mkiwa wazalendo hata haya tunayoyazungumza humu ya mapato, upungufu huu, nafikiri mtatusaidia kabla hatujaenda kwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, narudia tena, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TIS nawashauri sana kwa sababu ninyi ni watalaam, mnajua mambo mengi, tunaweza tukakusanya pesa nyingi zaidi mkiamua kutusaidia, tunaweza tukazuia mambo mengi mkiweza kutusaidia kwa kutumia vizuri weledi wenu, nafahamu ni watalaam. Hebu ongezeni weledi wenu najua ni wazalendo sana sina shaka na hilo, lakini ongezeni jitihada ili kusudi nchi yetu iweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la TARURA. Chombo hiki tumekianzisha juzi ni chombo kizuri sana. Nina ushauri kwamba tulipoanzisha Mfuko wa Barabara tulikubaliana kwamba tuweke asilimia 70 kwa 30 ili asilimia 30 hii iende kwenye barabara za vijijini kwa maana ya Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kwa sababu nia ni njema sana, tunaambiwa kuna kilometa zaidi ya laki moja, kwa pesa hii ya asilimia 30, naona kama vile haitoshi. Naomba kwa sababu tulianzisha Mfuko huu kwa Sheria ya Mfuko wa Barabara, niiombe Serikali ilete amendments ili tujaribu kubadilisha kwa jinsi tutakavyoona inafaa, kwa sababu hatuwezi tu kuamua hapa sasa hivi, ni lazima tulete mabadiliko ya sheria kwa sababu Mfuko huu tulianzisha kwa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ambayo napendekeza kwa kuanzia na Wabunge tunaweza tukaridhia, tutoke kwenye asilimia 70 twende kwenye asilimia 65, twende taratibu ili tusiathiri upande mwingine, tufanye 35 kwa 65. Nafikiri kwa kufanya hivyo tutakuwa tumesaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa sababu ya pesa hizi kidogo na makusanyo yetu hayajatengemaa vizuri na jambo hili nililisema huko nyuma wakati Waziri wa TAMISEMI akiwa marehemu Kingunge Ngombale Mwiru. Lazima tufike mahali tuzisaidie Halmashauri zetu, kwa sababu ya pesa hizi kidogo tukiamua kama ni mwakani au lini, tukiamua kila Halmashauri ikawa na grader lake kwa ajili ya kutengeneza barabara zinazoharibika, ni uamuzi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Halmashauri ikawa na Grader hizi pesa kidogo kidogo hizi tunazokusanya, barabara inapoharibika mara moja mnaweka mafuta, grader inakwenda kutengeneza barabara inapitika asubuhi na mchana lakini inapitika masika na kiangazi ni suala la uamuzi. Kwa zile Halmashauri ambazo zina grader nafikiri barabara zao huwa haziharibiki mara kwa mara. Huo ulikuwa ni ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye suala la Jimbo. Naomba Mheshimiwa Jafo nilishakwenda kwake, Waziri wa Elimu anisaidie shule zangu mbili za sekondari na huwa napata tabu wanapogawa pesa wanasema shule kongwe, lakini kuna shule moja kongwe, shule ya wasichana, Sumve Girls ya A-Level. Inachukua wasichana kutoka nchi nzima wanachaguliwa wa Lindi wapo, kutoka Mtwara wapo, wanakwenda Sumve kusoma pale, ni shule ya siku nyingi. Shule hiyo amesoma Mama Maria Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali mahitaji yao wanayo, upanuzi wao wanahitaji mabweni mawili, madarasa manne, bwalo moja na jengo la utawala moja, kiasi cha shilingi kama zaidi ya milioni 400. Naomba sana Serikali shule hii ya wasichana waiangalie kwa jicho la huruma. (Makofi)

Pia kuna shule ya Taro. Kuna pesa zilitolewa mwanzo milioni 206 cha kushangaza Serikali kwa makusudi ikaja ikazibeba zile pesa zote, baadaye ikarudisha milioni 80. Nakuomba sana Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Jafo, nilishakwenda ofisini tukazungumza na watu wake, nikaenda kwa Mama Ndalichako, Waziri wa Elimu, nikazungumza naye, pesa hizo mpaka leo hazijarudi. Naomba ili tukamilishe mabweni mawili, madarasa manne, maabara mbili, tunahitaji milioni 168 ili kukamilisha kazi iliyobaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri pia hivi sasa kuna ongezeko kubwa la wanafunzi kuanzia ngazi ya chekechea, shule ya msingi mpaka sekondari, sina uhakika tumejiandaa namna gani. Kwa ongezeko hili kufuatana na maelezo ya kitabu chako, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, ni lazima tuangalie sasa miundombinu ya madarasa, vyumba vya Walimu, vyoo pamoja na Walimu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja