Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia hotuba hii ya Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda niungane na Mheshimiwa Peter Msigwa, Mheshimiwa Joseph Selasini na Mheshimiwa Hamidu Bobali kumpongeza Mheshimiwa Selemani Jafo kwa kazi nzuri anayoifanya ndani ya Wizara yake. Hii inadhihirisha ni jinsi gani Waziri huyu kwa kushirikiana na Naibu Mawaziri wake wanavyoweza kuisimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotakiwa. Pongezi sana kwa Waziri huyu na Manaibu wake Josephat Kandege na Mheshimiwa Joseph Kakunda, bila kumsahau Mheshimiwa George Mkuchika, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa maombi ya jumla ndani ya Mkoa wetu wa Njombe. Mara kwa mara nimekuwa nikisimama ndani ya Bunge hili Tukufu nikiuliza maswali, nikichangia Mheshimiwa Selemani Jafo watu wa Njombe shida yetu katika Wilaya zetu zote nne kwa maana ya Wanging’ombe, Ludewa, Makete na Njombe tuna uhaba wa Walimu wa Sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba watuongezee Walimu wa sayansi, tunaomba watuongezee Walimu wa shule za msingi, tunaomba watuongezee Wauguzi na wataalam wa afya. Mheshimiwa Jafo tunamtegemea sana katika hili ili tuendelee kumsifu kwa utendaji wake mzuri wa kazi na tuna imani na yeye, sisi watu wa Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Selemani Jafo ukurasa wa 112, ameainisha mikakati mahsusi ambayo ataifanya mwaka huu mwaka wa fedha 2018/2019 na katika malengo hayo mahsusi ambayo ameainisha ni pamoja na ujenzi wa hospitali 67 katika Halmashauri 67 za Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri Jafo nimekuwa nikiomba mara kwa mara hospitali ya Wilaya ndani ya Halmashauri ya Wanging’ombe, namwomba Mheshimiwa Jafo na watu wa Wanging’ombe tuwe wanufaika katika kuhakikisha kwamba mwaka huu tuanze kujengewa hospitali ya Wilaya ya Wanging’ombe ndani ya Halmashauri yetu ya Wanging’ombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Wilaya ya Njombe katika Halmashauri ya Njombe Vijijini, wananchi wameshaandaa eneo square meter 52, wananchi wamejitolea ili kuiweza kujenga hospitali ya Wilaya. Tunaomba sasa kwa kuwa wananchi wameshajitolea eneo la square meter 52, Wizara sasa watusaidie tuingie katika malengo haya mahsusi ya kujengewa hospitali ya Wilaya ya Njombe ndani ya Halmashauri ya Njombe Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la elimu ndani ya Wilaya ya Wanging’ombe. Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia pesa na kushirikiana na wananchi pia katika kuhakikisha kwamba tumeweza kuboresha miundombinu ya shule ya Wanike Sekondari na miundombinu ya Makoga Sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Katibu Mkuu alikuja pale Makoga na Wanike Sekondari akatoa maelekezo ya kufanya. Sisi watu wa Wanging’ombe tumefuata maelekezo yale, tumekamilisha, miundombinu iko vizuri, tunachokiomba kwa Serikali ni kuhakikisha kwamba wanatupa kibali hivi sasa tuweze kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano kuanzia mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la vituo vya afya, Wanging’ombe tuna kituo cha afya cha miaka mingi sana cha Makoga. Kituo kile hatuna huduma ya upasuaji kwa sababu hatuna chumba cha upasuaji. Ikitokea mtu anahitaji huduma ya upasuaji, inabidi atembee kilomita zaidi ya hamsini (50) kwenda kufuata huduma ya upasuaji katika hospitali ya Kibena. Tunaiomba Serikali itujengee chumba cha upasuaji na vilevile tunaiomba Serikali itupatie ile ambulance na vitanda viwili ambavyo vilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Kituo cha Afya cha Palangavano, tunaishukuru Serikali kutupatia milioni 100 kuweza kujenga kituo kile. Niitarifu tu Serikali kwamba zile milioni 100 tuna uwezo wa kujenga mpaka kufikia lenta, tunaiomba Serikali mtupatie pesa tuweze kumaliza kituo kile cha Palangavano kwa sababu kituo kile ni kituo cha kimkakati, kipo katikati ya Wilaya ya Wanging’ombe, wananchi kutoka Luduga, kutoka Malangali, Usuka, Ilembula, Igwachanya ni rahisi kutumia kituo kile cha afya, hivyo basi naiomba Serikali iweze kutupatia pesa kwa ajili ya kuweza kumalizia ujenzi wa Kituo cha Afya Palangavano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara katika Halmashauri ya Wanging’ombe, tunaomba kilomita mbili tu Igwachanya na tunaomba kilomita mbili Ilembula, lakini vilevile tunaomba watujengee daraja letu la halali ambalo liko pale Kata ya Ilembula, kwani kipindi cha masika tunapata tabu kuvuka, tunaomba mtusaidie kwa sababu daraja lile ni muhimu, watu wanalitumia kwenda Makao Makuu ya Wilaya ya Wanging’ombe kwa sababu ile Tarafa nzima ya Wanging’ombe na baadhi ya Kata kutoka Tarafa ya Imalinyu wanatumia daraja lile kupita kwenda Igwachanya katika Makao Makuu ya Wilaya ya Wanging’ombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende Ludewa tuna shule yetu ya sekondari ya Manda, tunaiomba Serikali watusaidie tuweze kukamilisha kuboresha mabweni, hivi sasa tupo katika kuboresha miundombinu ya maji na umeme, watusaidie tuweze kukamilisha na baadaye watupe kibali cha kuweza kupandisha hadhi ya kuweza kuchukua watoto wa kidato cha tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la afya ndani ya Wilaya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa. Wananchi wa Ludewa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kujenga vituo vya afya 17, tuko kwenye mchakato wa kujenga vituo vya afya 17. Uwezo wetu ni kujenga kuanzia ngazi ya foundation mpaka kuezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokiomba kwa Serikali watusaidie katika suala zima la finishing kwa sababu wananchi wa Ludewa kwa kushirikiana na wadau tunaweza kujenga kuanzia msingi mpaka kuezeka. Hivyo ombi letu kubwa kwa Serikali ni kutusaidia katika finishing ya vituo hivi vya afya 17 ndani ya Halmashauri ya Ludewa ili viweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara za Halmashauri ndani ya Wilaya ya Ludewa, tunaomba watujengee barabara ya Lupingu kwenda Matema beach. Barabara hii ni muhimu katika suala zima la ulinzi na usalama kwa sababu barabara hii iko karibu na mpaka wa Malawi na Tanzania. Vilevile barabara hii itatusaidia katika masuala ya utalii na itasaidia kufungua uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Ludewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendee kwenye Halmashauri ya Makete. Kama unavyojua jiografia ya Wilaya ya Makete iko vibaya sana siyo rafiki katika suala zima la kufikika. Hivyo basi, tunaomba ile Tarafa ya Ukwama ipatiwe kituo cha afya ili wananchi wale wa Tarafa ya Ukwama ambao wapo pembezoni sana Makete waweze kupata huduma ya afya kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie katika suala zima la Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na Vijana, naomba Serikali ilete sheria ndani ya Bunge tuweze kupitisha ili tuweze kuwabana Wakurugenzi ambao hawatoi pesa zile za mikopo ya akinamama na vijana katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.