Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kwa ajili ya kuchangia kwenye hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwigulu Nchemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kumweleza kwamba mwishoni sitakuwa tayari kuunga mkono hoja ya Wizara yake na mambo yakienda hivi, basi nitaishia kushika shilingi kwa sababu kuna mambo ya msingi, sisi kama wakulima wa korosho tungehitaji kuyasikia na yanapata suluhisho katika Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi kirefu sana korosho tumekuwa tukiisifu kila mara kwamba ni moja kati ya mazao makubwa kabisa ya biashara kwa ajili ya Tanzania. Kwa mwaka huu peke yake asilimia 90 ya zao la korosho imekuwa exported kupelekwa katika nchi ya India. Ukiangalia kwa kina, watumiaji wakubwa kabisa wa korosho wapo katika nchi za Ulaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tulikuwa tukijiuliza kila mara, inakuwaje sasa Wahindi ndio wawe wanunuaji wakubwa wa mazao yetu badala ya kuwatafuta wale final consumers tukawashauri wao waje kutuwekea viwanda katika maeneo yetu?
Kwa hiyo, kimsingi tunaomba viwanda vyetu vile ambavyo vilikuwa vinazalisha korosho vifufuliwe kwa kutafuta watu kutoka Europe ambao na wenyewe wananunua korosho kwa madalali kutoka India. Naomba hili lifanyiwe kazi.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumshukuru kidogo Mheshimiwa Waziri Mkuu…
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika kipindi kilichopita amejitahidi na ameondoa tozo mbalimbali ambazo zilikuwa kero kwa ajili ya wakulima wa korosho lakini bado kuna mambo ya msingi ameacha.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Tunafahamu kabisa Serikali iliamua waziwazi kuondoa na kupunguza kodi ya magunia...
MHE. CECIL D. MWAMBE: …zilitumika kwa ajili ya wanachama wa vyama mbalimbali vya Ushirika katika Vyama Vikuu vya Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako, nikueleze kwamba kumefanyika ubadhirifu mkubwa sana katika biashara ya magunia na nashukuru Mheshimiwa aliyetoka hapa kuongea, anaitwa Mheshimiwa Kaunje alikuwa Mwenyekiti kwa kipindi kilichopita, sasa hivi tupo naye hapa Bungeni, anaweza akaisaidia Wizara yako kutueleza kimsingi. Wakulima wa korosho Mtwara wanakatwa shilingi 56 katika kilo moja kwa maana kwamba wanakatwa shilingi 5,600 ili kuweza kujaza gunia moja, kugharamia gharama za magunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda sokoni sasa hivi unaweza kununua gharama ya gunia moja kwa shilingi 4,000. Kitu ambacho tunajiuliza, magunia haya ambayo tunaambiwa yamesamehewa Kodi ya Ongezeko ya Thamani lakini mkulima anapata gunia hili kwa shilingi 5,600, tunaomba kufahamu hii biashara inakuwaje? Nani ana maslahi na hii biashara na tungependa tupate majibu yako hapa karibuni, kwa sababu kama nilivyoeleza, kesho naweza nikashika shilingi yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunataka tufahamu, kwa sababu kwa kipindi kirefu, tulikuwa tukiona wakulima wa korosho wanashindwa kulipwa pesa zao kwa wakati; imetokea sasa hivi na tushukuru uongozi wa Serikali ya Mkoa, kwa kupitia Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, ametueleza wazi kabisa kwamba vyama 49 vya msingi vya Tandahimba vimeshindwa kuwalipa wakulima shilingi bilioni 1.4. Tunataka tujue wazi kabisa kwamba wakulima hawa watapewa lina pesa zao kabla Mheshimiwa hujahitimisha hotuba yako?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imekuja kutokea na jambo linguine, vyama 36 vilivyopo chini ya Ushirika wa MAMKU kutokea Wilaya ya Masasi na vyenyewe vimeshindwa kuwalipa wakulima hawa four billion katika msimu huu tu mmoja; hivi ndiyo vitu ambavyo vimewasilishwa kwetu. Tumshukuru Mheshimiwa Mrajisi, alikuja pia kule, ameongea na wakulima, wana mambo mengi Mheshimiwa ya kukueleza, lakini kwa bahati mbaya sana kila mara tulipojaribu kutaka kukueleza jambo hili ulikuwa ukikosa nafasi, machache uliyasikia, lakini ukitaka kusikia mengi zaidi uje kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kabisa tunasema kwamba haturidhiki na utendaji wa bodi. Bodi ya Korosho imekuwa ikiyafahamu matatizo haya kwa kipindi kirefu sana, lakini imekuwa ikitumika kisiasa. Ukitaka kupata kazi kwenye Bodi ya Korosho, basi kwanza lazima uwe mstaafu wa siasa. Ndugu zetu wa Vietnam wameweka pale watu ambao ni creative, vijana wenye nguvu, wenye uwezo wa kuleta mawazo mbadala kwa ajili ya kuboresha korosho zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu wazi kwamba Vietnam walikuja kuchukua mbegu za korosho Mkoa wa Mtwara, tena walikwenda kuchukua katika kijiji ambacho kipo Jimboni kwangu, kinaitwa Kijiji cha Lukuledi. Wale wenzetu wamekuwa wakitumia zao la korosho kama zao kuu la uchumi kule kwao. Sisi sasa hivi tunaweka watu ambao ni wazee katika bodi, waliostaafu kwenye active politics, tunataka wao wawe creative. Tumeona hawawezi kutufanyia chochote. Wameshindwa kutatua kero mbalimbali za wakulima! Hii ipo katika bodi nyingi. Bodi nyingi sasa hivi zinatumika kisiasa, tunaomba ziwe dissolved, wawekwe pale watu ambao ni creative kwa ajili ya kusaidia Taifa na wakulima wa mazao mbalimbali katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, suala hili tulikupa taarifa mapema sana, lakini tunaona mpaka sasa hivi halijachukuliwa hatua. Naomba niliongee hapa na nitaomba Wabunge wanaotoka Mtwara na Wabunge wote walio na maslahi na masuala ya korosho watani-support kuhakikisha tunashika shilingi yako kama hautatueleza hatua gani za msingi utazichukua kwa ajili ya kuhakikisha watu hawa wanachukuliwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale waliopoteza pesa ya ukulima ambayo ni five billion katika msimu huu, lakini pia tunataka tuone bodi ilichukua hatua gani? Kama ilishindwa kuchukua hatua kwa wakati, basi bodi na yenyewe sasa hivi ichukuliwe hatua kwa sababu imeshindwa kufanya kazi zake za msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikueleze wazi, makato ya korosho yalifikia mpaka shilingi 264 katika msimu uliopita, lakini ukiangalia katika hizi shilingi 264, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu amepunguza baadhi ya tozo, lakini bado kuna tozo pale ndani ambazo ni kero kubwa kwa wakulima, tunataka sasa tukae ili wakulima watakapokuwa wanaanza kutayarisha mashamba yao basi wajue wazi bei ya korosho itakuwa ni kiasi gani? Kwa sababu sasa hivi watu wamekuwa wakilima kwa mazoea zao la korosho zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna hata mwaka mmoja ambao mkulima anaweza aka-realize kwamba sasa hivi nimepata faida, kwa sababu anatumia gharama kubwa kutayarisha mashamba, lakini pesa anayokuja kuipata mwishoni ni ndogo sana na ukichanganya na huu utitiri wa nvyama lakini pia pamoja na watu wasiokuwa waaminifu wanaodhulumu pesa zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni wazi kabisa tuseme haturidhiki na hali ilivyo katika zao la korosho katika Mikoa ya Mtwara na Lindi na maeneo mengine yote ambako wanalima korosho. Tuseme wazi, tunataka mabadiliko makubwa yafanyike kabla ya msimu ujao wa korosho haujaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu kuna kitu kinaitwa CDTIF. Wale watu lengo lao la msingi ilikuwa ni kwa ajili ya kusaidia kufanya utafiti, kuendeleza zao la korosho, kusaidia wakulima wadogo wadogo kuwapa mbegu, kuwasaidia kupata mikopo ili kudumisha na kuendeleza zao la korosho. Jambo hili halifanyiki na wale watu. Sasa hivi wamegeuka na kuamua kuwa wafanyabiashara. Wanajihusiasha na biashara ya magunia kwa sababu ndicho kitu kinachowapa wao fadia. Wamejihusisha na biashara ya pembejeo, pembejeo hizi haziwafikii wakulima kwa wakati, mpaka sasa hivi imefika wakati uzalishaji unapungua kwa sababu hawapati pembejeo kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wanashindwa kufanya research. Kuna wataalam walikuja kule kutoka SUA, wamekuja na utaratibu mpya sasa hivi, wana madawa ambayo yanaitwa GI Grow. Tunaomba sasa nalo liingizwe katika ruzuku kwa sababu tusiangalie tu kuondoa au kutumia sulfur ya maji lakini pia tuangalie jinsi ya kuwaongezea tija wakulima katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nikueleze kwamba watu wa Mtwara wanakusubiri sana wakakueleze kero zao. Bahati mbaya sana viongozi mnapokuja mnakuwa na utaratibu wa kutaka kukutana na viongozi wa Vyama vya Ushirika, kukutana na viongozi wa Bodi. Wale sio watu wenye kero, watu wanaokerwa kule ni wale wakulima wa chini kabisa ndio ambao wanahitaji wakuone wewe. Mkifika pale, achaneni na haya mambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakulima ambao wanadhulumiwa, Mheshimiwa Katani hapa kaongea kwa kirefu kidogo, lakini nami naomba nichangie hapa. Kwenye Jimbo langu kuna kijiji kimoja peke yake kimepoteza tani zake 103 za korosho. Sasa hivi ni mwaka wa nne hawajapewa fidia kuhusu korosho zao, Bodi ya Leseni ipo pale, inashindwa kuwasaidia chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba tukuelekeze majipu ya msingi ambayo tulitamani tuyaone yanatumbuliwa katika kipindi hiki tunachoelekea. Bodi ya Korosho tumesema sisi kama Wabunge tunaotokea Mtwara, hatuoni uwezo wao wa kufanya kazi, bodi ile imezeeka, tunataka wabadilishwe wawekwe watu ambao ni creative kwa ajili ya kuendesha zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wasimamizi wa Mfuko wa Leseni za Maghala na wenyewe hatuwahitaji wakae pale, wawekwe watu ambao nafikiri wanaweza kweli wakawasaidia watu wa maghala pamoja na wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikueleze, ule Mfuko wa CDTIF ambao Mheshimiwa Bwanausi kama ulimsikia pale akisema, wanafanya kazi zao kwa siri kubwa sana. Hatujui wanapata shilingi ngapi na wanazitumia kufanyia nini, lakini kiasi kikubwa cha pesa wanazozikusanya zinakwenda kufanya shughuli za utawala badala ya kwenda kuwasaidia wakulima katika maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine kubwa linatukera linaitwa export levy. Tunaomba hii pesa inapokusanywa, ipelekwe moja kwa moja katika Halmashauri husika na isibaki na hawa watu kwa sababu wanaitumia vibaya. Haiwasaidii wakulima, inawasaidia wao wanaokaa maofisini, wakulima wanaendelea kuwa maskini, wao wakijilipa mishahara mikubwa katika maeneo yao. (Makofi)
Kwa hiyo, Mheshimiwa nikueleze wazi, utakapokuwa unahitimisha hotuba yako, tunaomba tupate majibu kuhusu masuala yetu haya na usipofanya hivyo, sisi tutashirikiana kwa umoja wetu, tutahakikisha tunashika shilingi yako mpaka pale utakapotupa suluhisho la matatizo tuliyonayo. Ahsante, siungi mkono hoja.