Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuimarisha huduma ya matibabu ya kibingwa nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hivi sasa kumekuwa na uimarishwaji wa huduma ya matibabu ya kibingwa Tanzania ikiwemo kupandikiza figo na kupandikiza vifaa vya kuongeza usikivu. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri tumeona wagonjwa wa figo walikuwa wanatibiwa nje ya nchi kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 100, lakini hivi sasa tunaishukuru Serikali yetu hii ya Chama cha Mapinduzi sikivu kuleta huduma ndani ya nchi yetu kwa gharama nafuu ya shilingi milioni 20. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shilingi milioni 100 sasa tunakwenda kutibu wagonjwa watano, hili nalo dogo? Tumeona ongezeko la wagonjwa wa sukari, pressure na magonjwa yote haya yanapelekea matatizo ya figo.

Naipongeza Serikali imeweza kuleta huduma hii wakati muafaka ambao Tanzania tunahitaji huduma hiyo kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nikwambie dada yangu Mheshimiwa Ummy, kwa kazi hii nzuri mnayoifanya, historia itakukumbuka. Profesa Mseru - Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, endelea kufanya kazi baba yangu, kazi yako nzuri, historia itakukumbuka. Vilevile natambua kabisa jitihada hizi ni msukumo mkubwa na jitihada kubwa anazozifanya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la Saratani ya shingo ya uzazi. Kwanza niipongeze Serikali yangu kwa kuwa sikivu. Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu. Ukifuatilia hotuba yangu ya bajeti iliyopita ya mwaka 2017/2018 niliishauri Serikali ijikite katika suala zima la kinga katika magonjwa ya saratani ya shingo ya kizazi. Naipongeza Serikali na ninaishukuru, hivi sasa imeanza kutoa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanjo hii sasa hivi inatolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 14, lakini naendelea kuiomba Serikali yangu sasa, nawapa ushauri mwingine, mhakikishe kwamba chanjo hii ya saratani ya shingo ya kizazi, mtoe elimu kule vijijini ili wananchi waelewe umuhimu wa chanjo hii. Kwa sababu jambo lolote jipya linapoingia nchini kwetu, watu hujawa na hofu. Kwa hiyo, kwa kupeleka elimu kule vijijini wakajua umuhimu huu, sasa watajitokeza wasichana wengi na wazazi watapeleka wasichana wao kwenda kupata huduma hiyo ya chanjo ya saratani ya shingo ya uzazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa wale wanawake ambao wameshazidi umri wa miaka 14, naishauri Serikali iongeze jitihada za kuwapima ili tuweze kujua wangapi wamepata matatizo hayo na wangapi hawajapata. Kwa wale ambao wameshapata, basi waanze kupata matibabu kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la Hospitali za Rufaa za Mikoa. Naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kutupatia fedha, hivi sasa tupo kwenye ujenzi wa Hospitali yetu ya Mkoa ya Njombe.

Mheshimiwa Ummy nataka ukija kutoa majumuisho yako hapa wakati unajibu hoja, nataka kujua Hospitali ya Mkoa wa Njombe, Serikali mmetupangia pesa shilingi ngapi ili kuweza kuikamilisha kwa sababu mkoa wetu ni mpya. Kila siku nasema mkoa wetu mpya bado mambo mengi tunahitaji. Kwa hiyo, naomba mtupe kipaumbele sisi watu Njombe, mtupe pesa za kutosha ili tuweze kukamilisha ujenzi wa hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kuzungumzia suala la hali ya mapambano dhidi ya UKIMWI. Nimesoma taarifa ya hali ya maambukizi ya UKIMWI nchini (Tanzania HIV Impact Survey 2016/2017); napenda kuishukuru Serikali na wadau mbalimbali, hivi sasa Mkoa wetu wa Njombe maambukizi ya UKIMWI yanazidi kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya mwaka 2011/2012 inaonesha kwamba maambukizi ya UKIMWI yalikuwa asilimia
14.8 Mkoa wa Njombe, lakini taarifa ya mwaka 2016/2017 maambukizi ya UKIMWI yameshuka mpaka asilimia 11.4. Ninatambua hizi ni juhudi za Serikali pamoja na wadau mbalimbali wanaopambana na vita dhidi ya UKIMWI. Vilevile ushauri wangu kwa Serikali na wadau, ni muda muafaka sasa, mshuke kule chini kwa wananchi mkawasikilize maoni na ushauri wao ili kwa pamoja muweze kujua jinsi gani mtaweza kumaliza tatizo hili la UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeze Wizara ya Afya kwa kazi nzuri iliyofanya katika kuhakikisha kwamba sasa hivi dawa za Kifua Kikuu (TB) kwa watoto wetu zinapatikana. Zamani watoto wadogo walikuwa hawana dozi kamili ya dawa za kifua kikuu. Utakuta kile kidonge kinakatwa robo tatu, robo mbili, mara mtu anakosea kukata, mtoto anaongezewa dozi, mara mwingine anapewa dozi haijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwamba sasa wameleta dawa za kifua kikuu kwa ajili ya watoto, dozi ambayo iko rafiki kwa watoto. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, dawa ile ina flavor ya matunda, kwa hiyo, hata mtoto anakuwa anakunywa kwa urahisi na anaweza kupata matibabu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa napenda niungane na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kumpongeza Profesa Mohamed Janabi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kazi nzuri anayoifanya kuhakikisha utoaji wa matibabu ya moyo nchini kwetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.