Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niende direct to the point na naingia kwenye ukurasa wa 101 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu haki na maendeleo ya mtoto. Ninashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri amekiri mwenyewe kwamba ukatili dhidi ya watoto bado ni tatizo kubwa hapa nchini na asilimia 28 ambayo imeoneshwa kuongezeka katika wanaoripoti kuanzia mwaka 2016/2017 mimi ninasema bado hiyo itakuwa ni kidogo ikiwa Watanzania wengi watalielewa hili suala. Kwa hiyo, tunaweza tukafika hata kwenye asilimia 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa narudi tena kwenye ombi langu, namwomba Mheshimiwa Waziri kigezo cha kusema kwamba hawa wabakaji sugu, nikisema wabakaji sugu wa watoto wa kike na wa kiume sikusudii mtu mwingine yoyote, sikusudii mbakaji wa mume kwa mke, hilo ni lao. Nakusudia watoto wadogo wa kike na wa kiume. Naomba sana tuache hii ya kufikiria kwamba tunapowaamulia au kuwatungia sheria hawa wabakaji sugu kuhasiwa, ni kosa au ni haki za kibinadamu, naomba nije kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 30. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ninukuu; “Haki na uhuru wa binadamu ambapo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii havitatumiwa na mtu mmoja kwa maana ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma.”
Pili, inasema: “Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika sehemu hii ya Katiba yanayofafanua misingi ya haki, uhuru na wajibu wa binadamu, hayaharamishi sheria yoyote iliyotungwa wala kuzuia sheria yoyote kutungwa au jambo lolote halali kufanywa kwa mujibu wa sheria hiyo kwa ajili ya:- (a) kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru na haki za watu binafsi.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutumia ibara hiyo, ninaomba nikushawishi na ninaomba nishawishi Bunge, mwisho wa siku tusipolivalia njuga jambo hili litakuwa ni janga la kitaifa. Ninasema hivi nawaambieni mfano, mwisho wa siku hatima yake, kiongozi ambaye yupo mbele yetu sasa hivi ni mwanaume, atakuja kiongozi ambaye ana ndoa ya jinsia moja, hilo ndiyo mwisho wa siku. Kwa hiyo, naomba tusifanye masihara wala tusione hili jambo ni la utani. Taifa letu la kesho linakwenda kuangamia. Taifa letu lenye utamaduni bora Tanzania linakwenda kutoweka ikiwa tutakuwa hatupo makini katika suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema, Mheshimiwa Waziri kaa na Wizara husika tuangalie namna bora ya kutengeneza sheria ya kuwahasi wabakaji sugu wa watoto wetu wa kike na wa kiume ili tuweze kuondokana na janga hili sugu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo yangu ya leo.
Ahsante sana.