Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nikushukuru kwa kunipa muda huu wa kuweza kuzungumzia Wizara hii muhimu sana kwa sisi akinamama. Naomba nimshukuru kwanza Mungu ambaye ametulinda siku hii ya leo, ametupa kibali tuko mahali hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya, tunaona kwa ajili ya afya na pesa nyingi ambazo amezitenga tunaona na kushuhudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Waziri Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa nzuri. Kusema kweli Mheshimiwa dada Ummy Wizara ameiweza, lazima tumpongeze, Wizara ameiweza na ameimudu, hongera sana, Mungu ataendelea kukutetea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikipongeze Kitengo cha Jakaya, Profesa Janabi pamoja na Mkurugenzi wa Ocean Road, Kitengo cha Sukari, Meno, MSD kwa kazi nzuri ambayo walikuja Mkoa wa Katavi kupima afya za wananchi wa Mkoa wa Katavi. Naomba sana kazi hii Mungu ataendelea kuwalipa na waendelee kuwatumikia Watanzania kwa sababu Katavi ni mbali, lakini walikuja kuangalia afya za Watanzania wa Mkoa wa Katavi na wasichoke nitawaomba waje tena kuangalia kwa sababu walipunguza matatizo mengi ingawa hawakumaliza lakini matatizo waliweza kuyaona na kuweza kuyamudu kiasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi ni mkoa mpya. Tunajua Serikali katika ile mikoa mipya imepanga kujenga hospitali za mikoa. Mkoa wa Katavi 2017/2018 tulipangiwa bilioni moja, lakini pesa hii hatuwezi kuijua ilienda wapi, kwa sababu mpaka leo uwanja ule uko wazi

wala hakuna kitu chochote ambacho kilifanyika, wala kuonesha dalili ya kujengwa hospitali ya Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu vilevile sijaona kama tumepangiwa pesa au kuna dalili kwamba tumeambiwa kuwa tutajengewa hospitali ya mkoa sijaona dalili ya aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi, jiografia ni mbaya sana. Nashukuru sana Mheshimiwa Ummy alifika alijionea uhalisia, maana angekuwa hajajionea uhalisia angesema sifahamu, lakini uhalisia wa Mkoa wetu wa Katavi anaufahamu vizuri sana. Nashukuru sana Mheshimiwa Ummy alikuja Mkoa wa Katavi na vilevile aliniahidi Wadi moja katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda. Naisubiri sana hiyo Wadi ambayo aliwaahidi wananchi wa Wilaya ya Mpanda Manispaa, alisema atawajengea Wadi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kwa sababu hii hospitali ya Mkoa inapangiwa pesa na mpaka sasa hivi hakuna kitu kinachoendelea, naomba kwa vile hospitali ya Manispaa ya Mpanda ina eneo kubwa sana na ndani ya hospitali ya Manispaa ya Mpanda tuna matatizo mengi makubwa kwa sababu majengo ya Wadi ni machache, Madaktari hatuna, Manesi ni wachache mno, Wahudumu ni wachache mno kusema ukweli!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile hospitali ya Manispaa ya Mpanda ndiyo imekuwa kama hospitali ya Mkoa, sasa wananchi wote wa Mkoa wa Katavi wanakwenda kwenye ile hospitali, wodi chache, vitanda hakuna! Sasa namwomba sana dada yangu Mheshimiwa Ummy, mpenzi wangu, atusaidie basi aongeze hata Wadi tatu ndani ya hospitali ya Manispaa ili tuweze kukidhi mahitaji ya wananchi wa Wilaya ya Mpanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie kwa sababu wananchi wa Mpanda wanapata shida sana kimatibabu, ukiangalia vifaa tiba hatuna, vifaa tiba vyote, x-rays na kila kitu ni vibovu. Namwomba sana dada Ummy, Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto atusaidie vifaa tiba hatuna, wananchi wa Mpanda wanapata shida sana, wanakwenda Mbeya, wanakwenda Ikonda, lakini tukiiboresha hospitali ya Mpanda sidhani kama wananchi wa Mpanda watahangaika. Namwomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Ummy alikuja katika Mkoa wa Katavi akaenda katika Wilaya ya Mlele katika Tarafa ya Inyonga. Namshukuru alipandisha ile hospitali ikawa hospitali ya Wilaya, kile kituo cha afya cha Inyonga. Hata hivyo, mpaka leo hatujapata hati na kama hujapata hati ya kuwa hospitali ya Wilaya ina maana vitu vyote vinasimama, ina maana Madaktari wale bado wanaendelea kuwa Madaktari wa kituo cha afya na dawa zinaendelea kuwa zile za kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ummy, akitusaidia kutupa hati kamili sasa kwa sababu jengo la mortuary limekwisha, kila kitu ambacho vile vigezo vyote walivyoviweka, vimekwisha, tunaomba hospitali ya Mlele ipatiwe hati iwe hospitali kamili ya Wilaya ya Mlele ili iweze kupunguza kasi ndani ya Manispaa ya Mpanda. Namwomba sana Mheshimiwa Ummy ili tuweze kupunguza matatizo kwa wagonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Wilaya yetu ya Manispaa ya Mpanda tuna vituo viwili vya afya. Vituo hivyo ni kituo cha Ilembo pamoja na Mwangaza. Vituo hivi havijapangiwa pesa, Mheshimiwa Ummy naomba atuoneshe katika hivi vituo vya afya ambavyo vinapunguza kasi ya uzazi salama, kwa ajili ya msongamano pale Makao Makuu Manispaa na hajavipangia pesa. Naomba Mheshimiwa Waziri kesho wakati anafunga basi atanionesha vituo hivi viwili vya afya, Kituo cha Afya Ilembo pamoja na Mwangaza pesa yake iko wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunahitaji Kituo cha Afya kati ya Mwamkulu na Kakese kwa sababu ni distance ndefu kuja Mjini vilevile kuna watu wengi zaidi. Tulikuwa tunahitaji kituo cha afya katika maeneo hayo ya Mwamkulu na Kakese. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru masuala ya Bima ya Afya hususan Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Nashukuru Mfuko huu unafanya kazi vizuri sana na Mkurugenzi anafanya kazi vizuri sana, ndani ya mikoa yote vituo vipo na wafanyakazi wapo. Hata hivyo, kila Mtanzania anahitaji kutibiwa vizuri na vilevile katika mfumo wao waliouweka ndani ya makundi kuwapa kikundi cha SACCOS na kadhalika ndiyo uwalipie Bima ya Afya Sh.79,000 ni sawa, lakini kila Mtanzania anahitaji matibabu, naomba huu mfuko…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.