Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Naomba pia nami nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa maisha ya binadamu. Pia sichelewi kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jiji la Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kuipongeza Serikali kwa kuweza kupokea bilioni moja na milioni mia nne kama mpango wa Serikali wa kuboresha vituo vya afya kwa ajili ya mama na mtoto. Labda katika hilo niseme tu kwamba nimepokea milioni mia tano kwa Kituo cha Afya cha Makorora, milioni mia tano kwa Kituo cha Afya cha Mikanjuni, lakini pia milioni mia nne kwa Kituo cha Afya cha Ngamiani, kwa hilo nashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizi naomba Waziri wa Afya anisikilize kwa makini. Tanga ni Manispaa ya kwanza Tanzania tangu mwaka 1951, lakini mpaka leo miaka 57 baada ya Uhuru hatuna hospitali ya wilaya. Halmashauri tumejitahidi kidogo tukaweza kujenga jengo la administration block katika Kata ya Masiwani Shamba, kata mpya ili tuweze angalau kujikongoja tuweze kupata hospitali ya wilaya, lakini bado haijatosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya halmashauri mwaka huu tumetenga takribani shilingi za kitanzania milioni mia tatu. Kwa hiyo namuomba Waziri wa Afya atutafutie angalau bilioni mbili, tukichanganya na milioni mia tatu hizi angalau tunaweza tukapata jengo la OPD ili wananchi wetu waweze kupata huduma za hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, kuna upungufu mkubwa katika Jiji letu la Tanga katika sekta ya afya. Kuna upungufu wa watumishi, nikiwa na maana ya Wauguzi na Madaktari Bingwa. Kwa hiyo, Waziri napo kama wanavyosema wataalam the good charity beginning at home. Sasa naomba atupe upendeleo maalum ahakikishe katika hospitali yetu ya wilaya hiyo ambayo tunakusudia kuijenga tujiandae na Madaktari Bingwa na Wauguzi wa kutosha lakini hili la upungufu wa watumishi limepelekea sasa siku za weekend vituo vingi vya afya na zahanati kufungwa saa nane na nusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo nafikiri Wabunge wenzangu mtakuwa ni mashahidi; huu ni utaratibu ambao upo nchi nzima. Sasa inasababisha wananchi wetu kupata shida. Wananchi wanahoji sisi Watanzania tuna mkataba na Mungu? Kwamba kuumwa mwisho saa nane na nusu? Kama hatuna mkataba huo basi vituo vyetu vya afya na zahanati vifanye kazi masaa 24 ili wananchi wetu waweze kupata huduma bora na huduma ambazo zimekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kuizungumzia Hospitali yetu ya Rufaa ya Bombo. Bombo ni hospitali kongwe nchini Tanzania ambayo ilijengwa na wakoloni na ilikuwa hospitali iliyokamilika idara zote katika wodi na vifaa tiba; vile vile hata katika miundombinu ya lifti. Huu ni takribani mwaka wa nne Bombo hatuna lifti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri, najua nilifika kwake nikamweleza kwamba kuna utafiti mdogo nilioufanya katika kampuni ya lifti inayoitwa OTC ya Ufaransa wameeleza kwamba ili tupate lifti mpya za kisasa wanahitaji Euro 126,000 ambazo ni takribani shilingi za kitanzania milioni mia nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua, kama Serikali itaamua kwa dhati tutaweza kuzipata milioni mia nne kama tulivyoweza kupata fedha za kununulia ndege na mambo mengine. Kwa hiyo, naomba kupitia Bunge hili Mheshimiwa Ummy hata kwa kutafuta wafadhili tuwe tayari kushirikiana lakini tuipate lifti ya Bombo, Tanga. Wananchi wanapata shida, wagonjwa wanaangushwa; mtu anatoka operation amebebwa na baunsa. Kuna utaratibu pale, kuna mabaunsa wako special, mtu akitoka operation kupandishwa ghorofani huko lazima abebwe na mabaunsa familia ilipe. Sasa hii ni aibu kwa nchi yenye rasilimali kama Tanzania kukosa lifti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia, Tanga pia kuna ukosefu wa vitu kama CT Scan. Hospitali ya Rufaa ya Bombo haina vifaa hivyo; lakini kuna taarifa kwamba Watanzania wenzetu wenye asili ya kiasia, Mabohora wametoa mashine ya MRI kama sikosei na CT-Scan, lakini Serikali imeshindwa kujenga jengo la kufitisha mitambo hii. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri na Serikali, tusingoje mpaka wale Mabohora Watanzania wenye asili ya Kiasia wakaamua vinginevyo, mashine ile ikapelekwa mji mwingine. Tunaomba mashine ile Serikali iweze kujenga jengo pale ili tuweze kupata faida ya kutumia mashine ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kusema pia, nchi za wenzetu kama Kenya wameondoa ushuru katika mashine kama hizo za MRI, CT Scan, Ultra Sound na nyinginezo, hali inayopelekea hiyo huduma gharama yake kuwa ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitoa mfano mwaka jana na leo nautoa tena. Yupo mtu mmoja wa Tanga alikuwa na mke wake mgonjwa, alimpeleka Dar es Salaam kupata vipimo hivyo na aliambiwa ni laki nane. Jamaa yake wa Kenya alimwita, na alipofika Mombasa ikawa gharama ni sh 12,000 za Kenya, sawasawa na Sh.60,000/= za kitanzania. Kwa hiyo Serikali iondoe kodi katika vifaa tiba hivi kama MRI, CT Scan na nyinginezo ili gharama za matibabu ziwe nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi Madaktari Bingwa wa mifupa na vichwa kwa Tanga bado tuna tatizo kubwa. Kama tunavyojua kwamba watumiaji wa boda boda na vyombo vya usafiri wa miguu miwili ni wengi na kwa hiyo ajali ni nyingi. Anapoumia mtu lazima akimbizwe MOI Dar es Salaam au apelekwe KCMC Moshi na kwa sababu hiyo gharama zinakuwa kubwa. Hata hivyo, kama Serikali kupitia Wizara ya Afya itatuletea Madaktari Bingwa wa mifupa na vichwa pamoja na magonjwa ya akinamama tutaweza kuhudumia watu wetu pale Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu taulo za akinamama. Nilizungumza juzi kwamba juzi Rais Uhuru Kenyata alisaini sheria kwamba Serikali ya Kenya itawapatia bure taulo za kike wanafunzi wote wa Kenya. Sasa nikitazama Kenya hawana rasilimali nyingi kama Tanzania, wao waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini? Kama tumeweza kununua Bombadier tunawezaje kushindwa kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wetu nchini Tanzania? Mheshimiwa Waziri naomba hili ulifanyie kazi, ikibidi na sisi Tanzania isainiwe sheria kwamba wanafunzi wote wa kike wapewe taulo za kike free, no charge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni wenzetu hawa wa Tanzania ambao wana upungufu wa akili au vichaa. Hawa nao katika maendeleo ya jamii ni jamii ya Watanzania, wao wananufaika vipi na pato la Taifa? Nashauri Serikali itenge fedha na kuipeleka katika kila halmashauri ili wenzetu hawa ambao wana upungufu wa akili waweze kusaidiwa. Leo mtu mzima mwenye upungufu wa akili anatembea uchi wa nyama bus stand, sokoni na watu hawajali, huu ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)