Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye bajeti hii. Kwanza kabisa napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Ummy Mwalimu; Naibu Waziri, Dkt. Faustine Ndugulile; Katibu Mkuu, Dkt. Mpoki kwa hotuba nzuri ya bajeti, lakini vile vile kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii na katika sekta ya afya, kwa kweli nafasi walizopewa wanazitendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuonesha nia ya dhati ya kuiendeleza na kuiboresha sekta ya afya lakini pamoja na kazi zingine nzuri anazoendelea kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kupongeza kwa sababu kuna mambo makubwa yamefanyika katika Wizara hii. Kwanza, tumesikia hapa wanavyotuambia kwamba sasa hivi wanatoa chanjo dhidi ya kirusi cha papilloma (papillomavirus) ambacho kinasababisha saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana wa miaka 14. Hiki kitu kilikuwa hakijawahi kutokea Tanzania hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nakumbuka mwaka jana kulikuwa na makelele mengi na hasa mwaka juzi, juu ya kwamba hakuna dawa. Sasa hivi upatikanaji wa dawa umepanda mpaka asilimia 80 hadi asilimia 90, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa kusambaza ambulance nyingi katika vituo vingi kuliko miaka mingine yoyote ile. Nipende kuwapongeza sana Muhimbili, nampongeza Mkurugenzi wa Muhimbili, Dkt. Maseru kwa kazi nzuri ameirudisha Muhimbili kwenye chart, watu walikuwa wameshaikimbia, sasa hivi huduma zimekuwa nzuri kila mtu anataka kuja kutibiwa Muhimbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza watu wa MOI, Mkurugenzi wa MOI pamoja na watalaam wake wote. Sasa hivi wanafanya operation za magoti, za nyonga, lakini vile vile wameweza kufanya operation ya mgongo kwa njia ya matundu (laparoscopy) kwa mara ya kwanza ndani ya Tanzania, hongereni sana kumbe wataalam wetu wanaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumpongeza Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo, Profesa Janabi kwa kazi kubwa sana ambayo anaifanya. Tunakumbuka watoto wengi walikuwa wanapelekwa nje ili kuzibwa matundu yaliyo kwenye moyo, wao wanafanya sasa hivi. Betri maalum pacemaker zinawekwa kwenye moyo. Wameweza kufanya upasuaji wa mishipa kwa kutumia lazer, nilikuwa naisoma kwenye vitabu kumbe sasa hivi inafanyika Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile wameweza kufanya upasuaji wa moyo wakapandikiza mishipa bila kusimamisha moyo, kwa kweli wanastahili heko, hongereni sana. Mwisho wameweza kupandikiza hata na figo, kwa kufanya hivyo wameokoa pesa nyingi za kitanzania ambazo tungeweza kutumia kwa kwenda kutibiwa nje. Nipende kumkumbusha Mheshimiwa Waziri, kwamba watu wanaofanya vizuri namna hii haiwezekani bajeti yao ikapungua; sasa naomba waongezewe bajeti, waongezewe fedha, kusudi waweze kufanya makubwa zaidi ya hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mazuri yanayofanyika lakini bado kuna upungufu mkubwa wa watumishi na nafikiri huu umesababishwa kwa sababu utoaji wa huduma za afya umepanuka. Tumeongezea vituo vya afya, tumeongeza zahanati, tumeongeza hospitali, obviously lazima watumishi wapungue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa kwa kuwa kuna upungufu ni kilio cha kila mtu Serikali waliangalie kwa jicho la zaidi, kwa sababu hata kwenye hospitali tunazoziita hospitali maalum kama ya Benjamin Mkapa ambayo ina vifaa vingi vizuri vya kila aina lakini bado kuna upungufu wa watumishi. Ukienda kwenye hospitali za Kanda kama Bugando nayo unakuta kuna upungufu wa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Bugando ni Hospitali ya Rufaa kwa Kanda ya Ziwa. Mikoa yoyote ya kanda ya ziwa tunategemea Bugando. Tunawashukuru kwa kutuletea hata kituo cha kansa pale. Hata hivyo ukienda hasa upande wa chemotherapy unakuta kwamba hakuna wataalam. Tunaomba aidha wawapelekee wataalam wa kutosha au wale waliopo basi waweze kuwa-train kusudi watu wanaotoka Kanda ya Ziwa waweze kupata huduma za afya zilizoboreka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Mkoa wa Kagera kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya. Kati ya watumishi 6,245 wanaohitajika tuna 2,575 tu; kwa kweli ni upungufu mkubwa sana. Hata ukiangalia kitaifa upungufu wa watumishi ni asilimia 48; hii ni hatari kwa sababu pamoja na kupeleka dawa; tunasema dawa ziko kule kwa asilimia mpaka 90 kama hakuna daktari wa kuandika, hakuna muuguzi wa kuitoa hiyo dawa, kwa hiyo ina maana kwamba tutakuwa tumefanya kazi bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tusije tukaharibu kazi nzuri tunayofanya basi naomba, kwa kuwa tunajua wapo Madaktari wengi mitaani ambao tayari wako trained lakini hawajaajiriwa na kwa kuwa juzi Mheshimiwa Mkuchika ametutangazia kwamba sasa kuna mafuriko ya ajira. Ajira zaidi ya elfu arobaini zitatolewa, tunaomba vibali vitolewe vingi kwa ajili ya sekta ya afya ili watu wetu waweze kunanii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile niwaombe waendelee kuwa-train wale Madaktari Bingwa ili waweze kutoa tabibu za kibingwa katika hospitali zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera uko pembezoni…

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Bukoba ina Wataalam watatu tu, wa meno, akinamama na mama wajawazito. Hata hivyo, kama mtu ni mahututi lazima akimbizwe kwenda mpaka Bugando Mwanza. Anatumia masaa nane mpaka 10 wakati ambulance waliyokuwa nayo ni mbovu, spare hamna. Mheshimiwa Ummy nimeshampelekea hilo tatizo, Mheshimiwa Waziri Mkuu nilishamwambia, naomba kujua je, katika hii bajeti wataweza kutupatia hii ambulance kusudi tuweze kuondoa hizo kero. (Makofi/vicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera unahitaji hospitali nane za wilaya lakini tunazo mbili tu, kwa hiyo tulikuwa tunaomba, kwa sababu sasa hivi kila mtu anataka kwenda kutibiwa kwenye Hospitali ya Serikali.; tunaomba sasa tupatiwe Hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Biharamulo, Hospitali ya Bukoba Vijijini, Hospitali ya Karagwe, Hospitali ya Wilaya ya Kyerwa, Hospitali ya Wilaya ya Missenyi na Hospitali ya Wilaya ya Muleba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kutoa hela za kukarabati vituo ambapo walikuwa wanatoa kati ya milioni mia nne mpaka mia tano. Kwa bahati mbaya Manispaa ya Bukoba hawajapata fedha hizo. Tunaomba na Manispaa ya Bukoba waweze kupatiwa hizo fedha milioni mia nne mpaka mia tano ili waweze kukarabati hivyo vituo vya afya na hii itawasaidia kutoa huduma bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni bima ya afya. Bima ya afya ni muhimu sana ndugu zangu. Matibabu ni gharama mpende msipende, kuna siku utaugua huna hata senti tano ndani ya nyumba, lakini unaweza kwenda hospitali wakakwambia vipimo vinaenda mpaka laki nne mpaka laki tano. Unaweza ukaambiwa kuna operation ambapo inaenda mpaka milioni, huna hata senti tano utafanyaje. Kama tungekuwa kwenye mfumo wa bima ina maana tunabebana mchango wako, mchango wa huyu unampeleka yule na wewe ikiwa zamu yako unapelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia watu walio kwenye mfumo wa bima ya afya sasa hivi ni asilimia 32 tu, kwa hiyo napendekeza kwamba sasa Wizara ya Afya mfanye mtakachoweza kufanya, mfanye uhamasishaji mkubwa huko vijijini watu wengi waweze kujua umuhimu wa bima ya afya kama walivyosema kwamba wanaleta universal health coverage; kusudi kila mtu aweze kuingia kwenye mfumo wa afya na tuweze kutoa afya bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naendelea kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.