Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niungane na wenzangu kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Kwa kuwa leo nina dakika tano, nitaenda kwa haraka kama ifuatavyo; Mungu anisaidie niweze kuzitumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwanza naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunipa afya. Namshukuru yeye kwa sababu bila yeye nisingeweza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa uthubutu wake na kwa dhamira yake na kuhakikisha sekta ya afya inakwenda kuleta tija kwa wananchi kwa kuhakikisha anapeleka fedha za dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika nchi yetu ni 5% zinakwenda kwa wananchi. Kwa utayari wake sasa, Mheshimiwa Rais wetu anaboresha vituo vya afya, hospitali za wilaya na hospitali za rufaa. Nani kama Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema ni kwamba awasamehe ambao hawajui watendalo, kwa sababu waswahili wanasema, akutukanaye hakuchagulii tusi. Ukiwa kwenye maji unaoga, akija mwendawazimu, humfukuzi. Hata waliosema kuna fedha zilipotea na wenyewe pia awasamehe kwa sababu leo ufafanuzi umetolewa mzuri na ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya utangulizi huo, namshukuru sana Waziri na timu yake. Mwenyewe Mheshimiwa Ummy na Katibu Mkuu. Kusema kweli unapoona mambo mazuri, ujue kuna Watendaji na viongozi wazuri. Taarifa imeandaliwa vizuri na kazi inaendelea vizuri, hongera sana. Endeleeni kuchapa kazi, nchi yetu iweze kufika pale tunapohitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na Mheshimiwa Agness Marwa kuleta shukrani za wananchi wa Mkoa wa Mara kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Mwalimu Nyerere Memorial Centre. Hospitali hii kwa muda mrefu tangu ukoloni imejengwa kwa nguvu za wananchi. Wananchi wa Mkoa wa Mara walichanga fedha nyingi na kilikuwa ni kilio cha muda mrefu. Kwa uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, sasa hospitali inajengwa na fedha zinakuja. Tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokiomba sasa aendelee kutenga fedha, mahesabu yameshafanyika, zinahitajika shilingi bilioni 24. Fedha zipelekwe ili Hospitali ya Rufaa Memorial kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Mara iweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivyo kwa sababu katika Kanda ya Ziwa Hospitali ya Bugando imelemewa. Hospitali ya Bugando inahudumia mikoa zaidi ya tisa. Population ya watu kwa mujibu wa sensa ni watu zaidi ya shilingi milioni 15 ni pamoja na Kanda ya Magharibi. Hospitali ya Bugando inapokea watu wa ugonjwa wa kansa. Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika Kanda ya Ziwa ndiyo watu wanaathirika sana. Hospitali ya Bugando kwa siku inapokea wagonjwa zaidi ya 50 kwa siku wanaokuja kwa ajili ya mionzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Bugando haina hospitali hata ya kulaza wagonjwa wa kansa. Pamoja na kuishukuru Serikali kwa kuboresha Hospitali yetu ya Bugando ambayo inahudumia wananchi wa Kanda ya Ziwa wakiwemo na wa Magharibi na hata wa nje ya nchi, ninaomba sasa fedha zipelekwe ili hiki kituo cha kulaza wagonjwa wa kansa kiweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naishukuru sana Serikali kwa kupeleka fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya afya hapa nchini. Ni ukweli usiopingika kwamba kazi imefanyika vizuri, ushauri wangu sasa, katika bajeti inayoendelea na itakayokuja baadae, ninatoa ushauri kwa sababu nimekuwa nikitembea nchi nzima, ninaomba muwe mnaangalia na maeneo ya pembezoni. Mfano, Wilaya ya Nyasa, Wilaya mpya, ina kituo kimoja cha afya cha Serikali. Wananchi wote wanahudumiwa pale. Hospitali ile haina hata gari la kubeba wagonjwa na vilevile Wilaya ya Nyasa haina hata barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mtakapokuwa mkipeleka magari ya kubebea wagonjwa na hata kupeleka vipaumbele vya hizi fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali za Wilaya, na Vituo vya Afya, angalieni hapa ikiwemo na Musoma Vijijini imekuwa ni Wilaya ambayo imekuwa inaitii sana Serikali. Tumejenga shule nyingi kwa nguvu za wananchi, kuanzia msingi mpaka lenta; kila kata tumejenga. Sasa kwenye wilaya kama hizi ambazo tulijielekeza kwenye elimu, nilikuwa naomba na kwenye vituo vya afya, hebu angalieni na Musoma Vijijini. Tuna Kituo kimoja cha Mlangi ambacho kinahudumia kama Wilaya nzima ya Halmashauri ya Musoma. Musoma ina Hospitali ya Rufaa, lakini population ya watu wamekuwa ni wengi, haiwezi kuhudumia katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie upungufu wa wataalam katika sekta ya afya. Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa, hali ni mbaya. Madaktari hasa mabingwa hakuna, hata huko Bugando kuna upungufu mkubwa sana. Hata Hospitali ya Mkoa wa Mara tuna madaktari wawili tu. Siyo Mara peke yake kwa sababu, mimi Jimbo langu ni Tanzania nzima. Katika hospitali zote nilizozitembelea na hata Vwawa juzi nilikuwa Mbozi, hali ni mbaya. Tunaomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya kuwapeleka wataalam katika hospitali zetu na hasa Madaktari Bingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitoe ushauri, nendeni mkaongee na Watanzania walioko Botswana. Mimi nilishaanza kufanya nao mazungumzo; wako tayari kurudi nyumbani kwa manufaa ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, muda ni mfupi, naomba kuunga mkono na mambo mengine nitayaleta kwa maandishi. (Makofi)

Mhesimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.