Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia uzima na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako tukufu. Naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kuifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka na yenye tija. (Makofi)

Pili, nampongeza sana Waziri wa Afya na timu yake kwa juhudi kubwa wanayofanya kuboresha huduma za afya na upatikanaji wa dawa ambapo hapo awali ilikuwa ni changamoto kubwa na kero kubwa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na bajeti iliyowasilishwa mbele ya Bunge lako tukufu, bado kuna changamoto kubwa eneo la afya la mama na mtoto. Takwimu zinaonesha kwa mwaka 2004/2005 vifo vya mama wajawazito vilikuwa 578 kati ya vizazi hai 100,000; mwaka 2009/2010 vilishuka na kufikia 434 kati ya vizazi hai 100,000; lakini mwaka 2015/2016 vifo vya akina mama wajawazito vilipanda hadi kufikia 556 kutoka vizazi hai 100,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu hizi, bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kupunguza vifo vya wakina mama wajawazito. Ikumbukwe kwamba tulijiwekea malengo ifikapo mwaka 2020 tuwe tumepunguza vifo hivi viwe vimefikia 292 katika vizazi hai 100,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iongeze nguvu katika kuajiri wataalam hasa katika Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto lakini pia katika kada zote za afya, kwani kwa Mkoa wetu wa Singida tuna uhaba mkubwa sana wa watumishi katika kada ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuajiri wataalam hao, tuende sambamba na kuleta vifaa tiba katika wodi zetu za wazazi, kwani vilivyopo ni chakavu na havitoshelezi mahitaji. Katika Mkoa wa Singida jiografia yake ni ngumu sana na inahitaji ambulance nyingi za kutosha ili kuepuka vifo vya akina mama na watoto na kuwafikia haraka sehemu za kutolea huduma kwa wakati. Inasikitisha sana, baadhi ya Hospitali za Wilaya na Vituo vya Afya vya Ikungi, Manyoni na Itigi havina kabisa magari ya kubebea wagonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutarajie nini kwa mama ambaye tayari ameshashikwa na uchungu wakati hakuna usafiri wa kumfikisha katika kituo cha kutolea huduma? Mheshimiwa Ummy dada yangu mpendwa najua wewe ni msikivu na ni mama wa wanawake wanyonge na suala hili nimekuwa nikikuletea mara kwa mara kwamba Hospitali yetu ya Mkoa wa Singida haina kabisa gari ya kubebea wagonjwa, hivyo nakuomba unisaidie ili tuweze kupata magari ya kubebea wagonjwa na pia tuweze kusaidia kuokoa vifo vya akina mama wajawazito na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida. Hospitali hii imejengwa takribani miaka kumi iliyopita, lakini mpaka sasa haitoi huduma. Vitengo vinavyotoa huduma ni vitengo vitatu tu; Kliniki ya Uzazi na Mtoto, Kliniki ya Ngozi na Kliniki ya Wagonjwa wa Kisukari. Sasa inawezekana vipi hospitali yenye hadhi ya kuitwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa iweze kuhudumia vitengo vitatu tu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana hata baadhi ya majengo yameshaanza kuchakaa. Sasa ni kwa nini Serikali haitoi fedha za kutosha ili Hospitali hii ya Rufaa iweze kukamilika na kuanza kutoa huduma na hata hatimaye kupunguza msongamano katika hospitali zetu za Wilaya na vituo vyetu vya afya? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba wakati Waziri wa Afya atakapokuja kufanya majumuisho, anipe commitment ya Serikali ni lini Hospitali hii ya Rufaa itakamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hospitali yetu ya mkoa haina Madaktari Bingwa wa kutosha; madaktari waliopo ni sita tu, wakati ikama inahitaji kuwa na madaktari 33. Naomba Serikali iwaonee huruma…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na mengine nitayaleta kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.