Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngara
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Afya. Niungane na Wabunge waliotangulia kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, lakini pia kazi kubwa wanayoifanya Waziri na Naibu Waziri na watendaji wao wa Wizara katika kuboresha afya za Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi yamefanyika katika Jimbo langu la Ngara hasa katika kuboresha afya za wananchi wa Ngara ikiwa ni pamoja na kuboresha vituo vya afya Musagamba Mabawe, lakini pia hata upatikanaji wa dawa kabla ya hapo wananchi wa Jimbo la Ngara walikuwa wanaenda kutibiwa Burundi haya wa kata za mipakani lakini leo imekuwa ni vice versa kwamba kuna wanaotoka upande mwingine kutaka kuja kupata huduma upande wetu. Kwa hiyo, napongeza Serikali na Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo bado zipo changamoto, tuna vituo vinne katika Wilaya ya Ngara kati ya kata 22, lakini kipo Kituo cha Afya Lukole ambacho kituo hiki ni miongoni mwa hivyo vituo vinne. Hiki kituo kilikuwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Lukole wakati wakiwepo wakimbizi wa Burundi, majengo yaliyojengwa katika kituo kile ni majengo ambayo mengi yalijengwa kwa tofali za tope kwa hiyo siyo majengo ya kudumu lakini ni kituo ambacho kinahudumia watu zaidi ya elfu ishirini na tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Mheshimiwa Waziri Ummy, Naibu Waziri Dkt. Ndugulile mmefanya kazi kubwa kwangu, lakini niombe hili nalo tuliangalie kwa macho mawili kwamba hiki kituo nacho tuweze kukiboresha ili kiwe kwenye hadhi kwa sababu kinatoa huduma ka wananchi wa Jimbo la Ngara hata Jimbo jirani la Bihalamuro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa watumishi upo kwa kiasi kikubwa kwenye sekta hii ya afya, kuanzia kwenye hospitali ya Nyamiaga, vituo hivyo vinne na kwenye zahanati. Niombe kwamba sasa kwa watumishi hawa ambao wanaenda kuajiriwa, watumishi 16,000 kwenye bajeti ya mwaka huu, idara ya afya basi mtufikirie.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado pia kuna baadhi ya watumishi waathirika hususan katika Hospitali ya Murugwanza, Dada yangu jana aliiongelea na mimi nalisisitiza hili kwa sababu wapo watumishi 49 ambao wakati wa uhakiki wa vyeti siyo makosa yao, waliondolewa kwenye payroll wakati hawakuwa na kosa na bado wakarudishwa. Wengine wanadai miezi kumi, wengine wanadai arrears za mishahara yao miezi sita, saba kwa namna tofauti, niombe hilo liweze kushughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono mpango wa bima ya afya kwa watu wote, hii inaweza kuwa ndiyo suluhisho kwa ajili ya kuondoa double standard na kuwahudumia watu kwa usawa. Ni nia njema ya Serikali na niombe hili lifanyiwe haraka na Wabunge tupo tayari kwa ajili ya kuendelea kuhamasisha ili mpango huu uanze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipo Kituo cha Afya katika Kata ya Nyakisasa, kituo hiki kilianzishwa kwa nguvu za wananchi, lakini pia kwa kutumia Mfuko wa Jimbo; yapo majengo ambayo ambayo hayajaweza kutosheleza kuwa kituo cha afya, lakini tunaamini ikiwekwa nguvu kidogo kituo kile kinaweza kikafunguliwa kulingana na jiografia ya hali ya Ngara, kituo hiki ni muhimu na tunakihitaji. Niombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja ulifikirie hilo katika vituo ambavyo unaweza ukaviongezea fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwenye upande wa lishe. Lishe katika hali ya kawaida inaonesha kwa mujibu wa takwimu kwamba Tanzania tuna lishe duni ni watatu Afrika, lakini ni wa kumi duniani, unaweza ukaona ni jinsi gani ambavyo kuna changamoto hiyo. Pamoja na kwamba Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) wameonesha ni jinsi gani ambavyo wamefanya jitihada katika ku-control hata vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinavyotokana na udumavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kwamba twende zaidi tujaribu kushirikiana hata na Wizara ya Kilimo kuona ni namna gani tunavyoweza kuhamasisha baadhi ya mazao ambayo yanaongeza lishe. Kwenye ukurasa ule wa 89 kwenye kitabu hiki cha hotuba ya Waziri wameonesha ni jinsi gani ambavyo wanajaribu kutoa chanjo kwa asilimia kubwa kwa watoto chini ya miaka mitano kwa matone ya Vitamini A.
Mheshimiwa Naibu Spika, vipo vyakula lishe kama viazi lishe ambavyo vina Vitamini A nyingi ya kutosha ambavyo tukihamasisha ulimaji wa viazi lishe (orange sweet potato) vinaweza vika-cover eneo ambalo tunatumia gharama kubwa kwa ajili kuwachanja watoto hawa kwa matone ya Vitamini A. (Makofi)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia.