Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MOHAMED R. CHUACHUA: Mheshimiwa Nabu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii ya mimi kuchangia angalau dakika tano. Nataka niseme tu kwamba naipongeza sana Serikali, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake inayoonesha kwamba tumepiga maendeleo makubwa sana katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo ningependa kuzungumza ni kuishukuru tena pia Serikali kwa kunipatia uhakika wa kupata fedha kwa ajili ya kujenga kituo kimoja cha afya cha miongoni mwa kata zangu, kwangu mimi hili ni jambo kubwa sana katika kuboresha afya za wananchi wetu wa Masasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee pia suala la Hospitali ya Kanda ya Rufaa. Ni muda mrefu sasa Serikali imekuwa ikizungumza na ikiwa na utaratibu wa kutaka kujenga Hospitali ya Kanda ya Rufaa katika Mkoa wa Mtwara, lakini kwa bahati mbaya sana jambo hili linakwenda taratibu mno. Tunasikia kwamba NHIF wamepewa dhamana ya kutaka kumalizia hospitali hiyo, lakini mpaka sasa hatujui kwa sababu hatuoni kinachofanyika. Tungependa kusikia kauli ya Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja yake, ni kwa vipi wamejipanga kukamilisha Hospitali hii ya Kanda ambayo itakuwa inahudumia mikoa ya Ruvuma, Lindi pamoja na Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini nizungumze kidogo kuhusu suala la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Wabunge wa Mtwara wamezungumza jambo hili na sisi katika jambo hili ni wa moja sana nataka kusema miongoni mwa mambo ambayo ni magumu na ni mazito sana kwetu kuyatolea maelezo ni hali ya hospitali yetu ya mkoa. Hospitali hii ina hali mbaya sana kwa upande wa watumishi natoa tu mfano; kwa mfano tunatakiwa na Madaktari Bingwa 24 lakini tunao Madaktari Bingwa wawili tu, tunatakiwa tuwe na madaktari wa kawaida 30 tunao saba, Madaktari Masaidizi (AMO Assintant Medical Officers) tunatakiwa tuwe nao 23 tunao wanane tu, nursing officer wanatakiwa wawe 37 tunao wanne.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu wa ma-nurse wengi kwa sababu wanatakiwa wawe 131 tunao 44 tu. Hali ya hospitali hii ni mbaya na inajhitaji jicho la kipekee la Serikali ili kuhakikisha kwamba hospitali hii inaimarishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatukuishia hapo tu katika changamoto za hospitali hii kuna miundombinu chakavu sana. Tuna matatizo ya vifaa tiba, kwa mfano tunayo x-ray zeefu na ni ya kizamani sana na inaharibika mara kwa mara, tungependa Serikali sasa itupatie digital x-ray ili tuweze kutoa huduma kwa wananchi wetu kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifika katika chumba cha upasuaji hata mashine ile ya kuchemshia vifaa nayo imezeeka sana, lakini pia inaharibika mara kwa mara na inakwamisha sana shughuli za hospitali. Mashine ya kufulia nguo pamoja na mashuka ya wagonjwa ni mbovu na imezeeka sana, tungependa Serikali iangalie mambo haya. Kwa bahati mbaya sana tunalo gari moja tu la kusadfirisha wagonjwa na gari hilo nalo limezeeka sana, tunasikia kwamba Serikali ina mpango wa kutenga fedha kwa ajili ya kununua gari lingeni la wagonjwa yaani ambulance, tungependa Serikali ikamilishe jambo hili haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Mji wangu wa Masasi hatujapata bado fedha kiasi fulani cha fedha katika mfuko wa afya. Tulitengewa shilingi milioni 187 tumepata shilingi milioni 76 tu. Tunaimani Serikali sasa inapaswa kuhakikisha kwamba fedha hizi zinakwenda haraka iwezekananvyo ili tuweze kupata nasi fursa ya kununua dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze kidogo kuhusu huduma ya tumaini la mama; hii ni huduma nzuri na naipongeza sana Serikali kwa hatua iliyofikia. Hata hivyo nataka niseme kitu kimoja tu, kabla Serikali haijaanza jambo hili katika jimbo langu mimi nilikuwa natumia mfuko wa jimbo kununua package hizi kwa ajili ya akina mama kujifungulia. Hata hivyo hata baada ya Serikali kuanzisha utaratibu huu bado ninalazimika kutenga baadhi ya fedha kutoka kwenye mfuko wa jimbo kwa ajili ya kununua vifaa vya akina mama kujifungulia kwa sababu huduma ya tumaini la mama haitoi vifaaa vyote tunaomba sasa Serikali kwa sababu huu ni mpangao ambao umeamua kuianzisha kwanza mpango huu uwe endelevu, lakini pili u-accommodate vifaa vyote ambavyo vinahitajika kwa ajili ya akina mama.