Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la ukarabati wa zahanati na vituo vya afya. Ni jambo zuri la Serikali kujenga zahanati kila kijiji na vituo vya afya kila kata. Lakini vipo vituo vilivyopo ambavyo ni chakavu na havina wahudumu wa afya na vifaa. Ushauri, Serikali ingeviimarisha vile vilivyopo kwanza na kuhakikisha kuna vifaa, madaktari na manesi na dawa na hii kwa kiasi kikubwa itapunguza sana msongamano kwenye ngazi za juu Wilaya hadi Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu magonjwa yasiyoambukiza (NCD), pamekuwa na ongezeko kubwa sana la magonjwa yasiyoambukiza kama ugonjwa wa sukari ya kupanda na kushuka, shinikizo la damu ya kupanda na kushuka, magonjwa ya moyo na kadhalika. Magonjwa haya mengi yanachangiwa zaidi na mtindo wa maisha, vyakula tunavyokula na kutofanya mazoezi ya mwili. Inasemekana karibu asilimia 10 ya wananchi wana uzito uliopitiliza (obesity).
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri, elimu itolewe zaidi na Wizara ishirikiane na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ili barabara zinapojengwa wahakikishe wanajenga pavement ya wapita kwa miguu au kuendesha baiskeli, hili ni zoezi zuri sana. Wafanyakazi badala ya kwenda na magari kazini wanaweza kutembea na pia ofisi zote zinaweza kuwa na chumba cha kufanyia mazoezi kwa kufanyia mazoezi; kwa kufanya hivi Serikali itaokoa kwa kiasi kikubwa fedha kwa ajili ya matibabu. Pia pawepo na vipimo vya kupima sukari na shinikizo la damu kwenye maofisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ugonjwa hauna muda, mama mjamzito akija kujifungua anaweza pata uchungu muda wowote. Sehemu za vijijini wanawake wengi wanapoteza maisha kutokana na umbali wa kufika hospitali ya ngazi za juu. Je, kwa nini zahanati zisifanye kazi kwa muda unaozidi masaa nane? Sababu hizi ndizo zilizopo karibu na wananchi au pawepo na gari (ambulance) masaa 24 itakayosaidia kuwakimbiza wagonjwa kwenye kituo cha afya au ngazi ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upandikizaji wa figo; napenda kuipongeza Serikali kwa jitihada hizi kubwa na kuweza kuwasaidia watu wengi waweze kupata huduma hii ambayo ni ghali sana. Swali langu ni kwmaba kwa kuwa mtu akishapandikizwa figo ni lazima atumie dawa kwa maisha yake yote na dawa hizo ni ghali sana, je, Serikali imejipangaje kuhakikisha wagonjwa hawa watazipata dawa hizo kwa sababu sio kila mgonjwa atakuwa na uwezo wa kununua dawa hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona wagonjwa wengi wanaomba msaada wa matibabu kupitia magazeti, televisheni na wengine wamepewa barua kutoka Ofisi za Serikali kutoka kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mkoa kuwaombea misaada ya matibabu, je, ni jukumu la Serikali kuruhusu wagonjwa hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tatizo la vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi ni kubwa sana hapa nchini na badala ya kupungua vinaongezeka. Kuna haja ya kuliangalia suala hili kwa umuhimu sana na kuhakikisha vifaa na wakunga wanakuwepo wa kutosha; na upungufu wa wataalam naamini unachangia vifo hivi.
Mwisho kabisa niwapongeze Waziri na Naibu Mawaziri wanavyojitahidi katika sekta hii, lakini tukumbuke wote sisi ni wazee wa kesho, kambi za wazee mfano iliyopo Moshi Manispaa (Njoro) ipo katika hali mbaya, malazi sio mazuri hata vyoo vyao sio vizuri. Naomba Serikali iende ikakague kituo hicho ili waweze kuwasaidia wazee.