Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAJMA MURTAZA. GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa jinsi anavyokuwezesha Mheshimiwa Waziri (mwanamke mwenzetu) kufanya kazi zake kwa ujasiri na uweledi unaothibitisha kuwa wanawake tunaweza kabisa.
Mheshimiwa Waziri hoja yangu inajikita moja kwa moja kwenye hotuba yako kwenye ukurasa wa 101 hadi 107 na ukurasa wa 109 hadi 110. Umekiri kabisa kuwa ukatili dhidi ya watoto bado ni tatizo kubwa hapa nchini, na mimi ninakiri pia kwa kauli yako hii. Matukio ya ukatili dhidi ya watoto yameongezeka kwa asilimia 28 kutoka mwaka 2016 hadi kufikia mwaka 2017, ninaamini kabisa elimu sahihi kuhusu vitendo hivi ikiwafikia Watanzania walio wengi na kuweza kutoa taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya watoto, asilimia hii inaweza kuzidi hadi kufikia asilimia 60 au zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sichoki na wala siyachoka kutoa ushauri wa kuangalia adhabu mbadala kwa makatili wazoefu wanaoharibu maisha ya watoto wetu ambao ni Taifa letu la kesho.
Mheshimiwa Waziri inasikitisha sana kuona kuwa haki za binadamu zinapewa kipaumbele kwa hawa makatili wa watoto wetu na hasa wabakaji watoto wa kike na wanaolawiti watoto wakiume, mbali na kutumikia kifungo kwa miaka 30 makatili hawa sugu (ambao wanathibitika kuwa wazoefu katika kuwaharibu watoto wetu) wafikiriwe adhabu mbadala ya kuhasiwa uume wao ili iwe funzo kwa wengine na kuwaokoa watoto wetu kutokana na janga hili ambalo tukizidi kuwaonea huruma kwa kisingizio cha haki za binadamu tutaliangamiza Taifa la kesho kwani hili janga mwisho wa siku litakuwa janga la kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Ibara ya 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza wazi kwamba haki na uhuru wa binadamu ambavyo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii havitatumiwa na mtu mmoja kwa maana ambavyo itasababisha kuingiliana kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma; kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru wa haki za watu bibafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali kuwa ibara hii ya Katiba ikionekana kuvunjwa kwa namna yoyote kwa mujibu wa ibara 30 mtu anaweza kufungua shauri katika Mahakama Kuu. Hili suala la kufungua shauri katika mahakama zetu bado inaonekana siyo muafaka sana kwa maslahi ya watoto wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nakushukuru Mheshimiwa Waziri ukiwa kama mwanamama mwenzangu ulitafakari na kukaa na timu yako kutafakari zaidi suala la kuleta muswada wa sheria ya kuwahasi wabakaji sugu wa watoto wa kiume na wa kike, tukizingatia ibara hizo hapo juu za Katiba yetu zinaturuhusu kutunga sheria katika jambo la aina hii, tuache kabisa kisingizio cha kuvunja haki za binadamu wakati hawa wabakaji wanaendelea kuvunja haki za binadamu wadogo.
Naomba sana Wizara yako ijaribu kutafiti na kuona uwezekano wa kutungwa sheria hii ya adhabu ya kuhasi kwa kulinganisha na nchi nyingine ambazo tayari zina hukumu za aina hii. Mfano Mheshimiwa Mary Karooro Okurut, Waziri wa Jinsia Kazi na Maendeleo wa Uganda anaunga mkono suala hili la kuwahasi wabakaji hawa.
Mheshimwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.