Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi niwe mchangiaji wa kwanza kwenye Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wa Ta’ala ambaye ameweza kunipa afya njema na leo hii niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ili tuweze na sisi kunufaika na rasilimali za Tanzania hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja suala hili; hotuba ya Mheshimiwa Waziri imezungumza kwa kiasi kikubwa sana ujenzi wa barabara, na nichukue fursa hii kushukuru na kuishukuru Wizara kwa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa Barabara ya Uchumi ambayo inajengwa kuanzia Mtwara Mjini mpaka Mnivata kule kwenye Jimbo la Nanyamba na baadaye itafika mpaka Masasi. Nichukue fursa hii kuishukuru Wizara kwa kuanza kutekeleza kilometa hizi 50 kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nizungumze kwamba wakati barabara hii inazinduliwa na Mheshimiwa Rais alivyokuja Mtwara mwaka jana kuja kuzindua ujenzi wa barabara hii na miundombinu mingine, alitoa wasiwasi wake juu ya mkandarasi ambaye amepewa ujenzi wa barabara hii; kwamba kuna wakati fulani akiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi aliwahi kumsimamisha kazi, akawa amemuagiza Mheshimiwa Profesa Mbarawa kwamba awe makini sana; pale Mtwara tukiwa bandarini tunazindua ujenzi wa lile gati, na akasema kwamba atakuwa makini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nisikitike tu, yule mkandarasi bado yuko slow sana. Nimuombe Waziri, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, akaze buti huyu mkandarasi aendane na kasi ya ujenzi lakini pia aendane na muda ambao umewekwa; yuko slow sana yule mkandarasi anayejenga barabara ya Uchumi kutoka Mtwara Mjini mpaka Mnivata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze suala zima la barabara ya ulinzi; tulikuwa tumezungumza hapa kwa muda wa miaka miwili na huu ni mwaka wa tatu hivi sasa, kwamba kuna barabara ya ulinzi ambayo ilitumika kulinda mpaka wetu wa kusini, barabara inayoanzia Mtwara Mjini, inapita Jimbo la Mtwara Vijijini, inafika kule Kitaya Jimbo la Nanyamba, inafika Tandahimba, Newala mpaka kule Ruvuma. Hii ni barabara muhimu sana, ni barabara ambayo makamanda wetu walikuwa wanaitumia kumdhibiti Mreno ambaye alikuwa anakuja kutuchokoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwaka 1972 ndege ya Mreno ambayo ilikuja kuvamia Tanzania iliweza kudunguliwa Kijiji cha Kitaya pale Jimbo la Nanyamba, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini. Lakini baada ya kuidondosha ile ndege ya Mreno yule kamanda wetu aliuawa pale, pamejengwa mnara mdogo sana. Mimi naomba sana na naishauri Wizara hii, hii barabara ijengwe na pale pajengwe mnara wa kumbukumbu ambao utaonesha kweli kwamba shujaa wetu pale Kijiji cha Kitaya ndipo alipouawa akiwa analinda mpaka wa Tanzania ambao uko huku maeneo ya kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii imekuwa ikizungumza sana, imekuwa ikiongea sana kwamba tutatenga bajeti, niombe sana kwamba mwaka huu barabara hii ya ulinzi ambayo inalinda mpaka wa kusini itengewe pesa ili iweze kuanza kutengenezwa, kwa sababu hatuwezi jua huko mbeleni kwamba kitu gani kinakuja juu ya mipaka yetu ya Tanzania. Mpaka huu ni mpaka muhimu sana, barabara hii ni barabara muhimu sana, inaanzia Mtwara mpaka Ruvuma kule. Ninaomba sana Wizara iangalie kwa jicho la kipekee mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili ambalo tumekuwa tunazungumza la maendeleo ya Ukanda wa Kusini (Southern Development Corridor) ambalo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu hivi sasa na maendeleo ya Ukanda wa Kusini inaanzia katika ujenzi wa bandari. Tunashukuru kwamba Gati la Bandari la Mtwara linajengwa kwa mita 350, lakini ujenzi wa gati ya bandari unaendana sambamba na barabara ya reli. Miaka ya 1963 huko Mtwara, kule kusini kulikuwa na reli na ile reli ikaondolewa, hatujui ilipelekwa wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ili kuweza kufungua uchumi wa Kanda ya Kusini kuna ulazima Serikali ihakikishe kwamba huu ujenzi wa reli ambao umekuwa ukizungumzwa kila mwaka kwamba reli inayotoka Mtwara kuelekea Liganga na Mchuchuma kule kupitia kule Mbambabay ni muhimu mwaka huu sasa tuweze kutengewa pesa ile pesa iweze kupelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana ilizungumzwa hapa kwamba imetengwa pesa kwa ajili ya upembuzi yakinifu karibu shilingi bilioni mbili, sijaona upembuzi yakinifu uliofanyika mpaka leo hii. Kwa hiyo tunaomba sana, ili tuweze kufufua uchumi wa kusini (Southern Corridor) ambapo itaunganisha Mikoa ya Kusini – Mtwara, Lindi, Ruvuma lakini kule maeneo ya Malawi na nchi nyingine za Kusini, tujenge hii barabara ya reli ya Ukanda wa Kusini. Itengewe pesa mwaka huu na pesa ziweze kutolewa kwa ajili ya upembuzi yakinifu lakini na ujenzi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la utanuzi wa bandari; lengo la kujenga bandari hizi; Bandari ya Mtwara, Bandari ya Tanga, Bandari ya Mafia, Bandari ya Kilwa ni kuhakikisha ya kwamba tunafanya decentralization of the economy, hatuwezi kutegemea Bandari moja ya Dar es Salaam. Leo hii ukifika Bandari ya Dar es Salaam, mizigo yote ambayo inatakiwa kushuka Tanzania inashukia Bandari ya Dar es Salaam wakati Bandari za Mtwara, Tanga pamoja na Kilwa ni bandari zenye vina virefu, meli ya aina yoyote inaweza ikagati katika maeneo haya. Bandari ya Mtwara Wazungu wanasema ni natural habour, ni bandari ambayo ina kina kirefu kuliko bandari zote za Afrika Mashariki na Kati. Kuna meli nyingine, kama sio ukarabati wa Bandari ya Dar es Salaam, haziwezi kugati Dar es Salaam, lakini Mtwara zinaweza kugati kwa sababu ya kina kirefu cha maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa sana kwamba tunatumia Bandari ya Dar es Salaam tu. Leo hii ukiamua kuagiza gari kutoka Japan/kutoka nje ya nchi, katika East Africa kwa nchi yetu ya Tanzania iko Bandari ya Dar es Salaam pekee na Bandari ya Mombasa, wakati tungeweza kuongeza Bandari za Mtwara na Tanga ili tuweze kuuondoa msongamano Dar es Salaam. Mimi naiomba sana Wizara hii kwamba upanuzi wa bandari ambao tayari gati limeanza kujengwa pale Mtwara, kwanza uweze kukamilika kwa wakati, lijengwe kwa kasi lakini pia tuitumie Bandari ya Mtwara ili kuondoa msongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naamini Bandari ya Mtwara ikitumika sawasawa hii barabara yetu ya Morogoro haitaharibika hivi kwa sababu barabara inayotengenezwa Tanzania kila siku ni barabara ya Morogoro kwa sababu mizigo inakuwa mingi sana. Magari ya Zambia, magari ya Burundi, magari ya Tanzania, on transit zote zinatokea Dar es Salaam. Tupanue Bandari ya Mtwara, tutumie Bandari ya Mtwara ili kuondoa uharibifu wa barabara moja hii ambayo inatengenezwa kila wakati.

Jambo lingine ni suala hili la meli; usafiri wa meli wakati fulani hivi nilitembelea Comoro pale, ukifika Comoro, Comoro ilipigwa volcano, yaani Comoro hata nyanya hazistawi, kila kitu wananunua kutoka nje, wanategemea kutoka Tanzania. Sasa hatuna usafiri wa meli ambapo wafanyabiashara wa Tanzania wangeweza kutokea Mtwara; Mtwara na Comoro karibu sana; wangeweza kutokea Dar es Salaam kwa kutumia meli, wangeweza kutokea Pemba kuelekea Comoro kupeleka mizigo kule na Watanzania tungekuwa na manufaa, wafanyabiashara wetu wangeweza kuinuka kiuchumi kwa usafiri wa meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pale Mtwara tuna Kiwanda cha Dangote ambacho ana magari zaidi ya 1,000 yanayosafirisha cement kutoka Mtwara kuelekea kwenye soko kuu ambako ni huku Dar es Salaam na maeneo mengine. Kama tungeweza kumruhusu huyu Dangote akajenga ile bandari yake ndogo, lakini pia akalazimishwa kununua meli ili simenti yake aweze kusafirisha kwa njia ya meli, barabara hii isingeharibika, angeweza kuleta mzigo wake Dar es Salaam kupitia kwenye Bahari ya Hindi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)