Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Nami nianze pale alipoishia Chifu Kadutu kwanza kumpongeza mtoa hoja wetu, Mheshimiwa Profesa Mbarawa na timu yake yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu mapema tu kwamba Wizara hii imepata bahati ya kupata Mawaziri ambao ni wapole, lakini watendaji sana kuliko kuongea. Naamini wanaitendea haki nafasi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda wenyewe ni mfupi, nitakwenda kwa haraka kidogo, nianze na ujenzi wa gati la Nyamisati. Tunashukuru kwenye kitabu tumeiona humu na mkandarasi ameshafika pale na kama alivyosema kwenye hotuba yake Mheshimiwa Waziri kwamba kazi itaanza mwezi ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wasiwasi wangu ni mdogo tu kwamba anaonekana mkandarasi huyu katika kuji-mobilize pale ameanza kwa kusuasua, anakuja na magari na vifaa vichache sana. Ningeomba aongeze spidi kwa sababu hali ya bandari ya Nyamisati ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni shukurani vilevile tena kwa Serikali angalau kwenye kitabu tumeona kwamba meli ya Nyamisati - Kilindoni sasa inaelekea kujengwa. Tunaishukuru sana Serikali wametenga shilingi bilioni tatu ingawa tunaambiwa itagharimu shilingi bilioni saba, tutamalizia mwakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni mdogo tu kwenye hili. Mheshimiwa Waziri hali ya usafiri baina ya Kilindoni na Nyamisati ni mbaya sana. Tunafahamu nia ya dhati na nia nzuri ya Serikali katika kujenga kivuko hiki kipya lakini kitachukua zaidi ya mwaka mmoja kuwa tayari. Katika kipindi hiki cha mpito, tunaiomba kwa namna ya kipekee kabisa Serikali iangalie namna gani tunaweza tukaishi ndani ya mwaka mmoja na nusu huu tukisubiri kivuko ambacho kinatengenezwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanaweza wakatupatia hata vivuko vya jeshi au sehemu zozote ambazo tayari wana vivuko vya ziada watuletee Mafia angalau tuanze kwa kipindi hiki ambacho kivuko chetu kinatengenezwa tuweze kutumia mpaka hapo kivuko chetu kitakapokuwa tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi ya TEMESA anayoiongoza Mheshimiwa Waziri nashangaa sana, nia yake ya dhati na nia ya Serikali tunaiona lakini inaonekana limekuwa kama ni jeshi la watu watatu katika Wizara hii. Hawa TEMESA ni watu wa aina gani mbona hatuwajui? Jambo hili la kujenga meli kwa ajili ya Mafia tulitarajia watakuja Mafia wakae na wadau tuwaambie aina gani ya chombo ambacho kitatufaa watu wa Mafia kwa sababu kuna changamoto tofauti ya kutoka kwenye bahari na kuingia kwenye mto, kina kinaweza kikawa kinapungua, aina ya cargo, aina gani ya meli itakayotengenezwa, itabeba abiria wangapi, itabeba mizigo tani ngapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kama Waziri anapambana peke yake lakini taasisi yake ya TEMESA haimuungi mkono, hawajafika Mafia, kwa DC, kwa Mbunge wala kwa DED, hatujui hii meli mtaitengeneza katika specification zipi bila ya kuwashirika watu wa Mafia wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata mashaka sana na TEMESA kama kweli wana nia ya dhati ya kusaidia katika jambo hili. Kwa taarifa katika magari yanayotengenezwa pale Wilayani Mafia yamepelekwa TEMESA huu mwaka sasa wa nne, magari yale yako kule, hayajatengenezwa, yalikwenda kule kwa matatizo ya kama Sh.10,000,000 sasa hivi tunaambiwa yanagharimu zaidi ya Sh.40,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magari yale yametushinda yako TEMESA, vifaa vimeibiwa, spare parts zimenyofolewa, tunaambiwa chukueni gari lenu, lipieni gharama za ku- maintain ile gari pale mkatengeneze wenyewe. Kwa hiyo, nina wasiwasi sana na utendaji wa kazi wa hii taasisi ya TEMESA, Mheshimiwa Waziri atupie macho hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu taasisi hii ya SUMATRA. Mafia nadhani ndiyo itakuwa ni Wilaya pekee au eneo pekee katika nchi hii ambapo ukitaka kusafiri kwa boti lazima ufanye booking wiki moja kabla. Kwa sababu wameweka masharti pale ya kupakia mwisho abiria 50 na katika population ya watu karibu 70,000 kusafiri watu 50 kwa siku moja ni changamoto kubwa, watu wako foleni wanasubiri kusafiri zaidi ya wiki. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hili.