Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nishukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais. Kazi kubwa ambazo zinafanyika kwa sasa katika sekta hii ya ujenzi Watanzania wote tunaona. Hakuna ubishi kwamba katika kipindi cha miaka 10 cha Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli tutakuwa na Tanzania tofauti sana na Tanzania ambayo tumekuwa nayo kwa zaidi ya miaka 50 ya uhuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi, nina mambo machache yafuatayo ambayo kimsingi ni maswali tu ambayo nataka Mheshimiwa Waziri au Naibu wake wakati wa kuja kutoa majumuisho anisaidie. Nafahamu na kwenye vitabu nimeona lakini wananchi wanauliza na mimi pia nauliza, mwaka jana kwenye bajeti ya 2017/2018 tulipitisha shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kahama – Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazungumzo ambayo nimekuwa nikiyafanya na Wizara hii toka muda huo ni kwamba baada ya bajeti kuwa imepitishwa kilichokuwa kinafuata ni utaratibu wa kumpata mkandarasi. Leo ni mwezi wa nne, mimi na wananchi hatuna taarifa zozote kuhusu utaratibu wa kumpata mkandarasi wa kujenga barabara ya Kahama - Bulyanhulu - Geita umefikia hatua gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye bajeti ya mwaka huu tumeongeza tena fedha zingine, tumetenga shilingi bilioni 13 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa barabara hiyo, lakini kwa sababu wananchi hawaoni chochote kinachofanyika on the ground inakuwa siyo rahisi kuamini kwamba kweli barabara hii itakwenda kujengwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri atuambie ni nini hasa kilichofikiwa katika ujenzi, kupitisha bajeti hata mwaka jana tulipitisha lakini haitoshi wananchi wanataka kuona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tulikusudia kufanya Kahama iwe makao makuu ya kiuchumi kwa kanda hiyo. Ili kufikia azma hiyo tulisema ni muhimu sana kufungua barabara zinazounganisha Kahama au Shinyanga na maeneo mengine. Kuna barabara kama tatu ambazo zinaunga Kahama na Mkoa wa Mwanza kupitia Jimbo la Msalala ambazo sijaziona zimefikia hatua gani angalau kuanza kufanyiwa upembuzi yakinifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kutoka Kahama - Nywang’wale - Busisi - Sengerema - Mwanza. Nimeona upande wa Mwanza kuna upembuzi yakinifu umeanza kwa ajili ya kutengeneza daraja la Busisi. lakini barabara inayounganisha sasa daraja la Busisi hadi Kahama haijawekwa katika mpango wa kufanyiwa upembuzi yakinifu. Napenda sana jambo hili nalo nisikie limefikia hatua gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kutoka Kahama – Mhongolo - Burige - Solwa – Mwanangwa – Mwanza. Barabara hii ilikuwa ijengwe kwa MCC lakini kwa bahati mbaya fedha zile zilipoondoka ikawa imeingizwa kwenye mipango ya Serikali lakini sioni kama imewekwa katika mpango wa kufanyiwa upembuzi yakinifu. Nataka barabara hizi mbili niweze kuambiwa kitu gani kinaendelea au ni hatua gani imefanyika hadi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilimsikia Rais wa Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame akiwaelekeza viongozi wa Wizara ya Tanzania na Rwanda waanze kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga reli kutoka Isaka - Kigali. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijasikia lolote kwamba hatua gani imefikiwa sasa kwanza katika kufanya feasibility study na detail design ya reli hii lakini pia hata kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Mheshimiwa Rais niliyasikia vizuri kabisa alisema ifikapo mwaka 2020 angalau hatua fulani ya ujenzi iwe imeanza. Wananchi wa Msalala hasa Isaka na wananchi wa Tanzania kwa ujumla wanapenda kujua hatua gani imefikiwa katika utekelezaji wa agizo hilo la Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ambalo nataka kumalizia ni suala la mawasiliano. Nashukuru Serikali imefanya kazi kubwa sana kupitia wawekezaji wa private sector kuweka minara mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Tatizo tulilonalo ni kwamba maeneo ambayo yamejengwa minara hii wenye minara hawalipi ushuru kwenye halmashauri (service levy) na vilevile hawalipi tozo yoyote ya ardhi kwenye kijiji na hata kwa wananchi ambao ardhi yao imechukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, limekuwa ni jambo ambalo wamekuwa wakiliulizia na mara kadhaa tumekuwa tukiongea na Naibu Waziri, Mheshimiwa Atashasta Nditiye kuhusu suala hili, lakini kwa sababu tumekuwa tukiongea binafsi, wakati mwingine tunaongea tukiwa nje ya ukumbi huu ambao ni rasmi, napenda sana angalau leo awatangazie Watanzania kwamba ni utaratibu gani hasa ambao unapaswa kutumika kwa wananchi ili waweze kupata appropriate share ya service levy inayotoka kwenye makampuni ya simu yaliyoweka minara yao vijijini lakini vilevile…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba kuunga mkono hoja.