Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii ya Waziri wa Ujenzi. Awali ya yote, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, lakini na kwa namna ambavyo ameweza kujipambanua katika kitabu hiki maana miradi yote inaonekana na iko wazi, hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, nitaenda kwa haraka sana. Namba moja, nashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri alikuja Musoma na kama alivyokuwa ametuahidi Mheshimiwa Rais kujengewa uwanja wa ndege zoezi hilo limeanza na nimeona kwenye kitabu chetu hiki ziko kama shilingi bilioni 11, hongera kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu moja tu kwamba, kama Mheshimiwa Waziri alivyokuja tukazunguka katika maeneo yale kuna nyumba kama 106 ambazo zinahitaji fidia. Naomba atuambie lini tutawalipa hawa watu fidia ili waweze kuanzisha maisha yao mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla ya hizi nyumba 106 tulikuwa na mpango wa kuchukua eneo kubwa zaidi ambalo lilichukua zaidi ya nyumba 300. Zile nyumba zote ziliwekewa X na kwa sababu sasa tulipunguza tukarudi nyumba 106, naomba Mheshimiwa Waziri awaambie watendaji wake waende kufuta zile X kwa sababu nyumba zile watu wamehama na hawawezi kupanga tena wakiamini kwamba wakati wowote zitabomolewa. Mbaya zaidi hata benki sasa, wale wenye zile nyumba zingine hawakopi kwa sababu mabenki yanaamini kwamba nyumba zile nazo ziko katika mpango wa kuondolewa. Kwa hiyo, hilo nadhani ni vizuri likafanyika kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni barabara ya Nata – Mugumu – Klein’s Gate - Mto wa Mbu. Barabara hii tumekuwa tukiizungumza kwa kipindi kirefu lakini safari hii hata kuonyeshwa kwenye kitabu hiki Mheshimiwa Waziri hajaonyesha. Kwa hiyo, naomba tufahamu kama barabara hii imeondolewa maana ilikuwa inajengwa katika kiwango cha lami, kama imeondolewa basi ni vizuri tukajua kuliko kukaa kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni la muhimu kwetu ni ile barabara inayotoka Musoma Mjini – Makojo. Barabara hii tunashukuru kwamba angalau safari hii imepata kama shilingi bilioni tatu lakini ina zaidi ya miaka 10 kila leo ni upembuzi yakinifu sijui fedha hizi ndiyo zitaanza lami au bado tuko kwenye upembuzi yakinifu. Kwa hiyo, hilo nalo ningependa kupata maelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la reli ya kutoka Tanga – Moshi - Arusha - Musoma. Mimi ile naingia hapa Bungeni mwaka 2005 kulikuwa na mpango huu wa hii reli ya kuja Musoma, lakini mpaka leo hivi tunavyozungumza kila siku inapewa tu fedha ndogo mfano kama safari hii nimeona kuna shilingi bilioni mbili. Sasa ni zaidi ya miaka 15 suala la upembuzi yakinifu bado linaendelea. Napenda Mheshimiwa Waziri atoe maelezo ya kina kuhusiana na hiyo reli ya Tanga – Musoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho linahusiana na hawa wakandarasi wetu wa ndani. Kwa kweli wazo na mipango ya Serikali ni mizuri kuwawezesha wakandarasi wa ndani, lakini hawa wakandarasi wa ndani kwa utaratibu tunaoenda ni kweli kwamba hawawezi kukomaa. Mfano, ukiangalia barabara ya Makutano - Nata ni zaidi ya miaka mitano inajengwa katika kiwango cha lami lakini haisogei. Kwa hiyo, wakati mwingine tunakuwa na mashaka kwamba wale wakandarasi ndiyo hawana uwezo kwa maana kwamba ndiyo hawajengi lakini ukiangalia kwa kiasi kikubwa inachangiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inachangia kwa sababu gani? Kama kweli tumedhamiria kwamba tunahitaji kuwa-empower ni lazima hata pale wanapoomba zile advance payment tuwe tunawapa kwa wakati. Kwa hiyo, anapojikuta kwamba akiomba advance payment hatuwezi kuwapa na inachukua muda mrefu na tunatambua kwamba hawana uwezo hayo ndiyo matokeo kwamba mradi mmoja unachukua muda mrefu na matokeo yake badala ya kumsaidia mkandarasi yule tunaendelea kumdhoofisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliangalie sana suala la namna ya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naunga mkono hoja.