Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nichangie katika Wizara hii ambayo nayo ni mhimili wa uchumi katika nchi yoyote duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa jitihada zake za kujenga miundombinu ya reli lakini kutaka kuunganisha mikoa yote kwa njia ya barabara za lami. Dhamira hii ya Serikali ya kuunganisha mikoa kwa kiwango cha lami imekuwa ya siku nyingi lakini barabara ambazo hata Mheshimiwa Waziri ameionesha katika kitabu chake, barabara ya kutoka Makongolosi hadi Mkiwa, kuna kilometa 413, katika Jimbo ambalo mimi ndio mwakilishi wake ziko kilometa 219.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inajengwa kutoka Mbeya, Mbeya – Lwanjilo - Chunya, sasa wanajenga Chunya hadi Makongolosi katikati pale kilometa 43. Upande wa Singida barabara hii sijui kuna makosa gani ambayo watu wa Singida wamefanya hadi hii leo, mwaka jana katika kitabu cha Waziri alionesha dhamira kwamba barabara hii inajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati Naibu Waziri aliyekuwepo yeye mwenyewe Waziri amefika Itigi kuzungumza na wananchi kwamba barabara hii itajengwa na tukawaaminisha wananchi barabara hii sasa inajengwa. Ikatengwa pesa, ikatangazwa barabara na mkandarasi akapatikana. Hata hivyo, baada ya muda sijui kilizuka kitu gani barabara hii nayo mwaka huu imewekwa katika mpango vilevile, mkandarasi alipatikana Sinohydro lakini sasa sijui wamemwondoa sijui wamemfanyaje, tunapata taarifa kwamba watatangaza lakini sio rasmi, hizi ni redio mbao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri kwa kuwa mwenyewe yupo hapa hebu atuambie na awaambie wapiga kura waaminifu kwa chama hiki ambacho Serikali yake na yeye ndio anatoka wamenichagua mimi kwa ajili ya kuhakikisha barabara hii sasa inajengwa. Atawaambiaje wananchi wa Itigi, mwaka huu tunaanza kujenga barabara au tutabaki na zile story za miaka nenda, miaka rudi toka enzi ya Baba wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ina kilometa mia nne na kumi na, ni barabara pekee inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Singida, hakuna barabara mbadala na ukitoka Singida kwenda Mbeya lazima uje tena Dodoma – Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi Profesa Mbarawa yeye ni mwaminifu, ni mtu kweli; hebu sasa awaoneshe watu wa Itigi ukweli wake kwamba barabara hii mwaka huu wanaijenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,nifurahie na niseme kwamba Serikali hii imeonesha usikivu kwa kuonesha kuunganisha Mkoa wa Singida na mikoa mingine kupitia barabara hii ambayo ameitaja katika kurasa zake wakati anazungumza katika ukurasa huo wa 147 amezungumzia barabara ya Handeni – Kiblashi – Kibaya, ni kilometa 460 ukitokea Singida mpaka pale Handeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali kweli imedhamiria kuijenga barabara ile kwa kiwango cha lami ina maana inaungana na mpango ule wa East Africa wa Serikali ya Uganda kupitisha bomba lile katika ukanda huu wa kwetu. Kwa hiyo, wananchi wanaotoka na mizigo yao katika Bandari ya Tanga na bandari ambayo tunaamini Wizara hii inahusika itakuwa ni miongoni mwa bandari ambazo zitaihudumia sana nchi hii kuisaidia mzigo uliopo katika bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, barabara hii ikijengwa itasadia mizigo ambayo inakwenda nchi jirani pamoja na nchi ya Kongo, watu hawatapita tena Dodoma na hapa makao makuu patapunguziwa mzigo, wajasiliamali hizi by pass tunazozijenga za mji zitapunguziwa mzigo, watu watatoka Bandari ya Tanga, watapita Handeni pale moja kwa moja wanatokea Singida, tayari tunaboresha uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la mawasiliano, baadhi ya maeneo ya Jimbo langu yana shida ya mawasiliano ya simu. Maeneo ya Mbugani, Kintanula, Gulungu nilishaandika barua, lakini na Wizara ilishatambua maeneo ya Lulanga na Itagata kuwa yana shida hii ya mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara hii sasa basi waweke mkazo katika suala hili ili wananchi ambao nao ni wa nchi hii wanufaike na rasilimali za nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niisemee Serikali niipongeze kwenye suala la kuimarisha na kuhakikisha TTCL inasimama imara, lakini kuna tatizo ambalo TTCL wanalo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.