Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nichangie katika hoja hii ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Muda wa dakika tano ni mdogo sana, lakini nataka niseme na kuipongeza sana Serikali kwamba katika sekta hii tumetoka mbali sana, tulikuwa tukisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza tunapitia Nairobi, safari ya siku moja tunakwenda siku mbili. (Mkakofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeanza kujenga reli, tunaboresha Shirika la Ndege la Tanzania na tunaboresha communication nchi nzima, tusikate tamaa, pale tunapopata matatizo madogo madogo kwani hizi ndio changamoto za maendeleo na tuwe tayari kupambana nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu mwezi Aprili, mwaka 2015 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi alitutembelea kukagua barabara inayojengwa kwa lami kutoka Mwanga kwenda Usangi mpaka Uchamangofi. Barabara hiyo sasa inajengwa kwa nguvu kubwa kabisa na nataka nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaifanya na kwa kazi ambayo anatufanyia pale kwenye Jimbo la Mwanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha barabara hii ambacho kimebakia cha kutoka Kikweni kwenda Msangeni – Kifula – Mwaniko mpaka Uchamangofi na chenyewe kimetengewa fedha katika bajeti hii na napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na watendaji wake wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya bila kuchoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mkisikia kuna watu wanatoa hoja kuwapinga sana wapuuzeni, nendeni mbele kwa sababu hata Marekani leo inawekeza bado kwenye miundombinu, hata Uingereza ina kazi ya kuwekeza kwenye miundombinu. Matatizo tunayopata sasa hayawezi kwisha, kila siku yatakuwepo na kila siku tuwe tayari kupambana nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niishukuru Serikali kwa kupandisha daraja barabara mbili, moja kutoka Lomwe - Ndolwe - Kilomeni - Lembeni kuwa barabara ya TANROAD na nyingine kutoka Kilya - Kitichamungu - Nyabinda - Kagongo - Lang’ata - Tingatinga - Kifaru na katika bajeti hii naona shilingi milioni 565 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Napenda nichukue fursa hii kuishukuru sana Wizara inayohusika, lakini pia kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana ambayo anafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wa dakika tano ni mdogo sana, lakini napenda niseme kwamba katika barabara moja ambayo ndiyo kubwa sana ya TANROADS katika Wilaya yangu ya Mwanga kutoka Kifaru - Kigonigoni - Kichwa cha Ng’ombe kuna maeneo ambayo yameharibika sana na barabara wakati huu haipitiki kabisa kwa sababu ya mvua. Nawasihi sana, namsihi sana Mheshimiwa Waziri afanye kila juhudi ili eneo la kutoka Kisokoro - Kigonigoni - Mvuleni liweze kutengenezwa ili wananchi waweze kushughulika na shughuli zao za biashara kama ambavyo wamekuwa wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana pia nihimize kwamba maeneo ambayo hayafikiki kwa mtandao wa simu yawekewe juhudi maalum kule katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na maeneo ya Kisangara Juu na Jipendea yapate minara mipya ya mawasiliano ili wananchi waweze kuendelea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)