Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la barabara, lakini kwanza nianze na fedha iliyotengwa kwa ajili ya Mfuko wa Barabara kwa Mkoa mzima wa Tabora. Kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukiangalia fedha iliyotengwa kwa Mkoa wa Tabora barabara za ndani ni milioni mia nane themanini na tano tu, lakini ukiangalia Mkoa wa Tabora kwa Tanzania ndio mkoa unaoongoza kuwa mkubwa kwa sasa hivi kuliko mikoa yote na ni mkoa ambao una mzunguko mkubwa sana wa barabara tofauti na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, fedha iliyotengwa na hali ya barabara za Mkoa wa Tabora ni hatari sana kwa mwaka huu mzima. Iko mikoa mingine wamepata mpaka bilioni mbili, tatu, moja point, kwa Mkoa wa Tabora kuwapa milioni mia nane themanini na tano ni fedha kidogo sana.

Mheshimiwa Spika, tunaomba Wizara iuangalie Mkoa wa Tabora kwa jicho la pekee. Hivi tunavyoongea kuna maeneo ambayo hayapitiki kabisa wananchi wanaogelea, hali ya uchumi ni mbaya, mazao hayasafirishwi kwenda mjini kwa sababu barabara zile ni mbovu sana.

Mheshimiwa Spika, specifically nizungumzie barabara ya kutoka Kaliua na hasa eneo ambalo linatoka pale Kazilambwa Kaliua kwenda Chagu ambako ni mpakani mwa Uvinza Mkoa wa Kigoma. Barabara hii ni mbaya sana na nimekuwa nikiomba ipatiwe fedha za kujengwa kwa kiwango cha lami. Hivi ninavyoongea na wiki nzima iliyopita sikuwepo hapa Bungeni kwa sababu nilikuwa jimboni. Hali ni mbaya kweli kweli; watoto, wagonjwa, wazee wamekaa pale zaidi ya siku nne kwa sababu ya barabara.

Mheshimiwa Spika, TANROAD Mkoa wamejitahidi kurekebisha eneo moja, hilo ni eneo moja tu. Barabara hii imekatika maeneo manne tofauti, hivi tunavyoendelea huku ni bahari, huku ni bahari. Kwa mvua zinazoendelea barabara ile yote inaenda kuteketea mwaka huu. Ukiangalia barabara ya Mpanda imekatika, magari yamekuwa yakitumia kutoka Tabora kwenda Kaliua na kwenda Mpanda, leo haipitiki, Kaliua kwenda Tabora haipitiki, Watanzania watateseka sana.

Mheshimiwa Spika, tunaomba Serikali, nilikuwa naangalia pia kwenye kitabu, ukiangalia fedha iliyotengwa kwa fedha za ndani kwenye barabara kuu kwa Mkoa wa Tabora ni barabara mbili tu na mojawapo ni Kaliua kwenda Puge na fedha iliyotengwa ni milioni saba, inafanya nini kwa uharibifu ule?

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie, kwa Kaliua kwa kweli inahitaji special priority mwaka huu, vinginevyo tutakuwa ni kisiwa. Barabara zote hazipitiki za ndani hazipitiki, barabara kuu hazipitiki, wananchi wale wako katika hali mbaya sana sana.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la kampuni hizi za ujenzi. Tumekuwa tunashuhudia kampuni za ujenzi zinapewa tender zinakwenda kuchukua material kwa ajili ya kujenga kwenye vijiji huko changarawe, mawe, mchanga lakini bahati mbaya sana wanapokabidhi kazi baada ya ujenzi hawatengenezi zile barabara wanaziacha zikiwa katika hali mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, mfano mkubwa ni wa Kaliua, Kampuni ya Chico ilipewa mradi kutengeneza barabara ya Kazilambwa kuja Kaliua Mjini, wamekwenda kuchukua kokoto kutoka Igwisi; kwanza wamemaliza, tumepiga kelele sana kwenye halmashauri na hata hapa Bungeni, kwamba watengeneze barabara ya Igwisi kuja Kaliua, lakini wamemaliza kazi, wamekabidhi kazi barabara ile sasa hivi ni mashimo ni mahandaki, hakuingiliki na wameshaondoka tayari.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali bado Chiko wamepewa kazi nyingine Mkoa wa Tabora, waelekezwe wakatengeneze barabara ya Igwisi kuja Kaliua, ni barabara ya uchumi lakini kwa hali ambayo imeachwa ni hali ambayo ni mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia TARURA wanapewa fedha ndogo, hazitoshi kutengeneza zile barabara ambazo zimeharibiwa na Chico lakini wameondoka wameachia madhara makubwa pale. Pia hata fedha ya wananchi wa Igwisi ambapo walichukua kokoto na mchanga pia hawakuwapa stahili zao kama walivyokubaliana kwenye mikataba yao.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali itoe agizo, kampuni zote zinavyopewa tender kabla ya kukabidhi kazi na kupewa certificate ya mwisho wahakikishe kwamba wanatengeneza barabara na kufukia mashimo ili waweze kuacha mazingira yale yakiwa katika hali nzuri.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu uharibifu wa miundombinu barabani. Tumekuwa tunashuhudia barabara zetu zinatengenezwa kwa gharama kubwa sana lakini kiukweli zinaharibika sana sana na zipo taarifa za uhakika kwamba miundombinu yetu ya barabara inahujumiwa kwa namna ya kutumia kwamba ni screpa. Zipo taarifa kwamba vifaa vingi ambavyo vinaingia barabarani vinapelekwa kwenye scraper.

Mheshimiwa Spika, hebu Serikali tuangalie tunawezaje kuruhusu scraper mpaka zinapelekwa kwenye viwanda? Viwanda tunavijua, vinatengeneza chuma katika maeneo mbalimbali lakini vinatumika vifaa vya ujenzi barabarani, zinatumika alama za barabarani, ni miundombinu ya barabani. Leo haiwezekani kuendelea kutengeneza gharama kubwa hivi wakati inahujumiwa na tunajua.

Mheshimiwa Spika, ninazo taarifa kwamba nyingine zimefikia Serikalini lakini hazipatiwi taarifa, nitakuja kuongea na Waziri nimpatie takwimu ni namna gani ambavyo barabara zinahujumiwa na baadhi ya watu wanafahamika, lakini hatua hazichukuliwi.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu reli. Niipongeze Serikali kwa hatua ambayo imefikia ya kutengeneza reli kwa standard gauge kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro pia Morogoro mpaka Dodoma na nina imani kwamba itatoka Dodoma itakwenda Kaliua na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea bado mabehewa ni machache sana. Pamoja na kuwa kweli reli hii ni reli ya uchumi, reli hii, kama tunavyosema hatuwezi kuacha barabara kuharibiwa kama hatutengenezi reli zikawa imara. Pia reli inaweza ikawa nzuri ikawa inapitika lakini bado ikawa na mabehewa machache, Kaliua mabehewa ni machache sana na nimeongea na Waziri na yeye amefika jimboni ameona, wananchi wengi wanashindwa kutumia reli kwa sababu ya uchache wa mabehewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali, Waziri aliagiza kwamba ataongeza bajeti kwa ajili ya kununua mabehewa, nilikuwa nategemea niione huku bajeti tuongeze mabehewa ili usafiri huu wa reli uweze kunufaisha wananchi wa Kaliua, Mpanda na maeneo mengine. Kwa sababu sasa hivi wanahesabiwa watu 15 mpaka 20 wakati wengi wao wangependa kusafiri na reli lakini wanashindwa wanatumia barabara ambapo pia hazina uhakika sana.

Mheshimiwa Spika, lingine, ni pale wasafiri watakapotaka kusafiri reli imepata matatizo, wananchi wanashindwa kupewa taarifa kwa muda. Hivi wiki iliyopita wako wasafiri wamekaa Kaliua siku tatu mpaka wakaandamana kwenda kwa Mkuu wa Wilaya, kwenda kwa Mbunge kwa sababu wana njaa wameishiwa, hawaambiwi taarifa zozote ikawa ni matatizo.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali, kwa kuwa kuna communication nzuri pale inapotokea tatizo kwamba miundombinu ya barabara labda reli imekatika mahali waelezwe, tusisubiri waandamane waanze kulia na watu wanakuwa wameshateseka sana na wanaumwa na mbu. Tuwape taarifa kwamba reli itakuwa tayari siku fulani prior, kabla ya kuteseka na tuhakikishe kwamba wasafiri wetu wanaweza kusafiri kwa muda. Pia tuharakishe lile tatizo ambalo limetokea ili wasiendelee kuteseka. Kwa kweli ukifika pale Kaliua wakati ambapo reli imeharibika utaona uchungu, watoto wamelala chini, wagonjwa wamelala chini ni mateso ya hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu mawasiliano ya simu. Kwanza nashukuru kwamba kiukweli, hata mimi mwenyewe na wananchi wengi hawajui kwamba kuna mpango wa fursa za mawasiliano kwa wote ambao unajenga minara nchini.

Mheshimiwa Spika, sisi tulifikiri kwamba minara mingi inajengwa na kampuni za simu, lakini kumbe tuna mpango mzuri wa mawasiliano kwa wote ambapo unajenga minara. Kwa hiyo, kwanza naomba, kwa kuwa sisi kama Taifa tuna mpango wa mawasiliano kwa wote, tunaomba wahakikishe kwamba maeneo ambayo kampuni hazifiki wanafika waweke mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyoongea Wilaya ya Kaliua kuna maeneo mengi sana hakuna mawasiliano ya simu mpaka upande juu ya mti, juu ya paa ndipo upate mawasiliano. Maeneo ya Igwisi, Mloka, Usenye, Usinge na maeneo mengine, nikihesabu hapa vijiji zaidi ya 20 hakuna mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Wizara hii ijue kwamba mawasiliano sasa hivi ni uchumi, kama hakuna mawasiliano hakuna uchumi; huwezi kufanya biashara kama hakuna mawasiliano. Kwa hiyo tunaiomba Serikali ihakikishe kwamba inapeleka mawasiliano maeneo yote ya Kaliua ambayo hayana mawasiliano ili wananchi waweze kupata mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la mawasiliano ya redio; yapo maeneo ambapo hakuna radio kabisa. Tunaomba Serikali ihakikishe kwamba mawasiliano ya redio yanakuwepo, kwa sababu dunia ya leo kama hakuna mawasiliano ya simu wala redio ni kwamba unakuwa kisiwani.

Mheshimiwa Spika, kuhusu magari kujaza kupita uwezo. Tumekuwa tunalalamika, ukiona barabara zetu zilivyokuwa na mabonde; ni hatari kubwa, lakini ninachoshangaa ni kwamba tunayo mizani, sasa inafanya nini? Kwa nini tunaruhusu magari kujaza kupita uwezo licha ya kwamba pia barabara zinaharibika kwa haraka pia zinasababisha ajali?

Mheshimiwa Spika,Leo ukiwa unaendesha kutoka Morogoro kuja Dodoma unakutana na milima ndani ya barabara ingawa tunayo mizani. Naiomba Serikali tuhakikishe magari yanatii sheria…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.