Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niongee. Niliomba dakika 10 za kikanuni kwa sababu sijawahi kuchangia kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kwa kunipa nafasi hii tena kwa mwaka huu ili niweze kuchangia habari za wananchi wa Igunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti,, nataka niseme na jambo hili nimeendelea kulisema kila wakati, kijiolojia Jimbo la Igunga ni ziwa lililokauka miaka 60 elfu iliyopita. Narudia hili ili Mheshimiwa Waziri anielewe, kwamba kujenga barabara kwenye eneo hilo la Mbuga ni lazima ujenge tuta kubwa. Halmashauri imeshindwa kujenga barabara hizi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya zaidi Jimbo la Igunga halina barabara hata moja ya TANROADS. Tuna kata 13 ziko kwenye jimbo hili, sasa hivi ukienda hakuna hata kata moja ambayo unaweza kufika kwa sababu hapafikiki kabisa. Nimeomba mwaka jana na naomba tena kwa Mheshimiwa Waziri, Igunga hatuna barabara, tunaomba waje watutengenezee barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014, 2015 na 2016 tuliomba barabara ya kutoka Igurubi kuja Igunga ipandishwe hadhi. Barabara hii inaunganisha wilaya yetu na mkoa wetu na Mkoa wa Shinyanga. Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana wakatuambia kwamba wameirudisha TARURA, kwa kweli inatusikitisha sana, jimbo lisilo na barabara yoyote ya TANROADS inayohudumiwa na mkoa halafu wakairudisha TARURA tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu kuliko barabara zote kwenye Jimbo la Igunga kwa sababu sisi Jimbo la Igunga tunalima asilimia 90 ya pamba inayolimwa Mkoa wa Tabora. Sasa hivi ndiyo tunaozalisha mbegu kwa ajili ya wakulima wa pamba Tanzania. Hiyo mbegu au pamba inayozalisha hiyo mbegu inatoka kwenye barabara hii. Ziko kata kama 13 kwenye barabara hii ambazo zimelima pamba mwaka huu vizuri na tunategemea barabara hii ndiyo ibebe pamba hizo kutoka kwenye maeneo hayo, halafu wanatuambia kwamba imerudi TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli samahani sana nashindwa kuongea, naongea kwa uchungu na wananchi wa Igunga wananisikia. Barabara ya kutoka Igurubi kwenda Igunga tuliomba ipandishwe na tunaomba bado ipandishwe TARURA hawaiwezi. Sasa hivi ukitoka Igunga kwenda Igurubi hamna mtu anayeweza kwenda tena. Naomba sana Mheshimiwa Waziri anisikilize safari hii. Kwenye kitabu hiki cha bajeti mimi sina barabara yoyote humo ndani, nasema hapa kwa sababu ni kama vile wananchi wa jimbo lile wamesahauliwa wameachwa. Kuna Wabunge wamesema hapa hivi Jimbo la Igunga tuna matatizo gani au tumekosa nini hasa? Naomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambayo tuliomba ipandishwa hadhi ni barabara ya kutoka Igunga kwenda Itumba mpaka Loya. Hii barabara inafungua tena Mkoa wa Tabora inaunganisha na ile barabara wanayoifungua inatoka Tura kwenda Iyumbu na ukiziunganisha hizo barabara unakwenda mpaka Mbeya.

Mheshimiwa Spika, tuliomba ipandishwe hadhi, makaratasi yote tulipeleka na ikakubalika, lakini leo tumeambiwa tena bado iko TARURA na TARURA hawana uwezo. Sasa hivi hiyo barabara ya kutoka Igunga kwenda Itumba kupitia Mwanzugi daraja limebomolewa kabisa na kuna Mkandarasi alikuwa anajaribu kujenga pale, lakini hana fedha ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi niliuliza swali watafanya fanyaje basi kutusaidia barabara hiyo haipitiki kabisa saa hizi na huko ndiyo nyumbani kwetu, mimi nikifika kule inabidi nitembee kwa mguu kwenda nyumbani kwetu. Naomba tena hii barabara kama wanaweza kuipandisha hadhi ili wafungue Mkoa wa Tabora, wafungue jimbo hili liunganike na Singida na Mbeya, litakuwa jambo zuri kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naomba tena, Mheshimiwa Waziri kama anaweza kuja kututembelea Igunga aje; pamoja na kwamba kuna barabara moja tu kuu ya kwenda Mwanza kutoka Singida basi aje tumpitishe hata kidogo wakati wa masika aone mambo yalivyo, nadhani anaweza akaelewa hiki ninachokisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Igunga kwa sasa hivi hawawasiliani kabisa, hakuna mtu anayeweza kutoka Igurubi akaja Igunga, hakuna mtu anayeweza kutoka Itumba akaja mjini Igunga, hakuna mtu anayetoka hata Isugiro pale karibu karibu pale akaja mjini, hali ni mbaya kweli kweli na wananchi wanasema sasa Mheshimiwa Mbunge tunafanyaje? Nikawaambia nitalisemea hili jambo na saa hizi wanaweza kuwa wananisikia. Hamna Bunge live lakini nadhani nitapeleka kibwagizo kidogo wasikilize sikilize haya ninayoyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakinisaidia hizo barabara mbili wakafungua tukatoka tunaweza kutoka Kolandoto tukapita Ukenyenge, tukaja Igurubi, tukaja Mwamakona, Mbutu, Igunga tukaenda Itumba tukaenda Loya, Tura tukaenda mpaka Mbeya, watakuwa wamenisaidia sana. Kwanza wamefungua maeneo ya kiuchumi, pamba yote ipo maeneo hayo kama nilivyosema. Upande wa huku chini kuna mifugo, concentration ya mifugo mingi iko kusini mwa Igunga mpaka Loya kwa ndugu yangu wa Igalula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakifungua hii barabara tutakuwa na ng’ombe wengi ambao watafikia minada. Sasa hivi tunapeleka ng’ombe kwenye minada ya Singida. Tunaomba sana Waheshimiwa Mawaziri hebu wanisikilize na mimi, naongea taratibu kwa uchungu ili wanisikilize jamani, tafadhali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka kusema kuna madaraja ambayo yanaunganisha kata kwa kata ambayo ni makubwa kiasi ambacho hayawezi kujengwa na halmashauri wala na TARURA. Naomba madaraja hayo nitakayoyataja wayafanye kama walivyofanya daraja la Mbutu. Daraja la Mbutu lilikuwa ni daraja lililokuwa chini ya halmashauri lakini kwa umuhimu wake lilijengwa na mradi maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madaraja hayo pamoja na daraja la kutoka Igunga kwenda Mwanzugi, mahali ambapo saa hizi pamebomolewa panahitaji madaraja zaidi ya matano, mkandarasi aliyepo hawezi kuyajenga. Tuna daraja la kutoka Bukoko kwenda Mtungulu Mto Ncheli, mto mkubwa sana, watu wa Ncheli kule pamoja na Mtungulu hawawezi kuwasiliana na wilaya, kwa sasa hivi wanakaa huko mpaka mvua ziishe. Ni daraja kubwa kweli kweli linahitaji bilioni kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna daraja la kutoka Itunduru kwenda Kagongwa, wananchi wale wakati wa mvua lazima watembee kwa mguu, wanajaribu kwenda Shinyanga kwa upande wa pili. Kuja huku hawawezi, ni daraja kubwa kweli, halmashauri haiwezi pamoja na TARURA haiwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja la mwisho, ni kutoka Igunga kwenda Isugiro, ni hapo hapo karibu. Mto Igogo ambao unajaza maji kwenye bwawa la Igogo unapotoa maji unakatisha barabara, haiwezekani kabisa kujenga daraja hilo na halipo hilo daraja. Naomba Mheshimiwa Waziri wanisaidie ili na mimi angalau niwe kama wengine kama kata zingine, kama wilaya zingine, kama majimbo mengine niwe na barabara hata za TANROADS mbili, tatu hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunisikiliza na Mungu awabariki.