Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia hotuba ya Wizara hii. Kwanza kabisa, nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Mheshimiwa Injinia Nditiye pamoja na Mheshimiwa Kwandikwa pamoja na wataalam wa Wizara. Nimshukuru Mheshimiwa Profesa Mbarawa kwa kazi nzuri aliyoifanya alipokuja kule jimboni kwangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli mustakabali wa nchi hii unategemea sana miundombinu ya barabara. Tunakwenda kwenye nchi ya viwanda, tusipozungumza habari ya barabara, hakuna mafanikio tena kuhusu viwanda. Kwa hiyo, niwaombe sana hizi kelele ambazo tunapiga siyo kwa manufaa yetu bali ni kwa manufaa ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitakuwa na maneno mengi sana, nitakuwa na maneno kidogo sana. Kwanza nianze na barabara ya mkoa ya Kilolo ambayo inaanzia Iringa – Kilolo - Idete. Barabara hii si ngeni kwa sababu Marais wote waliopita walitoa ahadi, ni barabara ambayo iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mheshimiwa Profesa Mbarawa alifika na alituahidi alichotuahidi, wananchi wanaendelea kusubiri. Mheshimiwa Makamu wa Rais amefika, ameahidi na wananchi wanaendelea kusubiri.

Barabara hii siyo inaunganisha Kilolo tu, barabara ya Kilolo yenyewe sasa, tuliomba lami kutoka wilayani ni kilometa nane lakini inaunganika na kilometa tatu za Iringa Mjini, kilometa kumi za Kalenga, zote zinapita kwenye barabara hiyo zinafikia takribani kilometa 21.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ambayo tunayo ni ya kujenga kilometa mojamoja. Nilishawahi kuuliza hapa Bungeni, barabara hii kwa ahadi hiyo itajengwa kwa miaka 21, Mheshimiwa Profesa Mbarawa hatakuwepo kwenye nafasi hiyo, mimi sitakuwepo tena, miaka 21 mingi, ndugu yangu Mheshimiwa Injinia Nditiye na yeye hatakuwepo na Mheshimiwa Kwandikwa hatakuwepo. Sasa tunaomba waitendee haki, unaposikia ujenzi wa Makao Makuu Dodoma mbao asilimia 60 zinatoka Kilolo. Kama kweli zinatoka Kilolo inakuwaje unamwacha mtu ambaye analeta maendeleo kwenye makao makuu ya nchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali kubwa, nzuri ya halmashauri ya wilaya imejengwa Kilolo, ndiyo hospitali ya mfano, lakini hospitali ile itawasaidia hata watu wa kutoka Iringa Mjini, Mufindi na sehemu nyingine, unawasafirishaje? Sidhani kama kuna mgonjwa ambaye atapona akiwa anapelekwa kwenye ile hospitali. Ili waendelee kuwaombea vizuri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa afanye lile Mungu atakalomjalia kuhakikisha kwamba hizo kilometa tunazipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Mfugale ambaye kwa kweli ametusaidia sana nchi hii pamoja na Mkoa wa Iringa kwa ujumla kwa kujua umuhimu wake. Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema, aendelee kumlinda ili aendelee kutusaidia pale atakapoweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ya mkoa inakwenda mpaka Idete, nimeshawahi kusema hapa Bungeni kwamba barabara pekee inayounganisha Mkoa wa Iringa na Mkoa wa Morogoro inapita kwenye Milima ya Kitonga. Siku milima ile mawe yakadondokea barabarani
au kukatokea tafrani yoyote, uwezekano wa magari ya kutoka South Africa, Zambia, Malawi kwenda Dar es Salaam au Morogoro itakuwa hakuna. Kwa hiyo, barabara pekee ni kuunganisha Idete – Itonya – Muhanga - Morogoro (Mbingu) kwa Mheshimiwa Susan Kiwanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile siyo ndefu, ni kilometa takribani 25, wananchi wameshaifungua na ahadi ya mwanzo ilikuwa kwamba barabara ile mkoa iichukue kwa sababu ni barabara ambayo ilikuwa ya mkoa. Sasa baada ya TARURA kuanza bado TANROADS wanaweza kuweka mkono wao hata kwa wataalam ili barabara ile sasa ipitike. Leo tunazungumza hapa kama mzaha lakini kuna siku watakuja kukumbuka maneno yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sitaki sana kusema kwa sababu nimeshasema sana kuhusu suala hili niende kwenye mawasiliano. Ndugu yangu Mheshimiwa Injinia Nditiye anajua tumetoka wote Kibondo kule, sasa akija akinitupa leo kwa kukosa mawasiliano nikienda Kibondo nitazungumza kule kwamba ndugu yangu ameshindwa kunisaidia, itakuwa siyo kitu kizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu, kwa mfano, Ifua, Udekwa, Irambo, Ibumu, Magana, Ilindi ambako ni Mahenge, Imalutwa, Lugalo, hivyo ni Vijiji, Mbawi, Masisiwe, Isere, Ukwega, Ikula, Ruaha, Mbuyuni na Isagwa hakuna kabisa mawasiliano. Bado narudi palepale, tunakwenda kwenye nchi ya viwanda, unaendaje kwenye nchi ya viwanda wakati mawasiliano hakuna, barabara hakuna. Kwa hiyo, mimi nimwombe ndugu yangu, aliniahidi kufanya ziara, hebu afanye ziara. Kama atakuwa hana mafuta niko tayari kumwekea ili tuweze kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kwandikwa na yeye kwa sababu Mheshimiwa Profesa Mbarawa alishafika, kazi sasa ni yeye, wao ndiyo wasaidizi wake, aje Kilolo sio mbali, kilometa zile sio nyingi, ziko kwenye ilani. Nikileta Hansard hapa toka mwaka 2000 nikiwa Mbunge nimekuwa nikiambiwa habari zilezile. Sasa tusimuangushe Mheshimiwa Profesa Mbarawa, kama kweli wanampenda twende sote pale, sio mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli katutengenezea barabara, kutoka Iringa mpaka Dodoma ni saa mbili na nusu, hata kama Bunge limeahirishwa, twende tunarudi tunakuja kutoa maoni hapa. Mnajua hasira za watu wa Iringa, kuna mambo mengi ambayo hayaendi vizuri, sasa hivi hatujinyongi tena, tunapanda juu ya mti unajitupa kwenye lami unakufa vizuri. Kwa hiyo, tutengenezeeni lami tu ili tuache kujitundika kwenye miti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndege, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, amefanya kazi kubwa, ametuletea ndege za uhakika na kelele hizi zilikuwa zinapigwa nchi gani haina hata ndege, lakini leo tuna ndege. Mheshimiwa aendelee kuongeza kwa sababu siku zote vita ya kiuchumi lazima akubali na kelele lazima zipigwe. Wako ambao watasema huyo, huyo, yeye asigeuke nyuma, aende, pale alipo na sisi tupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, standard gauge, hata kama haipiti Kilolo, Iringa huko ni kwa ajili ya nchi hii. Barabara zetu zinakufa kwa sababu hatuna reli, kila mtu anajua hilo. Kwa hiyo, reli ile itakwenda mpaka Moshi kwa Mheshimiwa Mdee kule itafika na tunaomba waifungue ile. Mheshimiwa Injinia Nditiye wajitahidi waifungue ili Mheshimiwa Mdee naye aone manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema pia suala la kuimarisha barabara nyingine hasa hapa Dodoma. Mji huu umeshakuwa mkubwa na tumeshaanza kupata shida kwenye hizi barabara. Leo hii kama wanafikiria mambo ya mabasi yaendayo kasi hiyo mipango ianze sasa, siyo ifikie wakati tuanze kubomoa nyumba za watu, itakuwa ni aibu. Tufanye sasa, kama kuna madaraja wa-plan sasa hivi ili baadaye isije ikatokea bomoabomoa. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sipendi kuzungumza maneno mengi kwa sababu siasa ya Kilolo ni barabara. Waheshimiwa Wabunge wanashindwa hata kufanya ziara sehemu nyingine kwa sababu barabara zimeharibika. Unapokwenda kule unaulizwa habari ya barabara na uliahidi kutengeneza barabara unajisikia aibu. Kwa hiyo, tutengenezeeni barabara twende majimboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.