Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwa kusema hivi, mwaka jana, mwaka juzi na miaka mingine yote iliyopita tumezungumza hapa kuhusu uwanja wa ndege wa Mkoa wa Mara. Tumesema, tumesema, tumeonesha umuhimu wa huu uwanja ukilinganisha na viwanja vingine ambavyo vimetengewa mabilioni ya pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu uwanja ni muhimu kwa Taifa hili kwa sababu Mbuga ya Serengeti yote unayoijua iko Mkoa wa Mara, ambayo ndio inayoingiza watalii wengi kuliko sehemu nyingine yoyote ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikia mtu ametoka Ulaya anasema anakwenda Serengeti, mambo ya Ngorongoro na mambo mengine huwa yanafuata baadaye, lakini kichwani kwa watu wanaotoka nje mara nyingi wanasema wanakwenda Serengeti, tumeimba hatusikilizwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ndio mkoa ambao anatoka Mwalimu Nyerere, niliwaambaia hapa wakati fulani, lakini hatusikilizwi. Pesa zinachukuliwa, tena zingine haziko hata kwenye utaratibu wa kibajeti, hazijapitishwa na Bunge hili zinapelekwa kwenye maeneo ambayo hayana muunganiko wa kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Mkoa wa Mara ni watu wa misimamo na wanaona mnayoyafanya. Ukichukua barabara za Mkoa wa Mara kwa mfano ukaangalia barabara ya lami tuliyonayo mkoa mzima wa Mara ni barabara inayotoka Mwanza kwenda Sirari, iliyojengwa miaka ya 90 na kitu, hakuna barabara nyingine yoyote ya lami ambayo tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiwaeleza ni kama wametutupa, lakini mali inayotoka Mkoa wa Mara inachangia pesa nyingi sana kwenye pato la Taifa. Nafikiri ni lazima Mawaziri waangalie haya mambo ya msingi yanayohusu maisha ya watu wa Mkoa wa Mara. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nizungumze kuhusu ufufaji wa ATCL na kila mara tunapozungumza hapa watu wanafikiri sisi tunapinga nchi hii kununua ndege. Hakuna mtu miongoni mwetu anayepinga tusinunue ndege, hakuna mtu miongoni mwetu anayekata tusifufue shirika letu la ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosema, kama tulivyosema wakati wa makinikia, kama tulivyozungumza wakati ule walikuja hapa wakatuambia kwamba tunaletewa trilioni 450, tunazisubiri hapa. Tuliwashauri humu, wakatuzomea, tuliwaambia wao ndio walioliingiza Taifa hili kwenye matatizo makubwa ya mikataba mibovu wakasababisha nchi hii inaibiwa na wazungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye wakaja hapa wanatunga sheria, tunawashauri njia ya kwenda nayo hawakusikia, wakatubandika majina ooh vibaraka wa wazungu, sijui vibaraka wa mabeberu. Sasa wao wenyewe aibu yao, hakuna pesa hata Sh.100 hata ile ya bia kishika uchumba haijaja ile ya balimi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndivyo tunavyowashauri kwenye shirika hili la ndege tunawaeleza kwamba tusiende kununua ndege za nchi hii, mali ya Watanzania wote kama mtu unakwenda kununua machungwa ya nyumbani, kwako bila kushirikisha Bunge, bila kushirikisha bajeti ya Taifa hili, bila kufuata mipango na mikakati ya maendeleo ya nchi hii, hawataki kusikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaaambia hasara ambazo watasababisha kwa kununua ndege kwenye mashirika tofauti tofauti na utengenezaji wake na service yake itakavyokuwa ngumu, hawataki kusikia. Sasa leo na hapo Waziri atakuja ajibu, hatujui kama ni kwa mistake au ni kwa makusudi ATCL, ukaguzi wa CAG umefanyika lakini performance yake haijakaguliwa, performance audit haijakaguliwa, tunataka tujue kwamba pesa zilizochukuliwa ni kiasi gani na...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOHN W. HECHE: Shukrani sana.