Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi. Kazi inafanyika na naomba niungane na wenzangu waliotangulia kutoa neno la kushukuru kwa kazi ambazo zinaendelea kufanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo kimsingi ambayo niliomba nichangie ili kuweza kuona namna ambavyo watu wa Wizara ya Ujenzi wanavyoweza kuendelea kusukuma baadhi ya kazi ambazo tayari zimeshaanza na zimeshaanzishiwa utaratibu wa kukamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo nataka nilizungumze ni kuhusu suala la barabara ya Masasi kwenda Nachingwea. Barabara hii nikisoma katika ukurasa wa 148 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, wameeleza na wameonesha kiasi cha fedha ambacho wamekitenga jumla ya bilioni tano na hii ni nyongeza ya fedha shilingi bilioni moja na milioni 500 kutoka ile bajeti ambayo wamei-carry forward kutoka bajeti ambayo tumeimaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Nachingwea, Masasi na maeneo yote ambayo wananufaika na barabara hii, naomba nitoe neno kwa sababu ni hatua kubwa ambayo kimsingi tumeipigania kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia iko barabara ambayo inatoka Nanganga kwenda Ruangwa na inaenda kuunganisha na Wilaya ya Nachingwea. Nayo pia nimeona katika ukurasa huo huo wa 148 na ukurasa wa 208 imetengewa shilingi bilioni tano pia kwa maana fedha hii ikipatikana utaratibu wa kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami utafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeona milioni 800 katika kuanza utaratibu wa kufanya feasibility study kutoka Nachingwea kwenda Liwale. Haya yote ni mambo ambayo kimsingi mwanzo hatukuwa nayo, lakini Wizara wameonesha kwamba sasa wanayo nia ya kuanza kufanyia kazi barabara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kusema hayo, nimwombe sana Mheshimiwa Profesa Mbarawa, nimekuwa na yeye, nimekuwa nafuatilia kwake kwa karibu sana juu ya umuhimu wa kuanza kujengwa kwa hizi barabara. Ni muda mrefu sasa tumeahidiwa kwamba anatafutwa mkandarasi ambaye ataanza kufanya kazi, lakini mpaka sasa hivi kazi bado haijaanzwa na nimeendelea kufuatilia kupitia Wizarani kuona ni lini kazi hii na fedha hii ambayo tumetengewa itaenda kufanya kazi ili tuweze kutatua changamoto ya barabara ambayo kimsingi tumeipigia kelele kwa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii pamoja na kwamba ni ya muda mrefu ya kutoka Masasi kwenda Nachingwea barabara hii bado taratibu na speed yake kidogo inatutia mashaka sisi ambayo tayari tumeshawaelekeza wananchi wetu kwa majibu ambayo tumepewa kwamba itaanza kujengwa. Kwa hiyo, kupitia hotuba ambayo utakwenda kuhitimisha Mheshimiwa Profesa Mbarawa tunaomba atupe maelezo na haya ni maelezo ambayo wananchi wa Jimbo wanapenda kuyafahamu. Ni lini hii barabara hasa itaanza kwenda kujengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu ni ahadi ambayo kimsingi sasa ni kama tayari watu imeshaanza kuwachosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kidogo nipate ufafanuzi kuhusu barabara hii ya Nachingwea kwenda Masasi, ilikuwa inasomeka ni barabara ya Nachingwea - Masasi - Nanganga, lakini nikisoma kwenye hii hotuba barabara hii sasa naona kama kuna kitu kinaondolewa. Jumla ya barabara hii kwa bajeti ya mwaka jana ambayo walitupitishia ilikuwa inasomeka kilometa 91, lakini sasa hivi kuna kilometa 41 ya kutoka Masasi kwenda Nachingwea tu, Nanganga haizungumzwi na sasa hivi tunaizungumza barabara ya kutoka Ruangwa - Nanganga - Nachingwea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii ya katikati sijajua nini kimetokea hapo kwa sababu hii yote ni barabara moja. Ningependa kuwakumbusha watu wa Wizara, kama wamesahau basi ni vizuri tukarekebisha hili jambo kwa sababu tayari linatupa shida kutoa tafsiri sahihi ya barabara hii kama ambavyo tulianza ule mchakato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naomba pia nichukue nafasi hii kuwakumbusha watu wa Wizara ya Ujenzi, pamoja na kuunganisha hizi barabara ambazo nimezitaja, bado tunaona umuhimu wa kutengenezewa barabara ya kutoka Nachingwea kupitia Ruangwa Mjini kwenda Namichiga kwenda kutokea Kiranjeranje. Barabara hii ina urefu wa takriban kilometa 107.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana, barabara hii ndiyo itakayounganisha watu wanaotoka Tunduru, watapita Masasi, wanakwenda Nachingwea, wanatokea Ruangwa wanaenda kutokea Kiranjeranje, tayari kwa kwenda Dar es Salaam, hakutakuwa na sababu ya kupita Lindi Mjini na maeneo yale ambayo kimsingi tutakuwa tumepunguza umbali mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii sisi katika ngazi ya mkoa tayari tumeshaizungumza na tumeshaipitisha. Kwa hiyo, tunaomba watu wa Wizara katika bajeti yao wakumbuke kwamba kuna hii barabara na bado ni barabara muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambayo ningependa pia kuwaomba watu wa Wizara na Mheshimiwa Kwandikwa tulishazungumza juu ya hii barabara na mwenyewe ameshafika, amefanya ziara katika wilaya yetu ya Nachingwea. Tunayo barabara ya kutoka Nachingwea kwenda Kilimarondo kutokea Lumesule. Kwa ngazi ya Mkoa kupitia TANROADS tayari tumeshafanya taratibu zote za kuipandisha hadhi. Tulichokuwa tunaomba katika mipango ya Wizara, barabara hii iingizwe katika utaratibu wa kufanyiwa kazi ili tuweze kufungua mawasiliano kati ya Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka nizungumzie ni eneo la mawasiliano. Mheshimiwa Nditiye nimekwenda sana kwake, lakini pia naomba nimwombe, kazi niliyomfanyia nikiwa Kibondo nami pia naomba alipe fadhila awafanyie kazi watu wa Nachingwea. Tarafa ya Kilimarondo ambayo inajumuisha Kata za Kiegei, Matekwe, Mbondo, hizi kata kwa muda mrefu hazina mawasiliano ya mtandao wa simu, nimeshapeleka haya majina kwako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana ndugu yangu, kaka yangu, watu hawa wameteseka kwa muda mrefu sana wanahitaji mawasiliano. Sasa hivi wanatumia TTCL tu na TTCL hii toka mwezi wa 12 mpaka sasa hivi mawasiliano bado wananchi wale kule wanatumia message tu simu hazitoki. Tunaomba atusaidie katika Mfuko huu wa Fursa sawa wa Mawasiliano, aweze kututengea utaratibu wa kuweza kupata mawasiliano na kampuni nyingine ili tuweze kuwaunganisha hawa watu wa tarafa pamoja na wilaya nzima ya Nachingwea ili tuweze kuboresha uchumi wa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo ningependa kulizungumzia ni eneo la hawa wenzetu wa TARURA. TARURA wamefanya upembuzi yakinifu juu ya ukarabati wa barabara zinazozunguka Jimbo la Nachingwea. Kwa Mwaka wa Fedha uliopita waliomba bajeti ya bilioni moja karibu na milioni 300, lakini fedha ambayo ilitoka ni almost bilioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bilioni moja hii, milioni 750 imetumika tu kwa ajili ya kulipa madeni ya Mwaka wa Fedha uliopita. Fedha iliyobaki milioni 300 ndiyo ambayo imetumika kutengeneza barabara na itakayotumika, kitu ambacho bado kwa mtandao wa barabara wa Wilaya ya Nachingwea, fedha hii ni ndogo sana na umuhimu wa Wilaya ya Nachingwea unafahamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nachingwea sasa hivi tunazalisha korosho, ndani ya Mkoa wa Lindi ndiyo tunaongoza, lakini mtandao wa barabara ni mbovu na hauwezi kuhimili taratibu zozote za kuweza kusafirisha mazao kutoka eneo moja kwenda eneo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri katika utaratibu wa fedha ambao wanaenda kuugawa, katika bajeti ya fedha ambayo wameitoa pamoja na kutoa ceiling ya mwaka uliopita, tumeomba jumla ya bilioni tatu, lakini mpaka sasa hivi kiasi ambacho wame-approve bado Wilaya ya Nachingwea hawajatoa hata shilingi moja. Tunashindwa kujua dhamira yao hasa ni nini katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio lazima Wabunge wote tukisimama hapa tuongee kwa kutokwa mapovu, tunaona umuhimu wa kuzungumza kwa lugha laini ili tuweze kuelewana kwamba keki ya Taifa hili tugawane katika misingi ambayo inalingana. Haipendezi kuona maeneo mengine wanapata fedha, barabara zao hazina umuhimu mkubwa sana, lakini maeneo mengine barabara zao hazipati fedha kama ambavyo sisi tumekuwa tunalilia. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze anatupatia shilingi ngapi kwa ajili ya kukarabati barabara ndani ya Jimbo la Nachingwea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.